Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe
  
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amesema upo uwezekazo wa Katiba Mpya ya Tanzania Bara ikapatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
 
Chikawe alizungumza Dar es Salaam jana kuwa, ikiwa mchakato wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano utakamilika kama inavyokusudiwa na rasimu hiyo kupitishwa na wananchi katika ngazi zote bila mabadiliko, muda utakaobaki utatosha kuandaa Katiba ya Tanzania Bara.
“Watu wasiwe na hofu. Sioni tatizo endapo rasimu itapita bila mabadiliko na kupata Katiba Mpya. Aprili mwakani mpaka Desemba inatosha kabisa kuandaa Katiba ya Tanzania Bara na tukaenda katika Uchaguzi Mkuu tukiwa na Katiba Mpya,” alisema na kuongeza:
“Tunaweza kuwatumia wajumbe walewale wa Tume ya Katiba, lakini safari hii tukawachukua wale wa Tanzania Bara pekee wakashiriki katika kuandaa Katiba hiyo.”
Hata hivyo, Waziri Chikawe alisema kutokana na muda kuwa mfupi, Tume hiyo inaweza isifanye kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi kama ilivyofanya sasa na badala yake ikaandaa rasimu na kujadiliwa na wadau kisha kupelekwa katika mabaraza ya Katiba kabla ya kupata Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kukamilika Aprili mwakani.
Chikawe anasema kuanzia hapo Serikali inaweza kuitumia tume ya sasa kutangaza rasimu ya kwanza ya Katiba ya Tanzania Bara kwa kurejea maoni iliyokusanya hivyo hatua ya kwanza ikawa ni kujadiliwa kwa rasimu hiyo kwenye mabaraza ya Katiba kwa miezi miwili na baadaye kupelekwa katika Bunge la Katiba jambo litakaloifanya ipatikane mapema.
Waziri Chikawe alisema kinachotakiwa sasa ni kujiandaa kwa Tanzania Bara kuwa na Katiba yake ambayo itatumika kwa ajili ya mambo mbalimbali, ukiwamo Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Waziri huyo aliwatoa hofu Watanzania kwamba hakuna mpango wa kumwongezea muda wa uongozi, Rais Jakaya Kikwete kama ambavyo imekuwa ikielezwa kwani Serikali ina uhakika kwamba kila kitu kitafanyika katika muda uliopangwa.
Siku chache zilizopita Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba alikaririwa akisema kuwa Serikali ina mpango wa kumwongezea Rais Kikwete muda wa kuongoza.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
Wakati Chikawe akitoa kauli hiyo, habari kutoka ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), zinasema kutokana na mapendekezo ya kuwapo kwa Serikali tatu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema anaandaa “kitu muhimu” ambacho atakiwasilisha bungeni siku chache zijazo.

“Kuna kitu AG anafanya na ndani ya wiki hii atakiwasilisha ndani ya Bunge kuhusu Tanzania Bara,” kilisema chanzo hicho bila kufafanua ni kitu gani hasa.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Abubakar Hamisi Bakari alisema, suala la visiwa hivyo kuwa na Katiba Mpya au la, lipo mikononi mwa wananchi wa Zanzibar… “Hayo watasema wananchi wa Zanzibar kupitia wawakilishi wao kama wanataka kufanya mabadiliko watafanya.”
Wasomi wanena
Mapema jana, baadhi ya wasomi walieleza wasiwasi wao kuhusu hatima ya Tanzania Bara ikiwa mapendekezo ya Serikali tatu yatakubaliwa na kupitishwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema mabadiliko yaliyopendezwa mengi yameachwa kwa sababu ya pendekezo la kuwapo kwa Serikali tatu.
“Katiba hii haiwezi kufanya kazi bila kuwa na Katiba mbili za washirika ambazo, lazima ziundwe na haijulikani itakuwa lini. Katiba ya Zanzibar lazima ifanyiwe marekebisho na Tanzania Bara kuandikwa,” alisema Ally na kuongeza: “Wananchi walihitaji demokrasia siyo Serikali tatu, jambo hili lina mkanganyiko mkubwa na litapita tu kwa sababu muda wa kujadiii haupo.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Gaudence Mpangala: alisema “Kwa muda mrefu wananchi na wanaharakati wamekuwa wakililia Serikali tatu hatimaye limefanikiwa.”
Hata hivyo, alisema jambo linalotakiwa kufanyiwa kazi ili kwenda sambamba na utendaji wa Serikali tatu ni Tanzania Bara kuwa na Katiba yake kama ilivyo Zanzibar.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Profesa Tolly Mbwete mbali na kutoa pongezi alisema: “Kitu ambacho naona hakikufanyiwa kazi ipasavyo ni suala la madaraka ya Rais kutopunguzwa pamoja na kutoelezwa mchakato wa Tanzania Bara kuwa na Katiba yake.”
 Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top