Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela
Rais mstaafu nchini Afrika Kusini, Nelson Mandela aliyelazwa hospitalini tangu tarehe nane mwezi Juni, anaonyesha dalili za afya yake kuimarika.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa serikali. Hata hivyo Mandela mwenye umri wa miaka 95 angali hali mahututi ambayo inadhibitiwa na madaktari.

Rais Jacob Zuma amewataka watu kuendelea kumuombea Mandela na kuwashukuru wale waliotenda mema kwa niaba ya Mandela.
Mandela ambaye ni rais wa kwanza wa nchi hiyo kuchaguliwa kidemokrasia, anatazamiwa na wengi kama baba wa taifa.

Alifungwa jela miaka 27 baada ya kuanzisha vita dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

Anajulikana na ukoo wake kwa jina Madiba, na alichaguliwa kama rais wa Afrika Kusini mwaka 1994 baada ya wazungu kumaliza utawala wao na kisha akaondoka mamlakani baada ya miaka mitano ya kutawala nchi.

Katika taarifa yake, bwana Zuma alitoa wito kwa wafanyabiashara kuunga mkono mradi unaofadhiliwa na wakfu wa Mandela kujenga hospitali ya watoto.

"Madiba anapenda sana watoto, na anawatakia afya nzuri. Anatutaka tuhakikishe kuwa wanaishi maisha mazuri katika siku za baadaye,'' alisema Zuma.

Wakfu wa Mandela , ungependa kujenga hospitali yenye uwezo wa kuwashughulikia watoto 238 wa kulazwa pamoja na kuwatibu watoto kote nchini Afrika Kusini.
Chanzo: BBCSwahili
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top