Majeneza yaliyowekwa miili ya marehemu waliokufa katika shambulio la bomu Jumapili iliyopita kwenye misa ya  uzinduzi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi la Parokia ya Olasiti, Jimbo Kuu la Arusha, majeneza hayo yalikuwa ndani ya Kanisa hilo wakati wa misa ya kuwaombea kabla ya kuzikwa.

Watu watatu, waliofariki katika shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, mkoani Arusha wamezikwa jana na mamia ya watu, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa kuliko kawaida na viongozi wa dini na Serikali kutoa kauli nzito.
 
Marehemu hao, ni  Regina Loning’o Laizer (45), James Gabriel(16) na  Patricia Joachim Assey(9) walizikwa katika eneo la kanisa hilo Katoliki, mazishi yaliyohudhuriwa na maaskofu wanane wa majimbo tofauti ya Kanisa Katoliki, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), Askofu Alex Malasusa, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na viongozi mbalimbali wa dini, Serikali na kisiasa.
Kauli za viongozi
Katika ibada hiyo ya viongozi mbalimbali wa kidini, walitoa salamu zao akiwamo Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa aliyeitaka Serikali kutumia msamiati wa mwenye macho haambiwi tazama na kukomesha mpasuko wa kidini aliosema unalitafuna taifa.
Askofu huyo alisema kuwa miongo mitatu sasa, Serikali imekaa kimya, ikishuhudia mafundisho na mihadhara ya kidini inayochochea na kuhamasisha uhasama kati ya Ukristo na Uislamu, bila kuchukua hatua kukomesha hali hiyo.
“Matukio mbalimbali yanayoashiria uhasama wa kidini yanatokea nchini. Kuna mihadhara, CD, DVD, machapisho na mafundisho yanayotishia maisha na usalama wa viongozi wa kanisa na waumini wao, ambayo yamefuatiwa na uchomaji wa makanisa,” alisema Askofu Ngalalekumtwa.
Alitaja mfano wa kongamano la Januari 15, mwaka juzi iliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubillee jijini Dar es Salaam kuwa moja ya mikutano iliyojaribu kuchochea chuki ya kidini kati ya Waislamu na Wakristo kwa kudai kuwa Serikali ya Tanzania inaongozwa kwa mfumo wa  Kikristo ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Askofu huyo alisema kwamba katika kongamano hilo, washiriki waliaminishwa kuwa Serikali inatoa fedha za ruzuku kujenga shule na taasisi za kanisa kutokana na kuwapo mkataba maalumu kati ya kanisa na Serikali, jambo ambalo siyo kweli.
“Kinachosikitisha zaidi ni kwamba Serikali haikukanusha madai na uchochezi huo, licha ya mambo hayo kufanyika na kusemwa hadharani kwa wahusika kuzunguka nchi nzima kueneza chuki na uchochezi huo,” alisema Askofu Ngalalekumtwa.
Mkuu wa Kanisa la KKKT, Askofu Dk Alex Malasusa alisema kuwa tukio la Arusha ni la kikatili na aibu kwa taifa akiwataka wenye dhamana ya ulinzi na usalama kuchukua hatua kudhibiti hali hiyo akionya kuwa wasipofanya hivyo watahukumiwa kwa kosa la kukaa kimya mambo yakiharibika mikononi mwao.
“Wote wenye jukumu la kulinda na kuitunza amani waifanye kazi hiyo bila uoga. Wasipofanya hivyo iko siku watahukumiwa,” alisema Dk Malasusa.
Mwakilishi wa Muungano wa Madhehebu ya Kikristo mkoani Arusha, Askofu Stanley Hotay aliwataka viongozi wa kisiasa kuepuka kutumia jukwaa la dini kutimiza malengo ya kisiasa, akionya kuwa makanisa hayana itikadi, bali waumini ndiyo wenye itikadi mbalimbali.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top