Freeman Mbowe
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Freeman Mbowe, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya
kutoa kauli za uchochezi dhidi ya jeshi hilo, vyombo vya dola na
serikali kwa ujumla.
Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa na Msemaji wake, Mrakibu Mwandamizi,
Advera Senso, imesema kuwa Mbowe amekuwa akitoa kauli ambazo zimekuwa
na mlengo wa uchochezi na kuijengea jamii taswira hasi juu ya vyombo vya
ulinzi na usalama na kuwafanya wananchi kuwa na hofu.
Mbowe akiandamana na mawakili, Nyaronyo Kicheere na Peter Kibatara,
alijisalimisha mwenyewe makao makuu ya polisi majira ya saa 8:30 mchana,
mara tu baada ya kuwasili jijini kutoka safarini.
Hatua hiyo imetokana na kitendo cha polisi juzi usiku wa manane
kuvamia nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na walipomkosa waliacha
namba ya simu ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ili
ajulishwe kwamba anahitajika.
Aidha, jana askari wengine kutoka Polisi na wengine wanaoaminika kuwa
ni wa Idara ya Usalama wa Taifa walikwenda katika hoteli moja mjini
Moshi walikoamini kwamba kiongozi huyo amejificha kwa nia ya kumkamata
lakini hawakuambulia kitu.
Hata hivyo, wakati Mbowe akishikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma hizo,
wenzao wa Mkoa wa Dar es Salaam wamedai polisi hawawezi kusumbuka
kumkamata kiongozi huyo kwa mambo ya kisiasa.
Naibu Kamishina wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Ally Mlege, aliwaambia jana jijini Dar es Salaam waandishi wa habari
kuwa polisi hawawezi kujiingiza katika malumbano ya kisiasa baina ya
vyama hivyo viwili.
“Hatuna kauli yoyote kuhusu mivutano ya kuanzisha na kuendesha vikosi
vya ulinzi na usalama inayoendelea ya kisiasa kati ya CCM na CHADEMA,
jamani hayo ni mambo ya kisiasa,” alijibu Mlege.
Mbowe amehojiwa kutokana na uamuzi wa Kamati Kuu ya CHADEMA kutaka
kuanzisha kikosi cha vijana cha ulinzi cha Red Brigade na kauli ya
kulituhumu jeshi hilo kumjua aliyehusika na bomu lililorushwa kwenye
mkutano wa CHADEMA jijini Arusha na kuua watu wanne.
Mwenyekiti huyo pia anahojiwa kwa madai ya kulituhumu Jeshi la Polisi
kuisaidia CCM katika uchaguzi mdogo wa madiwani Arusha, pia madai ya
kutoa kauli kwamba kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kukaa kimya kuhusiana
na mauaji hayo, kunaonesha dalili za serikali kujua nani alihusika na
tukio hilo.
Tuhuma nyingine ni madai ya kuhamasisha chuki kati ya jeshi na wananchi, pia kuchochea wakazi wa Mtwara katika sakata la gesi.
Mbowe ambaye alihojiwa takriban kwa saa tano, aliachiwa kwa dhamana na
anatakiwa kuripoti tena Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Julai 23, saa 8
mchana.
Kauli ya CHADEMA
Kufuatia tukio hilo, CHADEMA wamesema kitendo cha kumkamata kiongozi
huyo kimedhihirisha wazi kuwa serikali ya CCM imeshindwa kuongoza nchi
kwa mujibu wa sheria.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema hatua
ya serikali ya kuwafungulia wapinzani tuhuma za uchochezi kwa kusema
ukweli haina tofauti na vitendo vya serikali ya kikoloni iliyomkamata na
kumfungulia mashitaka Mwalimu Julius Nyerere tuhuma kama hizo.
“CHADEMA kama ilivyokuwa TANU, tunashinda. Jeshi la Polisi ambalo
askari na maofisa wake ni watuhumiwa wa mauaji si tu ya bomu na risasi
Arusha, bali hata ya Mwangosi na mauaji mengine, isitumie madai ya
uchochezi kuidhibiti CHADEMA na viongozi wake.
“Polisi kumhoji Mbowe siku chache baada ya kauli za Kikwete alizotoa
kwenye mkutano wa TCD ni dalili kwamba wamesukumwa na mamlaka za juu
yao. Jeshi la Polisi limshauri Kikwete kama anaona CHADEMA inasema uongo
na uchochezi, basi aunde tume ya majaji ili ukweli ujulikane,” alisema
Mnyika.
CHADEMA imesema chama hicho kimekuwa kikisimamia ukweli kuhusu mauaji
yenye mwelekeo wa kisiasa tangu mwaka 2011, Arusha, 2012 Morogoro na
Iringa na 2013 mkoani Arusha.
“Vyombo vya dola vikiwa ni sehemu ya watuhumiwa, ukweli huo unaitwa uchochezi na kutukamata badala ya watuhumiwa wa mauaji.
“Alichokisema Mbowe ni maamuzi ya Kamati Kuu na kama wanaona ni
uchochezi basi wakamate wajumbe wote wa Kamati Kuu na wakishitaki
chama,” alisema Mnyika ambaye katika kumsindikiza Mbowe aliandamana na
Benson Kigaira na John Mrema.
Tendwa ashambuliwa
Katika hatua nyingine, CHADEMA imemshambulia vikali Msajili wa Vyama
vya Siasa, John Tendwa, kwa kile walichokiita ‘undumila kuwili’ kutokana
na suala zima la ulinzi wa vyama.
Taarifa iliyotolewa na John Mnyika alisema Tendwa katika Mkutano Mkuu
wa chama hicho Agosti 13, 2006, akiwa kama mgeni mashuhuri alibariki na
kukubaliana na mabadiliko ya katiba yaliyofanywa na chama hicho.
Alisema moja ya mabadiliko yaliyofanywa na kuungwa mkono kwa pongezi
na Tendwa ni uamuzi wa chama kuwa na chombo cha kulinda viongozi na mali
za chama kitakachoitwa Brigedi Nyekundu.
“Tendwa katika hotuba yake alipongeza mabadiliko hayo ya katiba na
ikasajiliwa katika ofisi yake mwaka 2006, baada ya kukubali kwamba
imekidhi mahitaji yote muhimu.
“Leo anapogeuka na kuwaacha polisi kuadhibu viongozi wetu kwa kile
alichokiunga mkono wakati ule ni jambo la kusikitisha sana na lenye
lengo la kufuata mkumbo wa kauli ya Kikwete na polisi badala ya
kuzingatia katiba na sheria za nchi.
Mnyika alisema badala ya Tendwa kuitishia CHADEMA ambayo haijavunja sheria, ingekuwa bora akakifuta Chama Cha Mapinduzi.
“Hiki kimevunja sheria katika chaguzi ndogo za Kiteto, 2007, Tarime
2008, Busanda na Biharamulo 2009, Uchaguzi Mkuu 2010, Igunga 2011,
Arumeru 2012 na za marudio kwenye kata 21, mwaka 2013 kote nchini.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukieleza kuhusu makambi ya Green Guard
yanayofanya mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kufanya mashambulizi na
matukio kwa Wanachadema na wanahabari.
“Mathalani mbali ya kushambuliwa CHADEMA, Green Guard ya CCM imewahi
kuwashambulia waandishi wa habari, Frederick Katulanda wa Mwananchi
mwaka 2010 katika kampeni za Uchaguzi Mkuu, Musa Mkama wa Dira ya
Mtanzania huko Igunga katika uchaguzi mdogo 2011, Munir Zacharia wa
Channel Ten huko Zanzibar katika uchaguzi mdogo wa Bububu na ushahidi wa
hayo upo,” ilimaliza taarifa hiyo.
Via Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment