Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa rasimu ya mwongozo kuhusu
uundwaji wa Mabaraza ya Katiba yakiwemo yatakayoundwa na asasi, taasisi
na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana, huku ikitoa siku nane kwa
wadau kutoa maoni yao kuhusu rasimu hiyo.
Mwongozo huo unaainisha muundo, utaratibu na
uendeshaji wa mabaraza yote ya Katiba, huku mwisho wa kuwasilisha maoni
kwa tume hiyo kuhusu Rasimu ya Mwongozo huo ikiwa ni Mei 19, mwaka huu.
Watakaounda mabaraza hayo ni pamoja na Jumuiya ya
Kidini, Chama cha Siasa, Asasi ya Kiraia, Taasisi ya Elimu ya Juu, Chama
cha Wafanyakazi, Chama cha Wakulima, Chama cha Wafugaji, Chama cha
Wanahabari na Baraza la Watoto. Nyingine ni Taasisi ya Wafanyabiashara, Baraza la Wanawake, Taasisi ya Wanataaluma, Baraza
la Vijana, Baraza la Wazee na Kundi au makundi ya watu wenye mahitaji
maalumu katika jamii.
Kutolewa kwa rasimu hiyo kumekuja mwezi mmoja
tangu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutishia kujitoa
kwenye mchakato wa Katiba Mpya, kikitaka kurekebishwa kwa baadhi ya
mambo katika mchakato huo.
Aprili 11, mwaka huu chama hicho kilitangaza
kwamba ifikapo Aprili 30, mwaka huu kitajitoa endapo mambo muhimu mawili
hayatapatiwa ufumbuzi.
Mambo hayo ni kufutwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa
Mabaraza ya Wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata
(WDC), badala yake wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa kata husika
bila kuchujwa na kamati hizo.
Hata hivyo, baadaye kilieleza kuwa kinafanya mikutano ya ndani kabla ya kutoa jibu kamili kuhusu suala hilo.
“Tume inaweza kuruhusu asasi, Taasisi na makundi
ya watu wenye malengo yanayofanana kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa
fursa kwa wanachama wake kutoa maoni yao juu ya rasimu ya Katiba na
kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume.
Hilo tumeruhusu kwa mujibu wa sheria,” alisema Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Alisema kuwa tume hiyo imeamua kuwa mabaraza ya
Katiba yatakuwa katika makundi mawili, la kwanza likiwa ni mabaraza
ambayo tume itayasimamia na kukusanya maoni (Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa).
Mabaraza mengine ni yale ambayo hayatasimamiwa na
tume hiyo, bali yatajisimamia yenyewe na kukusanya maoni
yatakayowasilishwa kwenye tume kwa mujibu wa maelekezo.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment