Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ndugu Freeman Mbowe akizungumza kwenye mkutano uliofanyika katika manispaa ya Songea jana jioni.

Taifa lipo katika kipindi kigumu kutokana na wananchi kukabiliwa na umaskini wa kupindukia unaosababishwa na mfumo uliopo kulenga kuwanufaisha watu wachache wakati walio wengi wanazidi kubaki maskini.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mheshimiwa Freeman Mbowe, alipokuwa akihutumia mamia ya wananchi katika uwanja wa shule ya msingi Matalawe Manispaa ya Songea.


Mbowe alisema kuwa wananchi wamebaki maskini kiasi kwamba kila sehemu wanalia juu ya hali ngumu ya maisha kutokana na mfumo uliopo kutowasaidia. 

Vivile aliwasihi wananchi kuunganisha nguvu bila kujali vyama ili kudai haki zao kitaifa.


“Ndugu wananchi tuache ushabiki wa vyama, wanachadema msigombane na wana-CCM kwa sababu wako CCM na wala uliye katika chama kingine usimchukie aliye Chadema... Mwanachadema ukiona mtu amebaki CCM ujue hujafanya kazi ya kutosha kumuelimisha hivyo unawajibika kumshawishi zaidi ili akuelewe”. Alisema Mbowe.


"Sisi ni watoto wa maskini tunahitaji kuunganisha nguvu  ili kuikomboa nchi hii kutoka mikononi mwa watawala wachache, wasiowajibika, ambao hawalitakii mema taifa letu".


Aidha, Mbowe alitahadharisha juu ya tabia ya serikali kutumia risasi na mabomu bila sababu za msingi kiasi cha kuwafanya wananchi waanze kuiogopa Serikali na kutokuwa na imani nayo.


“Tunajenga Taifa la watu waoga na wasiojiamini tena matokeo yake  wananchi wameacha kumwogopa Mungu wanawaogopa watawala” alisema.


Mwenyekiti huyo wa CHADEMA akizungumzia mfumo wa utawala uliopo, alisema unawapa nguvu zaidi za kimaamuzi viongozi wanaoteuliwa na Rais kuliko wawakilishi halali wa wananchi kwa vile wateule wa Rais hufanya baadhi ya maamuzi mazito kwa nchi ambayo wawakilishi wa wananchi hawayaoni kutokana na usiri uliopo, ambapo alitolea mfano wa mikataba ya Gesi na madini kuwa haiko wazi.


Alisisitiza kuwa kitendo cha kumpa Rais uhuru wa kuamua mtu wa kumchagua kinatoa mwanya kwa Rais kuteua baadhi ya watendaji kwa maslahi binafsi, undugu na hata urafiki jambo linaloifanya serikali ishindwe kuwajibika ipasavyo.


Akaendelea kusema msimamo wa Chadema ni kuona wakuu wa wilaya na mikoa wanachaguliwa na wananchi na wawe wenyeji wa maeneo wanayotaka kuongoza tofauti na sasa ambapo wanaweza kuongoza popote pale nchini.

Akizungumzia suala la mgogoro wa gesi Mtwara, Mbowe alisema serikali haikupaswa kutumia nguvu kubwa ya kuwapiga wananchi kwa mabomu au risasi badala yake ilipaswa kukaa nao ili kupata suluhu ya kudumu.
  
Awali Kaimu mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Lindi, Ally Omary Chitanda alisema migogoro inayotokea katika nchi hii, ukiwemo wa Mtwara, inasababishwa na serikali ya CCM kutokuwa tayari kuwasikiliza wananchi pamoja na mfumo wake unaowapa mamlaka watu wachache waishio Dar es Salaam kutaka kila kitu kizuri kiwe Dar es Salaam na kuwasahau watu wa mikoani.

Naye mwenyekiti CHADEMA mkoa wa Ruvuma ndugu Edson Mbogoro aliishutumu serikali ya CCM kulitumia jeshi la polisi vibaya na kulifanya lipoteze hadhi yake kisha akalitaka  jeshi la polisi kuwa huru kwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria zinavyotaka.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top