Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, amelivunja
baraza lake la mawaziri pamoja na kumfuta kazi makamu wa rais Riak
Machar katika mabadiliko makubwa zaidi kuwahi kutekelezwa katika
historia ya miaka miwili ya taifa hilo.
Aliyekuwa waziri wa habari, Barnaba Marial
Benjamin, ameiambia BBC kuwa mawaziri wote kutoka kwa Makamu wa Rais
Riek Machar wameondolewa.
Duru zinasema haijabainika iwapo
kuna waziri yeyote miongoni mwa wale waliofutwa kazi atarejeshwa katika
baraza jipya la mawaziri litakalobuniwa.
Pia hakuna sababu iliyotolewa kuhusiana na hatua
ya Rais kuwafuta kazi maafisa hao, lakini wadadisi wanasema kuwa Bwana
Kiir na makamu wake Machar wamekuwa na mgogoro wa mamlaka kwa miezi
kadhaa sasa.
Sudan Kusini imekumbwa na matatizo chungu nzima hasa ya kiuchumi tangu kujitenga na Sudan mwaka 2011.
Uthabiti wake umetatizwa na malumbano kati yake na Sudan kuhusu mipaka na swala la mafuta.
Hivi karibuni baadhi ya maafisa wa Bwana Kiir, wamekuwa wakizungumzia kuwepo minong'ono kuhusu uongozi wake.
Ripoti zinasema kuwa Kiir anajitahidi kusalia na
ushawishi katika chama cha Sudan People's Liberation Movement (SPLM),
ambacho kinathibiti serikali.
Kwa upande wake bwana Machar, ambaye mwezi
Aprili alipunguziwa mamlaka, alisema huenda akagombea uongozi wa chama
cha SPLM dhidi ya rais Kiir, kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka
2015.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment