Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye (kushoto) akiagana na wajumbe wa
Mkutano Mkuu wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata),
baada ya kuufungua mjini Morogoro jana.
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amewatahadharisha
Watanzania kuwa makini na watu wanaotaka madaraka kwa kugawa fedha
katika sehemu mbalimbali za nchi au majimbo akionya wanaweza kujikuta
wakimweka madarakani kiongozi anayejihusisha na biashara ya dawa za
kulevya.
“Hivi kama mtu anaweza kuhonga sehemu kubwa ya
wapigakura katika jimbo la uchaguzi au hata katika nchi kama nafasi
anayosaka ni urais; tumeshajiuliza hizo fedha nyingi hivyo anapata wapi?
Kama anajihusisha na biashara hizo chafu akipata nafasi hiyo watoto
wetu watapona?” alisema Sumaye jana na kuongeza:
“Haya ni maswali muhimu ya kujiuliza tunapoelekea
mwaka kesho kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2015 wakati wa
Uchaguzi Mkuu.”
Alisema hayo mjini Morogoro kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata).
Akizungumza kwa tahadhari alisema haizungumzii
Serikali yake iliyoko madarakani wala mtu yeyote, bali tabia mbaya,
Sumaye alisema biashara ya dawa za kulevya inahusisha fedha nyingi na
mitandao mipana ambayo isipodhibitiwa inaweza kulitumbukiza taifa katika
janga.
Alisema Katiba Mpya siyo mwarobaini wa matatizo
yanayolikabili taifa bali, utekelezaji na usimamizi wa sheria na kwamba
jambo muhimu ni kuwa na Serikali itakayosimamia na kutekeleza sheria ili
kulinda yale yaliyoelekezwa katika Katiba.
“Katiba haiwezi kumzuia mwizi kwenda kuiba na
sheria haitamzuia mwizi kwenda kuiba ila itatamka adhabu ya kupewa huyo
mwizi. Kwa hiyo ili vyote hivi viwe na maana ni lazima awepo mtu au
chombo cha kumkamata huyo mwizi na kumfikisha katika mikono ya sheria na
chombo hicho ni Serikali. Kama haiwezi kufanya hiyo kazi kwa ukamilifu
tutaishia kulalamika tu na maonevu na maumivu yataendelea kuumiza
jamii.”
“Kwa hiyo hata Katiba iwe nzuri namna gani na
ikatamka kuwa rushwa ni adui wa haki na hata ikatoa adhabu kali sana kwa
kosa hilo; kama tutaweka viongozi madarakani kwa rushwa, hiyo Katiba
wala haitatusaidia. Hivyo Katiba nzuri mpya lazima iambatane na Serikali
safi yenye kusimamia masilahi ya umma. Huwezi kumweka madarakani
mwenyekiti wa kijiji au diwani au mbunge au hata Rais kwa rushwa ya
kuwanunua wapigakura halafu utegemee Katiba Mpya itajibu matatizo ya
jamii.”
Azungumzia Mviwata
Sumaye alisema Mtandao huo wa Wakulima Wadogo
Tanzania ndiyo unaojua tatizo la kilimo na shida zao na ndiyo unaotakiwa
kuulizwa cha kufanya ili kilimo chetu kibadilike na mkulima afaidike...
“Kama hatuwahusishi na kuwashirikisha katika sera,
mipango na programu za kilimo, basi tujue kuwa sera, mipango na
programu hizo zitashindwa.”
Alisema Tanzania ni nchi ambayo wananchi wake
wengi wanategemea kilimo kwa maisha yao na uchumi wa taifa pia kwa kiasi
kikubwa hutegemea sekta hiyo, lakini bado ni duni na hakijamkomboa
mkulima mwenyewe wala uchumi wa taifa... “Nchi na watu wake bado ni
maskini pamoja na kuwa watu wachapakazi wapo na ardhi kubwa na nzuri
yenye rutuba ipo.”
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Alisema suala la usindikaji wa mazao lazima lipewe kipaumbele vinginevyo kilimo hakitamwondoa mkulima katika umaskini.
“Kama tutaendelea kuuza mazao ghafi ambayo bei
yake katika masoko ya nje ni duni na haitabiriki, basi wakulima wetu na
uchumi wa taifa letu vitazidi kudidimia. Mazao yaliyoongezwa thamani kwa
usindikaji yanapata bei nzuri na usindikaji nao pia hutoa ajira kwa
watu wetu.”
“Kwa mfano, badala ya kuuza pamba ghafi
tubadilishe pamba yetu kuwa nyuzi na vitambaa, katani yetu iwe katika
kamba na mazulia, chai na kahawa ziwe katika paketi za kutumia, matunda
yasindikwe katika makopo na kadhalika. Kwa msaada wa Serikali yetu,
Mviwata inaweza kabisa kufanya kazi hii ama peke yake au kwa
kushirikiana na wadau wengine wa uwekezaji ili kujenga viwanda vya
usindikaji mazao. Tusiisubiri Serikali peke yake haitaweza na
tutajichelewesha.”
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment