Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Ametoa
kauli hiyo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa
29 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika hoteli ya Sundown Carnival, nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Waziri Mkuu alisema haipendezi
kusikia baadhi ya wakuu na watendaji katika Halmashauri wakituhumiwa kuwa
sehemu ya mitandao ya wizi katika Halmashauri au wana maslahi katika kampuni
zilizohusika kutoa huduma na bidhaa duni kwa Halmashauri.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu
alisema kuna malalamiko amepokea kwamba Meya wa Halmashauri moja amefungua
kampuni sita na zote anataka zipewe tenda kwenye Halmashauri anayoiongoza.
“Kuna Halmashauri zenye taarifa
za wizi, upotevu na ubadhirifu ambao kwao umekuwa ni maisha ya kawaida. ALAT
mnayo nafasi kubwa kuendelea kuboresha usimamizi wa fedha za Halmashauri kwa
vile Jumuiya yenu inawaunganisha watendaji wakuu na viongozi wakuu wa
Halmashauri zote chukueni hatua. Waaibisheni na kuwaumbua wale wanaobanika
kutumia vibaya fedha hizi za umma.”
“Lakini, ili muweze kufanya
hayo lazima ninyi wenyewe msiwe sehemu ya uovu huu. Inafadhaisha sana kusikia
minong’ono kuwa baadhi ya madiwani wanatuhumiwa kuwa sehemu ya mitandao ya wizi
katika Halmashauri .... huo ni ukosefu wa wajibu na ni kuvunja mkataba wenu na
umma.
Akuzungumzia kuhusu utunzaji wa
mahesabu, Waziri Mkuu alisema upo udhaifu katika eneo hilo kwani upo ushahidi
unaoonesha kwamba taarifa za vitabuni hazifanani na kazi iliyofanywa (value for
money) akimaanisha kwamba kazi inayofanyika hailingani na thamani halisi ya
fedha iliyotumika.
“Tatizo hili ni kubwa na lina
sura mbili kuu. Moja ni kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya watumishi
na madiwani katika usimamizi wa fedha za Serikali za Mitaa. Baadhi ya madiwani
wamediriki kushirikiana na watumishi wasio waaminifu katika
kuhujumu fedha za umma. Pili, ni Watumishi wa Serikali za mitaa
kushindwa kutekeleza wajibu wao hivyo kulipwa mishahara ambayo hawaitumikii
ipasavyo,” alisema.
“Hili nalo nataka lijadiliwe
kwa kina na mkitoka hapa kila Kiongozi na Mtendaji ajue ana jukumu gani la
kufanya. Aidha, hili ndilo eneo ambalo nataka hatua zichukuliwe ili
kunusuru Fedha za Halmashauri,” alisisitiza.
Alisema kwa kutambua ukweli
huo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameendelea na ukaguzi wa
thamani ya fedha zaidi ya ukaguzi wa kawaida.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu alipokea hundi ya mfano ya sh. milioni 10
iliyotolewa na Benki ya NMB ili ziweze kusaidia kununua dawa na vifaa tiba kwa
ajili ya majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu mkoani Arusha kutokana
na mlipuko wa bomu uliotokea Mei 5, mwaka huu kwenye Kanisa la Mt. Joseph
Mfanyakazi, eneo la Olasiti.
Akizungumzia msaada huo, Mkuu
wa Kitengo cha Biashara na Serikali wa benki hiyo, Bibi Domina Feruzi alisema,
kama taasisi wameguswa na maafa yaliyowakumba wakazi hao wa Arusha na wameamua
kuchangia kiasi hicho cha fedha ili kiwasaidie kwa dawa na vifaa vya tiba
vinayohitajika.
0 comments:
Post a Comment