Taasisi moja ya masuala ya mapato imetoa ripoti yake ya mwaka
2011/12 kuhusu Utendaji na Utawala katika rasilimali. Ripoti hiyo
inaonyesha kuwa Tanzania ni dhaifu katika usimamizi wa rasilimali zake
ikishika nafasi ya 27 kati ya nchi 58 zenye usimamizi mbovu katika sekta
hiyo.
Ripoti ya taasisi hiyo ya Revenue Watch Institute,
inaeleza kuwa Tanzania iliyo na madini ya shaba, fedha, almasi na gesi
asilia, imeshindwa kulinda na kudhibiti rasilimali zake, hivyo kuathiri
utendaji katika sekta nyingine.
Inaeleza kuwa katika masuala ya kisheria kuhusu
madini Tanzania imeshika nafasi ya 46 kati ya nchi 58, ambayo ni sawa na
asilimia 44 na kufafanua kuwa hali hiyo imetokana wananchi wake kutojua
mambo mengi kuhusu rasilimali zao hali inayochangiwa na kutokuwa na
sheria huru ya vyombo vya habari.
“Kingine ni Wizara ya Nishati na Madini pamoja na
Mamlaka ya Mapato (TRA), zote kukusanya malipo kutoka katika kampuni za
madini. Kampuni hizo pia hufanya baadhi ya malipo moja kwa moja kwa
wananchi walioathirika, vinginevyo mapato yote huenda Hazina,” inaeleza
sehemu ya ripoti hiyo.
Inaeleza kuwa baada ya miaka mingi ya Tanzania
hupata mrabaha mdogo kutoka katika kampuni za madini, mwaka 2010 sheria
ya madini ilifanyiwa marekebisho na mrabaha kuongezwa, lakini bado
mikataba ya kampuni za madini imeendelea kuwa siri.
Inaeleza kuwa kampuni hizo zinatakiwa kueleza
athari za mazingira katika migodi, lakini nyingi hazifanyi hivyo na
kwamba hali hiyo ni kinyume na matakwa ya leseni zao.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo kampuni hizo zinatakiwa
kuweka wazi taarifa zake za mapato kwa kuwa mwaka 2012, Tanzania ilitia
saini mpango wa uwazi katika shughuli za madini.
Inaeleza kuwa sababu ya Tanzania kuwa na usimamizi
mbovu katika sekta ya madini ni pamoja na kushindwa kuchapisha mikataba
ya madini wala kuwa na takwimu za kampuni zinazomilikiwa na Serikali,
licha ya kuwa inatoa baadhi ya taarifa juu ya uzalishaji na mapato ya
madini.
“Wizara ya Fedha huchapisha habari juu ya kiasi
cha uzalishaji na thamani ya mauzo ya nje, lakini haitoi maelezo juu ya
mapato katika madini,” inasema sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza;
“Wizara ya Nishati na Madini inachapisha maelezo
kuhusu hifadhi, kiasi cha uzalishaji, bei ya kuuza nje, idadi ya
kampuni, kodi na mirabaha, lakini haitoi takwimu juu ya ada ya leseni,
gawio au mafao.”
Inafafanua kuwa licha ya Benki Kuu ya Tanzania
(BOT) huchapisha ripoti kila mwaka kuhusu mauzo ya nje na kiasi cha
uzalishaji, sheria mpya ya madini haijaondoa mamlaka ya hiari ya Waziri
wa Nishati na Madini katika utoaji leseni na mazungumzo ya mkataba.
Inaeleza kuwa Tanzania pamoja na kuwa na mazingira
mazuri imepata alama za chini katika utawala wa sheria, hali
inayotokana na kuwepo kwa vitendo vya rushwa na uwajibikaji mdogo.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa katika usimamizi wa kampuni za madini
Tanzania imeshika nafasi ya 31 kati ya nchi 45, ambayo ni sawa na
asilimia 33.
Inaeleza kuwa shughuli mbalimbali za usimamizi wa
madini hufanywa na Shirika la Madini la Taifa (Stamico), ambalo
linaimarishwa na Serikali ili kuboresha utendaji wake, lakini bado
kumekuwa na kasoro kubwa katika uchapishaji wa mapato na kampuni
zilizokaguliwa kwa mwaka.
Inaeleza kuwa nia ya Serikali ya Tanzania ni kuanzisha mfuko wa maendeleo ya madini, lakini mpango huo bado haujatekelezwa.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment