Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imemhukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja katibu wa Taasisi za Jumuiya ya Kislaam nchini Sheikh Issa Ponda.

Katika hukumu hiyo pia mahakama imewaachia huru watuhumiwa wengine zaidi ya 49 waliokuwa wameshitakiwa pamoja na katibu huyo.

Majira ya asubuhi ya mei 9 katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Dar es Salaam, waumini wa dini ya kiislam walitanda huku wakiwa wamejawa na shauku  ya kusikia hukumu ya kiongozi wao sheikh Issa Ponda.

Lakini ulinzi ulikuwa umeimarishwa kila kona ya mahakama hii ya kisutu kwa ajili ya usalama.

Tofauti na siku zingine, maafisa wa magereza walimfikisha mtuhumiwa huyo na wenzake 49 mahakamani hapo majira ya 12:49, ambapo majira ya saa 3:48 watuhumiwa hao walianza kuingia ndani ya chumba cha mahakama tayari kusubiri uamuzi wa mahakama dhidi yao.

Dakika tatu baadaye Chini ya hakimu mkazi wa mahakama ya kisutu, Bi Victoria Nongwa, hukumu  hiyo ilianza kusoma ambapo mashahidi wa pande mbili zinazopingana wakiwasilisha ushahidi.

Katika hukumu hiyo hakimu Victoria Nongwa pamoja na masuala mengine amesema kuwa kosa 1,2,3,4,5  hayakuthibitika kwa watuhumiwa 49 ambapo mahakama imelazimika kuwaachia huru.

Sheikh ponda alikutwa na hatia katika kosa la kumilikisha ardhi ya markasi iliyoko Temeke kinyume na sheria na kwamba kwa mujibu ya kifungu cha 23 kifungu kidogo cha G, cha kanuni za adhabu  kinampa uhalali hakimu kuchagua aina ya adhabu anayopaswa kupewa mtuhumiwa.

Na ndipo hakimu Victoria Nongwa alipomchagulia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja nje na kumtaka  katika kipindi chote hicho kuhakikisha hajihusishi na vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani.

Akizungumza mara baada ya kuachiliwa huru sheikh ponda alionekana wazi kutokuwa na imani na vyombo vya ulinzi na usalama.

Kwa upande wao baadhi ya wafuasi wa kiongozi huyo walionekana wazi kuwa na imani na mahakama huku wengine wakionekana kuwa tofauti na mahakama.

Mapema Oktoba 18 mwaka 2012  katibu wa Taasisi za Jumuiya ya Kiislaam Tanzania walifikishwa mahakamani hapo kwa makosa kadhaa yakiwemo  kuvamia kiwanja kinyume cha sheria na tuhuma za  wizi wa mali  mbalimbali zenye thamani  ya shilingi milioni 59.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top