Marekani imesema kuwa itachelewesha mpango wake wa
kuikabidhi Misri ndege za kivita aina ya F-16 huku mgogoro wa kisiasa
ukiendelea kutokota nchini Misri kufuatia kuondolewa mamlakani kwa
aliyekuwa Rais Mohammed Morsi.
Msemaji wa idara ya ulinzi nchini Marekani,
George Little alisema kuwa uamuzi huo ulifikiwa kutokana na hali
inayokabili Misri kwa sasa.
Marekani inadadisi ikiwa kuondolewa
mamlakani kwa Morsi ilikuwa mapinduzi ya kijeshi, hali inayoweza
kusababisha Marekani kusitisha msaada wake kwa Misri.
Hapo jana mkuu wa jeshi la Misri Generali Sisi ,
aliitisha maandamano ya umma akiwataka wananchi kuliruhusu jeshi
kukabiliana na kile alichokiita tisho la ugaidi.
Lakini Abdel Fattah al-Sisi aliongeza kuwa
hakuwa anaitisha maandamano kwa lengo la vurugu huku akiwasihi wananchi
kuwa na maridhiano.
Katika jibu lake kwa wito wa jeshi, chama cha
Muslim Brotherhood, ambacho kinamuunga mkono Morsi, kilisema kuwa
Generali Sisi alikuwa anaitisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ndege hizo nne aina ya F-16 ni sehemu ya ndege
nyingine 20 ambazo zimeitishwa, kati ya hizo nane tayari zikiwa
zimepelekwa Misri.
Hata hivyo Marekani iliahidi tarehe 11 mwezi Julai kuwa bado ina mpango wa kuikabidhi Misri ndege hizo.
Chanzo: BBC Swahili
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment