Rais wa zamani wa Afrika ya kusini, Nelson Mandela.

Wananchi wa Afrika Kusini hii leo wamekuwa na wasiwasi baada ya rais wa nchi hiyo Jacob Zuma kutangaza kuwa hali ya afya ya rais mstaafu Nelson Mandela sio nzuri sana.

Asubuhi waliamkia kwenda kazini wasijue taarifa watakazopokea hii leo baada ya rais Zuma kutoa taarifa hiyo.
Taarifa kutoka ikulu ya rais zilisema Jumapili jioni kuwa Mandela alikuwa amezidiwa ingawa madaktari wanafanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa anapata afueni.

Afisaa mmoja mkuu alisema kuwa raia wa Afrika Kusini wasiwe na matumaini kupita kiasi.

Mandela ambaye alikuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, akiwa na umri wa miaka 94,alipelekwa hospitalini mapema mwezi huu, ikiwa ni mara ya tatu kwake kulazwa hospitalini akiugua ugonjwa wa mapafu mwaka huu.

Rais Jacob Zuma alisema Jumapili kuwa alimzuru Mandela Hospitalini na kuzungumza na mkewe kuhusu hali ya rais mstaafu.
Madaktari wanaomtibu Mzee Nelson Mandela wamesema hali yake imekuwa sio nzuri kwa saa ishirini na nne zilizopita na sasa ni mahututi.

Habari hizo zimekuja kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais ya Afrika Kusini.

Taarifa hiyo imesema bado Mzee Mandela ameendelea kusalia hospitalini mjini Pretoria kwa siku ya kumi na sita akitibiwa mapafu yaliyosababisha tatizo kwenye mfumo wake wa upumuaji.

Rais Jacob Zuma amemtembelea Mzee Mandela na pia kuzungumza na jopo la matabibu wanaomtibu.

Baadaye bwana Zuma alirejea kauli yake ya kulitaka taifa na dunia kumuombea Mzee Mandela apate nafuu.
Chanzo: BBC-Swahili
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top