KATIKA Rasimu ya Katiba Mpya imependekezwa kuwa Kiswahili kiwe ni mojawapo za tunu ya taifa. Kama rasimu hii ikipitishwa na kuthibitishwa na wananchi katika maoni yao, itabidi juhudi zielekezwe katika mambo yafuatayo ili kuleta mafanikio yanayotarajiwa.
Kwanza ni kuimarisha vyombo vilivyoko vya kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili. Vyombo hivi ni Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Baraza la Kiswahili la Zanzibar (Bakiza), Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (Tataki), Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (Takiluki). Hizi ni taasisi na mashirika yaliyoundwa kisheria hapa nchini ambayo hayana budi kuhuisha sheria zilizoyaunda ili ziweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Kabla ya kueleza mambo yahusuyo kuyaboresha mashirika na vyombo vya lugha, ningependa kwanza kuwe na msukumo wa kisiasa ili uwezeshe serikali kutoa fedha za kutosha kufanya kazi za utafiti na uchapishaji wa vitabu, makala na majarida ya Kiswahili.
Nikianzia na Bakita ambalo lilianzishwa mwaka 1967, ningependa sheria hii irekebishwe na kuliwezesha kuwa na uwezo wa kuchukua hatua kali kwa waandishi na wachapishaji vitabu ambao wanakiuka taratibu za uandishi bora.
Waandishi na wachapishaji wahakikishe kuwa taarifa wanazotoa kwa umma zinatolewa kwa kutumia Kiswahili sahihi na sanifu. Huko Bakita kuna kitengo cha kusanifisha lugha. Mojawapo ya jukumu la kitengo hiki ni kupitia maandishi ya kutoa maelekezo pale penye makosa.
Maelekezo yatakayotolewa yakikiukwa, hatua zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kulifungia gazeti au kitabu kama waandishi na wachapishaji hawafuati masharti yaliyowekwa.
Kwa upande wa watangazaji nao wafuatiliwe. Wako watangazaji katika vyombo vya habari ambao wanakiuka miiko ya lugha, hasa katika matamshi yao. Wanazungumza kwa lafudhi isiyokubalika na ambayo imeathiriwa na lugha za asili.
Wengine wanazungumza Kiswahili kwa kutumia lafudhi ya Kiingereza. Mbaya zaidi watangazaji wanatumia maneno ya Kiingereza na hata sentensi kamili zenye maneno ya Kiingereza na kuzipachika katika mazungumzo ya Kiswahili.
Katika utafiti niliofanya kuwasikiliza watangazaji katika redio za FM wengi wao ni vijana. Vijana hawa wanapenda kujikweza kwa kutangaza kwa mikogo na mbwembwe kuonyesha kuwa ni wasomi. 

Pengine wamesoma hadi kidato cha sita na kusomea kozi fupi ya utangazaji. Kwa hiyo kama wamesoma, wamekaribia tu elimu ya juu lakini bado ni wabichi na hawajaelimika vya kutosha. Watangazaji hawa wanakuwa na mpangilio mbovu wa maneno, wanachanganya lugha ya Kiswahili na Kiingereza wanapokosa maneno sahihi ya Kiswahili, n.k.
Watu wa aina hii wanatakiwa waelekezwe na endapo hawabadiliki wachukuliwe hatua. Bakita lipewe uwezo wa kuwazuia wale wanaoharibu lugha pamoja na vyombo wanavyotumia na wakatazwe kuandika au kutangaza katika vyombo vya habari hadi watakapobadilika.
Suala jingine ni kukiimarisha Kiswahili kwa kupitia upya mitalaa ya ufundishaji wa Kiswahili katika ngazi za elimu ya msingi na sekondari kwa kuwa na vitabu vya kitaaluma vinavyozingatia sarufi na fasihi ya Kiswahili. Vitabu vinatakiwa kuwa na mambo yafuatayo:

Kwanza ni kutayarisha vitabu vitakavyozingatia kukuza stadi za lugha kama kusikiliza, kuzungumza, kusoma, kuandika na pia kuchora.
Yawepo mazoezi ya kutosha kwa wanafunzi kujieleza kwa kuzungumza, kuandika na kuchora. Walimu wajitoe zaidi kuwasaidia wanafunzi kwa kusahihisha kazi zao mapema na kuzirejesha mapema kwa wanafunzi.
Upungufu uliopo katika vitabu vya lugha zikiwamo Kiingereza na Kiswahili ni ukosefu wa mazoezi ya kutosha kwa wanafunzi.
Umakini wa utayarishaji wa vitabu hauko kama ikilinganishwa na siku za nyuma. Hivi sasa utayarishaji vitabu unazingatia sera ya ubinafsishaji.
Hatua hii ilitibua sana viwango vya kitaaluma kwani wachapishaji vitabu walianza kuchapisha vitabu visivyo na ubora. 

Wachapishaji hawa wengi wao walipitisha miswada yao katika kitengo cha kutoa ithibati ya vitabu cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (EMAC) lakini kwa masikitiko makubwa yalikuwapo makosa chungu nzima ya tahajia, matumizi mabaya ya maneno, ukosefu wa umakini katika mantiki katika aya. 

Haya yote na mengine mengi yanaonyesha kuwa vitabu hivyo havikupitiwa na wataalamu wa lugha.
Vilevile vitabu hivyo vilikuwa na kasoro za kitaaluma hasa usahihi wa mada zilizowasilishwa. Iko mifano ya vitabu vya Jiografia, Uraia na Historia ambavyo vina makosa ambayo yangeweza kusahihishwa mapema kabla ya kuchapishwa.
Ni vyema kama Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ingerekebisha muundo mzima wa Kitengo hiki pamoja na mfumo wa kufanya kazi badala ya kuwaondoa waliopo na kuweka wengine wapya.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top