Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa.
OFISI ya Msajili
wa Vyama Vya Siasa nchini imevitaka vyama vya siasa
kutii agizo la kutoanzisha kambi za mafunzo ya kulinda amani maarufu kwa
jina la mgambo kwa minajili ya kujilinda.
Kauli hiyo imetolewa na Rajab Juma
kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa kufutia Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kutangaza hivi karibuni kuwa kinakusudia
kuanzisha kambi za mafunzo ya kujilinda kwa vijana wake nchi nzima.
Taarifa ya ofisi hiyo imedokeza
kuwa Katiba ya nchi imempa jukumu kila mwananchi kulinda amani na
usalama wa nchi,pia kujilinda yeye mwenyewe na mali zake kwa kutoa taarifa
katika vyombo vya dola pale anaposikia au kuona mtu anataka kufanya au
anafanya uhalifu au amemdhuru mtu.
Amesema suala hilo lilitangazwa na
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na kuandikwa katika vyombo vya habari
kabla ya chama hicho, kuwasiliana na taasisi husika ikiwemo ofisi hiyo
ili kupata ushauri kuwa jambo wanalotaka kufanya ni sahihi .
Bwana Rajab amesema Katiba ya nchi na katiba za vyama vya siasa, hazina maana kila mwananchi au kikundi cha watu kufanya mafunzo ya kijeshi au ukakamavu ili
kufanikisha jukumu hili.
Bwana Rajab amesema kuwa kama CCM
wanakiuka sheria ni jukumu vyama
vingine au Mtanzania yeyote,kutoa taarifa na ikiwezekana na ushahidi katika
taasisi husika, ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa ili suala hilo
lishughulikiwe kisheria.
Taarifa ya msajili imefafanua kuwa
Jukumu la vikundi kama hivyo ni kutoa
taarifa kwa vyombo vya dola na si kupambana na wahalifu au watu wanaotaka kuwadhuru
kwani wenye jukumu la kupambana na wahalifu ni vyombo vya ulinzi na usalama
ambavyo vipo kisheria, mojawapo ikiwa ni Jeshi la Polisi.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment