Na Mimi Mwanakijiji
Kwa mara nyingine tena Waziri Mkuu Pinda ametoa kauli ambayo
inatafsirika kuwa ni kuhalalisha vyombo vya usalama kuvunja haki za
msingi za wananchi kwa kuwapiga na hata kuwaua. Kauli hiyo iliyotolewa
leo Bungeni inatukumbusha sisi wengine kauli yake nyingine aliyoitoa
wakati mauaji ya Albino yamepamba moto pale alipoonekana kuhalalisha
wananchi kuchukua hatua mikononi. Inawezekana watu wengi wameshasahau
kauli ile. Akizungumza Bungeni Waziri Mkuu Pinda akionesha kuchoshwa na
mauaji ya Albino alisema hivi “Mkimuona mtu akamkata mwingine shingo
naye muueni kwani sasa viongozi wote tumechoka... no more, I can't
tolerate anymore (imetosha, siwezi kuvumilia tena” na hakuishia hapo
bali aliagiza Umoja wa Vijana wa Chama chake kutekeleza agizo hilo kwa
kuwaambia “Umoja wa vijana wa CCM mna jeshi zuri ambalo naamini mkiamua
mnaweza kutokomeza mauaji ya wazee wetu pmoja na ndugu zetu maalbno na
kazi hiyo nawaagiza muanze leo msisubri auawe mwingine tena”
Kitu ambacho Pinda hajakielewa na inaonekana hana uwezo wa kukielewa ni
kuwa hakuna binadamu anayependa kutendewa kama vile si binadamu. Hakuna
mwanadamu ambaye anaweza kuendelea kukubali kudharauliwa, kupuuzwa,
kunyanyaswa na kuteswa kwa vile tu wale wanaofanya hivyo wanaamini
wanauwezo wa kufanya hivyo. Kauli ya Pinda ni ushahidi wa yeye na wale
walioshangilia kutokujua historia.
Nimesoma baadhi ya michango
ya watu ambao wanaunga mkono kauli ya kipuuzi kama hii wakiamini
wanafanya hivyo wakiwakilisha jambo jema. Historia inao watu kama hao na
ni wengi wameenda na kusahauliwa katika giza la historia wakiamini
walikuwa wanatetea ‘uzalengo’ au ‘utaifa’. Ni vizuri kumkumbusha Pinda
na mashabiki wake kuwa binadamu ana kikomo cha kunyanyaswa, kupuuzwa na
kudharauliwa anapofika kwenye kikomo hicho (prespice) mwanadamu
atachukua hatua tu!
Uasi wa Watumwa wa Meli ya Amistad 1839
Meli ya Kihispania ya La Amistad ilibeba kundi la watumwa kutoka Afrika
ya Magharibi (Sierra Leone) na walikuwa wanaenda kuuzwa tena (kama
bidhaa) kwenye mojawapo ya nchi za Amerika. Watumwa wale walijitambua
kuwa wao ni binadamu na kuwa waliishi kama watu huru kabla ya kukamatwa
na kuuzwa utumwani. Hawakuwa wanajua mambo mengi ya watekaji wao lakini
walijua kitu kimoja - minyororo waliyofungwa ilikuwa ni minyororo siyo
tu ya kufunga mifupa yao bali pia kufunga fikra zao.
Julai 2,
1839 (miaka 174 iliyopita) Wakiwa njiani kuelekea kwenye soko hilo la
watumwa (Cuba) watumwa wale walikula njama wao wenyewe na kuasi na
kuwapiga wafanyabiashara wa utumwa na kuwalazimisha wawarudishe Afrika.
Lakini kiujanja manahodha badala ya kuipeleka meli Afrika wakati wa
usiku wakawa wanailekeza Kaskazini na lakini ikakamatwa na majeshi ya
Marekani na kulazimishwa kutia nanga Long Island, New York.
Kutoka Long Island kesi moja kali sana ya haki za binadamu ilifanyika
ambayo bado imeoneshwa katika filamu ya Amistad (1997) ya Steven
Spielberg. Swali kubwa lilikuwa je watumwa wale walipoamua kutumia nguvu
na hata kuua watekaji wao wakidai uhuru wao walifanya uhalifu? Na je
kuwa kwao Waafrika kuliwafanya wasiwe binadamu wenye haki?
Kesi
ilinguruma na hoja zilibishaniwa lakini mwisho wa siku Mahakama zote
zilizosikiliza kesi hii zilikubaliana kuwa Watumwa wale walikuwa ni watu
huru walipokamatwa na hivyo walikuwa na haki ya kupigania uhuru wao kwa
namna yoyote ile na hivyo uasi wao ulikuwa halali! Mahakama ikaruhusu
Waafrika wale kufanyiwa mipango ya kurudishwa kwao na fidia walipwe.
Waafrika wale hawakuhitaji kupewa elimu ya uraia kujua kuwa walikuwa
wanadhulumiwa na wala hawakuhitaji chama cha siasa kuwaongoza kukataa
dhulma! Hawa hawakuwa peke yao katika historia.
Uasi wa Meermin wa Madagascar 1766
Japo uasi wa Amistad unajulikana sana (labda kwa sahabu unahusisha
Marekani) lakini uasi mwingine wa Waafrika waliokataa kuchukuliwa
watumwa ulifanyika miaka 73 nyuma katika bahari ya Hindi. Meli ya
Meermin ilikuwa nimojawapo ya meli za Waholanzi zilizobeba watumwa na
ilikuwa imebeba watu wa Malagasy ambao walikuwa waende kuwa vibarua
kwenye mashamba ya kampuni ya Dutch East India Company huko kwenye jimbo
la Cape Africa ya Kusini. Watumwa wale wakaamua kuasi na wakafanya uasi
mkubwa kwelikweli; waliua nusu ya wazungu waliokuwemo mle na kuagiza
meli igeuze njia kuwarudisha Madagascar. Kama ilivyokuwa kwa Amistad
manahodha wakatumia ulaghai na kuielekeza meli Afrika y a Kusini ambako
ilitia nanga na watumwa wale waliohadaiwa wakajikuta wanaangukia
mikononi mwa watesi wao.
Maofisa wa meli walishtakiwa na
watumwa waliachiliwa isipokuwa viongozi wa uasi huo ambao walijikuta
wakitumikishwa katika Kisiwa cha Robben - ambapo miaka karibu mia mbili
baadaye mpigania haki za weusi Nelson Mandela naye alifungwa. Watumwa
hawa nao ambao kwa kiasi kikubwa historia imewasahau walijitambua kuwa
wao ni nani na hawakujali waliowakamata walikuwa ni kina nani au wana
nguvu gani; walitambua utu wao na walikuwa tayari kuupigania.
Hawakuhitaji elimu ya uraia, hawakuhitaji viongozi wenye elimu kubwa
walichohitaji ni kujitambua kuwa ni binadamu na hawakuwa tayari
kuburuzwa, kudharauliwa, au kuteswa. Hawa nao hawakuwa peke yao.
Uasi wa Majimaji 1905
Miaka 139 baada ya uasi wa Wamalagasy kule Afrika ya Kusini na miaka 66
baada ya uasi wa Amistad kule Uingereza Waafrika bado walijitambua utu
wao na bado hawakutaka kunyanyaswa, kudharauliwa, na kuteswa na watawala
wao. Wananchi wa makabila mbalimbali katika Tanganyika walijikusanya
pamoja kuukataa utawala wa Mdachi (Mjerumani). Kilichowafanya kuukataa
utawala huu haikuwa kukataa rangi ya Wadachi! Walikuwa wanakataa utawala
wa mdachi juu yao.
Katika kufanya hivyo waliamua kuasi;
walinyanyaswa sana na waliteswa sana na kudharauliwa katika nchi yao na
walipofikia kikomo walisema inatosha na wakaanza kujibu mashambulizi.
Watawala waliwaita waasi, watawala walisema ni wachochezi na wanaleta
vurugu katika koloni lililokuwa limetulia na lenye ‘amani’. Watawala
wakasema wamechoshwa na wakaja na sera ya kuwashambulia mababu zetu; na
kweli wengi walikufa mikononi mwa Wadachi! Nani atasahau yaliyomkuta
Chifu Mkwawa, au kina Mpambalioto na Nduna Songea?
Kuanzia
Umatumbi hadi Umatengo, Mahenge hadi Nachingwea, toka ghala za silaha za
Ifakara hadi ngome za Iringa; mto Rufiji hadi Mto Luwegu wazee wetu
wakiwa hawana zaidi cha kupoteza isipokuwa utu wao. Walisimama na
kupigana na watu waliowazidi kwa kila namna. Na kweli walishindwa, damu
ilimwagika na watawala waliamini kuwa wameweza. Lakini historia
haikuwahurumia watawala wale kwani miaka si chini ya kumi tu walijikuta
wanapoteza koloni lao la thamani zaidi kwa wababe wengine. Historia ina
tabia mbaya sana ya kujirudia rudia, hasa ukiidharau.
Hivi kuna
watu wanaamini wazee wetu walihitaji elimu ya uraia ili kujitambua?
Hivi walihitaji kusoma sana kujielewa kuwa utu wao ulikuwa
unadharauliwa? Kwamba wanahitaji wazungu waje kuwapa elimu ya
kujitambua? Hivi kweli inahitaji usomi kujijua unadhulumiwa,
unadharauliwa, na kuwa unatawaliwa isivyo haki?
Kwa kuhalalisha uhalifu wa vyombo vya dola Pinda amewapa wananchi haki ya kujitetea!
Alichokisema Pinda ni kitu ambacho hakina jina jingine isipokuwa
amehalalisha uhalifu kufanywa na vyombo vya dola. Kama nilivyosema
wakati ametoa ile kauli yake ya kuhalalisha uhalifu mwingine dhidi ya
watuhumiwa Pinda anastahili kujiuzulu yeye mwenyewe ili kumpisha mtu
mwingine mwenye hekima na uwezo wa kuongozza wakati kuna pressure.
Alichokifanya kwa upande mmoja ni kutoa kibali kwa Polisi kuwapiga
wananchi kwa sababu yoyote ile kwa kisingizio cha kuleta amani na
utulivu! Lakini amefanya kitu kingine; amewapa wananchi haki ya
kujitetea wakishambuliwa na Rais pasi ya haki.
Haki ya Kujitetea ni Haki ya Msingi ya Mwanadamu
Mojawapo ya haki ambazo labda hatujazizungumza sana na hazieleweeki ni
haki ya kujitetea (the right of self defence). Haki hii haijaleweka au
haieleweki kwa wengi kwani inachanganywa na kuonekana ni uhalifu.
Mwanadamu anayo haki ya kulinda nafsi yake na mali yake kutoka kwenye
dhulma yoyote ile. Mara kwa mara haki hii tunaitumia kwa njia za sheria -
kama kwenda mahakamani au kumkamata mwizi. Lakini inakuwaje kama
jambazi amevamia familia yako na kuitishia maisha na wewe una silaha? Je
unaweza kutumia silaha kuitetea familia yako? Jibu ni ndiyo! Hiyo ni
haki yako na ukifanya hivyo kwa kujitetea maisha yako na ya familia yako
ni vigumu kwa mahakama kukuta una hatia isipokuwa kama inaonekana kwa
mfano, umeweza kumweka jambazi chini ya ulinzi na kumnyang’anya silaha
halafu kwa kisasi ukaamua kumuua! Hapo huwezi tena kujitetea
‘self-defense”.
Lakini inakuwaje kama wanaokushambulia ni
maafisa wa vyombo vya usalama? Je maafisa wa vyombo vya usalama
wakifuata agizo la Pinda wakakukufuza na kuanza kukupiga bila kujaribu
kukukamata au kukuletea mashtaka au si kwa ajili ya kukuweka chini ya
ulinzi unatakiwa kufanya nini? Je, polisi au wana usalama wanaweza kuja
nyumbani kwako na kukushambulia kwa vile wanakushuku wewe ni mkorofii
kama walivyofanya Mtwara je wewe nyumbani kwako una haki ya kujitetea?
Baadhi ya watu ambao nimewasoma toka jana wanaamini kuwa serikali
inaweza kupiga wananchi wake na wananchi hawapaswi kujitetea! Kuna watu
ambao ukiwasoma wanaamini kabisa kuwa polisi na vyombo vya usalama vina
haki na uwezo wa kuja na kukuambia “bong’oa” na wewe unatakiwa ubong’oe
kwa sababu unatakiwa ‘kutii sheria bila shurti’! Wapo kabisa ambao
wanaamini kabisa kuwa Mkuu wa Polisi fulani anaweza kuja na nyota na
mwenge wake na kukuambua “panua” na wewe unatakiwa upanue tu kwa sababu
yeye kasema! Kwamba wanaamini wananchi hawatakiwi kuwabishia polisi,
hawatakiwi kuwauliza na kwa hakika hawatakiwi kuwapinga! Je hili ni
kweli? Je ni kweli polisi wana nguvu hiyo katika maisha ya watu wetu
kiasi kwamba watu wetu wanatakiwa watii bila shurti!? Yaani, watii
lolote, popote, kwa lolote na vyovyote kwa vile wameamriwa hivyo?
Mifano niliyotoa hapo juu inatupa jibu. Mwanadamu siyo mnyama ambaye
anaweza kusukumwa sukumwa au kunyanyaswa na watu wenye nguvu na
madaraka. Mwanadamu ameumbwa na dhamira na utu wake. Wapo wanadamu kati
yetu ambao hawajali kunyanyaswa alimradi wanaachwa na “amani”. Wapo kati
yetu ambao utu wao kwao ni chakula cha leo tu na ukiwapa chakula cha
leo tu basi unaweza kuwafanyia lolote, popote, na kwa lolote! Naam, wapo
kati yetu ambao hawawezi kuhoji serikali yao, hawawezi kuipinga, na
kamwe hawatothubutu kulalamika kwa sababu wanaogopa au kuhofia kuonekana
siyo watiifu. Hawa wakiambiwa ‘inama’ wanainama, ‘inuka’, ‘lala’
wanalala na wakiambiwa ‘lia’ wanalia kama wameona mzimu! Hawa hawana
namna ya kuwasaidia kwani kila jamii inayo watu kama hao; watu ambao
wanaabudu kwenye altare ya watawala wa zama zao!
Wapo kati yetu wanaojitambua
Lakini wapo kati yetu ambao wanajitambua. Wanajitambua kama watumwa wa
Amistad au wazee wa Majimaji na kujiona kuwa na wao ni binadamu wenye
kutaka kutambuliwa na kuthaminiwa utu wao kama walivyofanya wale wa
Malagasi. Wapo kati yetu ambao wameamua kukataa watawala wa sasa,
kuwapinga na kuwabishia; wamekataa kuendelea kufukiza uvumba mbele zao.
Watawala hawawapendi hawa na maneno ya Pinda kimsingi yanawalenga hawa.
Hawa hawatokubali kunyanyaswa na kudharauliwa na kwa vile Pinda amewapa
kibali vyombo vya dola kuwapiga wananchi basi wananchi nao watakuwa
wamejipa haki ya kujitetea dhidi ya polisi.
Hili si jambo geni
na mara nyingi ndio mwanzo wa machafuko makubwa ya nchi. Polisi
wanapoanza kutekeleza amri kama za Pinda wananchi nao wanaanza kutenda
kwa kujitetea na wanatangaza uadui na polisi na matokeo yake ni kuwa
polisi watakaojifanya ndio wa kwanza kupiga wananchi bila sababu
watajikuta wanarushiwa mawe na wao kuanza kupigwa. HIli likikitokea mimi
sitoshangaa kwa sababu Mwanadamu ana haki ya kujitetea. Huu mtindo wa
polisi kwenda kwenye nyumba za watu na kuanza kuwapa kipigo kutageuka
kwani wananchi nao wataanza kutetea nyumba zao na familia zao.
Pinda asije kudhani kuwa serikali inaweza ikashindana na wanananchi
wake. Ni kweli inaweza kuwa na silaha nyingi na mbinu nyingi lakini
wananchi wakiamua kujibizana na polisi serikali itashindwa na itaanguka
yenyewe. Ndiyo historia ilivyo. Pinda afute kauli yake au aiweke vizuri.
Akiiacha hivyo ilivyo kuwa polisi waanze kuwapiga tu wananchi kwa
sababu ati wao kina Pinda wamechoka ajue kabisa kuwa amewapa na kibali
wananchi haki ya kujitetea watakapoanza kupigwa.
0 comments:
Post a Comment