JESHI la Wananchi, Polisi, Uhamiaji na vyombo vingine vya
usalama pamoja na baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara maarufu nchini
wametajwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya ambayo
imeharibu maisha ya maelfu ya vijana na kuvunja vunja familia.
Taarifa za kuhusika huku kwa maofisa wa vyombo hivi vya usalama na
watu mashuhuri zimekuja baada ya Mtanzania mmoja kukamatwa huko Hong
Kong na kuandika barua ya kukiri kuhusika kwake na biashara hiyo pamoja
na kuwataja watu waliomuingiza na kumwezesha kufanya biashara hiyo.
Barua hiyo ilipostiwa katika mojawapo ya tovuti zinazofuatilia mambo
ya dawa za kulevya na kubandikwa chini ya kichwa cha habari cha “Punda
wa Madawa” kwenye mtandao wa waumini wa Kanisa Katoliki ambao umeundwa
ili kuunga mkono mabadiliko na mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa
Vatikano.
“Punda wa Madawa” ni jina linaloelezea watu wale wanaotumiwa na
kutumika kusafirisha dawa za kulevya kutoka kwa wafanyabiashara wa
jumla kwenda kwa wafanyabiashara wa reja reja. Watu hawa wanaweza kuwa
ndani ya nchi au kati ya nchi na nchi.
Mara nyingi – kama jina linavyoashiria – watu hawa ni vyombo tu vya vinara wa dawa za kulevya na lolote litakalowakuta huwa ni juu yao wenyewe. Hata hivyo, endapo wanafanikiwa kusafirisha ‘mzigo’ kutoka pointi moja kwenda nyingine basi huweza kulipwa vizuri na wengine huishi maisha ya kifahari kabisa kutokana na biashara hii.
Mara nyingi – kama jina linavyoashiria – watu hawa ni vyombo tu vya vinara wa dawa za kulevya na lolote litakalowakuta huwa ni juu yao wenyewe. Hata hivyo, endapo wanafanikiwa kusafirisha ‘mzigo’ kutoka pointi moja kwenda nyingine basi huweza kulipwa vizuri na wengine huishi maisha ya kifahari kabisa kutokana na biashara hii.
Kabla ya kuwataja watu ambao mwandishi anawatuhumu kujihusisha na
biashara hii, anaelezea kwa kirefu jinsi alivyoingia katika mtego wa
biashara hiyo na hatimaye kuangukia kwenye mikono mikali ya sheria ya
polisi wa Hong Kong, China.
Mwandishi anaelezea aliingia katika biashara hiyo baada ya shida za
maisha kumzidia na kujikuta hana njia ya kupata kipato kingine halali
ili kuisaidia familia yake.
“Pamoja na misukosuko yote hiyo nilivumilia, lakini mtihani mkubwa ni
pale kodi ya nyumba ilipoisha na mwenye nyumba akanipa ‘notice’ ya
mwezi mmoja (nihame), au nimpe kodi ya miezi ya 360,000 tsh,” ameelezea
mwandishi huyo ambaye hakuweka jina lake.
Mwandishi huyo wa barua anadai kuwa baada ya kujitahidi kutafuta
fedha hiyo na kushindwa, alijikuta ameomba msaada kwa marafiki zake
ambao anawaita ‘wabaya’ kwani ni wao ndio walimchukua na kumpeleka kwa
bosi wao ambaye alimlipia kodi ya miezi sita na kumpa fedha za ziada
shilingi laki mbili. Tajiri huyo ni mtu anayeishi Magomeni Mwembechai
jijini Dar es Salaam.
Ni hapo ndipo alipoanza kupewa mazoezi ya kumeza vidonge vya heroine.
Siku chache baadaye alipewa vidonge 93 vya dawa hizo ambavyo kila
kimoja kina gram 15 kwa jumla ya gram 1,395 (sawa na paundi tatu hivi).
Kutokana na kuanza kupata matatizo na kutoka vidonda, kijana huyo alijaribu kutaka kuacha biashara, lakini akakumbushwa kuwa ana deni la sh 560,000 na upande mwingine aliahidiwa kuwa endapo angefikisha mzigo ule salama basi angelipwa dola 5,000. Akapewa mpango wa safari kwenda Hong Kong akiwa katika hali ya udhaifu mkubwa wa mwili.
Kutokana na kuanza kupata matatizo na kutoka vidonda, kijana huyo alijaribu kutaka kuacha biashara, lakini akakumbushwa kuwa ana deni la sh 560,000 na upande mwingine aliahidiwa kuwa endapo angefikisha mzigo ule salama basi angelipwa dola 5,000. Akapewa mpango wa safari kwenda Hong Kong akiwa katika hali ya udhaifu mkubwa wa mwili.
Mwandishi alitarajia akamatwe uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere
jijini Dar es Salaam. Haikuwa hivyo na kwa maelezo yake kijana huyo
anasema: “Ajabu pale airport kulikuwa na mtu ambaye aliandaliwa
kunipitisha mimi mpaka boarding room.” Ilikuwa ni hali aliyokuwa nayo
ndiyo iliwafanya maofisa wa Hong Kong kumtilia shaka na kumweka
kizuizini.
Kitu ambacho mwandishi inaonekana hakuwa anakijua ni kuwa Hong Kong
hawana huruma na watu wanaojihusisha na dawa za kulevya kwani wana
vifungo vikali kabisa na kwa maelezo yake kuwa hadi hivi sasa kuna
vijana wa Kitanzania karibu 150 ambao wameshafungwa na wengine
wakiendelea kusubiri kesi zao ziendelee.
Alichoshukuru mwandishi ni kuwa angalau yeye na wenzake wamekamatwa Hong Kong kwani kama wangekamatwa China yenyewe basi wangenyongwa kwani tayari – kwa maelezo yake – wapo vijana wa Kitanzania walionyongwa huko.
Alichoshukuru mwandishi ni kuwa angalau yeye na wenzake wamekamatwa Hong Kong kwani kama wangekamatwa China yenyewe basi wangenyongwa kwani tayari – kwa maelezo yake – wapo vijana wa Kitanzania walionyongwa huko.
Kwa maelezo yake ambayo yanashabihiana kwa kiasi kikubwa na taarifa
za vyombo vya usalama vya kimataifa vinavyofuatilia biashara hii haramu
mizigo ya dawa za kulevya yanaingia nchini Tanzania yakitokea
Pakistani na Afghanistan kupitia maeneo ya Tanga, Dar es Salaam, Mtwara
na Bagamoyo ambazo huja kwa boti na kupokelewa na wahusika wakubwa
nchini.
Mwaka jana mtoto mmoja wa aliyekuwa afisa wa Benki Kuu ya Tanzania
alikamatwa na wenzake huko Lindi akiwa na mzigo wa dawa za kulevya
wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 9.
“Mizigo hiyo huwa inasindikizwa na magari ya jeshi na polisi na hii
siyo siri kwani hata wahusika wanajua,” anasema kijana huyo.
Kuhusishwa kwa vyombo vya usalama na biashara hii haramu si jambo la
kushangaza. Ipo mifano ya baadhi ya watumishi wa vyombo vya usalama
waliokamatwa:
- Mwaka 2011 – Mwanajeshi wa JWTZ alikamatwa mjini Morogoro akijaribu kusafirisha magunia 12 ya bangi kutoka Iringa kuja Dar es Salaam. Hii ilikuwa ni mwezi Desemba mwaka huo. Kijana huyo wa miaka 26 alikamatwa na askari polisi waliokuwa doria akiwa amevaa sare za jeshi hilo. Ni ofisa wa Kambi ya Lugalo mwenye namba MT86879.
- Januari 2013 – Ofisa wa JWTZ mwenye namba MT 59503 Sajenti Aziz Athumani alikamatwa huko Arusha akiwa na pembe mbili za ndovu.
- Aprili 2013 - Askari wa Magereza Brighton Octavian alikamatwa katika gereza la Keko akiwa na kete 732 ambazo inadaiwa alikuwa anazipitisha kwenda kwa wafungwa. Kuna ushahidi mkubwa wa uwepo wa mtandao wa kihalifu wa maofisa wa Magereza ambao wamekuwa wakitumiwa na wafungwa kupeleka habari nje au ndani kutoka kwa mabosi wa dawa za kulevya nchini.
- Julai 2013 – Hivi majuzi tu mwanajeshi mwingine Seleman Chasama (50) katika hali ya kushangaza akili kabisa, amefikishwa mahakamani akishitakiwa makosa ya uhujumu uchumi na yale ya uhifadhi wa wanyama pori baada ya kukutwa na pembe 357 za ndovu zenye thamani ya dola milioni 2.6.
- Julai 2013 – Maofisa waandamizi wa Jeshi la Magereza akiwemo Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Joseph Sauli, Warden Richard Barick na Koplo Silvester Bukha walikamatwa na twiga wawili, pundamilia wawili, swala palapala wawili na mbuni wawili, wote wakiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 55.
Hiyo ni mifano michache tu ya kuhusishwa kwa maofisa wa usalama na
mambo ya ujangili, dawa za kulevya na hapo hatujaangalia uhalifu
mwingine. Na hapa izingatiwe hawa ni wale ambao walikamatwa tu na
hatujaangalia wale wa polisi ambao kama watu wanakumbuka waliwahi
kutuhumiwa kujaribu kumtegeshea mtoto wa Mzee Mengi dawa za kulevya
pale Uwanja wa Ndege na barua hii inatupa mawazo tu jinsi gani hilo
linaweza kutokea kweli.
Ikumbukwe barua hii imekuja tayari kukiwa na habari za mabinti wawili
wa Kitanzania wamekamatwa Afrika Kusini baada ya kutua nchini humo na
mzigo wa dawa za kulevya wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6;
na hawa waliondokea Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es
Salaam. Bila ya shaka kuna kuhusika kwa maofisa wa kikosi cha Uhamiaji
ambao wana wajibu wa kusimamia watu wanaoingia na kutoka nchini.
Vilevile, barua hii imekuja siku chache tu toka Mbunge wa Musoma
Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA) kuzungumza na waandishi wa habari
kutaka serikali ijisafishe kwani inaonekana kuwaogopa vinara wa dawa za
kulevya. Katika tamko lake la Julai 19 Nyerere ambaye pia ni Waziri
Kivuli wa Mambo ya Ndani alisema kwa ukali kuwa;
“Kupuuzia na kutochukua hatua kwa wahusika wa dawa za kulevya ni
kuangamiza nguvu kazi ya taifa ambayo ikishaharibiwa na dawa za kulevya
hatuna taifa tena. Hivyo serikali ifahamu kwamba kuendelea kulifumbia
macho jambo hili kwa manufaa ya mafisadi wachache ni kulihujumu taifa
na huo ni usaliti dhidi ya kiapo ilichokula cha kulitumikia taifa na
kusimamia ustawi wa wananchi wa Tanzania.
“Aidha, serikali itambue pia kwamba kuendelea kukaa kimya bila
kuchukua hatua yoyote juu ya jambo hili kunatoa dalili kwamba yamkini
na yenyewe inahusika na biashara hiyo.”
Katika kuhitimisha barua yake, mwandishi wa barua hiyo alienda mbali
na kuwataja baadhi ya watu ambao wanahusika na mtandao wa dawa za
kulevya na namna ya ushiriki wao huku akisema kuwa wapo wengine ambao
majina yao yakitajwa nchi itashituka kwani ni watendaji wa ngazi za juu
serikalini. Barua yake hiyo ilitumwa kwa vyombo mbalimbali vya habari
vya Tanzania.
Kitu kimoja ambacho kiko wazi ni kuwa kijana huyo amefanya kile ambacho watu wengi wameshindwa kukifanya.
Kukithiri kwa biashara hii nchini kunafichua tu kundi ambalo
limejikita kwenye madaraka, ambalo licha ya kufanya vitendo vya ufisadi
serikalini lipo pia kwenye mtandao wa uhalifu (organized crime) na
limejipenyeza hadi kwenye vyombo vya dola.
Barua ya kijana huyu kuhusisha vyombo vya usalama yaweza kuwa ni
andiko la mwisho kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuangalia utendaji
wa vyombo vyake ambavyo anaonyesha kuwa anaviamini sana.
Je, serikali itapokeaje taarifa hii? Je, kuna mtu mwenye ujasiri wa
kupambana na kuufumua mtandao huu? Je, kama kijana huyu kawataja majina
na mahali je, Serikali ya Tanzania ina maana kuwa miaka yote hii
haikuwajua? Na Rais Kikwete anahalalisha vipi kuendelea kuwatumia watu
wale wale walioshindwa kusimamia usalama? Kama yaliyomo kwenye barua
hiyo ni kweli je, tunaweza kusema kweli nchi iko salama? Salama kwa
nani?
Maswali mawili ya kujiuliza na kufikirisha:
- Kwa kila dawa zinazokamatwa na kwa kila watuhumiwa wanaokamatwa ni wangapi wanafanikiwa kupita na kuishia mitaani au nchi jirani?
- Je, majina ya hawa waliotajwa yamo kwenye ile orodha aliyopewa Rais Kikwete, au ile ya viongozi wa makanisa au ile ya Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya? Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment