TAARIFA YA
UCHUGUZI JUU YA KUTEKWA NA KUUMIZWA
KWA ABSALOM
KIBANDA
IMEWASILISHWA
NYUMBANI HOTEL - TANGA MEI 30, 2013
UTANGULIZI:
Usiku wa Jumanne ya
Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013, Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd,
ambaye pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda
alivamiwa na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake
Mbezi Juu, Dar es Salaam.
Tukio hilo liliishtua
na kutikisa taifa kwa kiwango kikubwa si tu katika tasnia ya habari nchini,
bali pia jamii kwa ujumla hasa baada ya aina ya utekaji, utesaji na usiri
uliotumika katika kufanikisha uhalifu huu kufanana kwa karibu na tukio
lilomkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madkatari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka
lililotokea karibu miezi tisa kabla ya tukio la Kibanda yaani, usiku wa Juni
26, 2012.
Ukiacha matukio hayo,
miezi sita kabla ya Kibanda kutekwa na kuteswa Mwandishi Daudi Mwangosi, aliuawa
akiwa mikononi mwa vyombo vya dola Septemba 2, 2012 huko Nyololo, Iringa akiwa
kazini.
Tukio la Kibanda limekuwa
na sura ya mwendelezo wa mauaji au utesaji wa wanahabari, hasa ikitiliwa
maanani kuwa Mwandishi Issa Ngumba (45) wa Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia
kazi zake katika Wilaya ya Kakonko, Kigoma, Januari mwaka huu, alipigwa risasi
na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha.
Kama hiyo haitoshi,
tukio la kutekwa na kudhuriwa kwa Kibanda limetokea mwezi mmoja tu baada ya
Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu kupigwa risasi na polisi
akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam kwa maelezo kuwa kimakosa polisi walidhani Matutu
ni jambazi.
Mazingira ya kutekwa na
kuumizwa kwa Kibanda yalitia wasiwasi kuwa upo uwezekano, na dalili zilionyesha
kwamba waliofanya kitendo hicho cha kinyama hawakuwa wezi wala majambazi
kutokana na ukweli kwamba licha ya kuwa na fedha zipatazo shilingi milioni tatu
taslimu ndani ya gari, laptop, simu tatu za gharama (ipad, iphone na
Blackberry), watekaji hawa hawakuchukua chochote baada ya kukamilisha uhalifu
wao.
Kibanda aliumizwa kwa
kiwango kikubwa. Alitobolewa jicho la kushoto, akaumizwa vibaya kichwani kiasi
cha kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya mifupa
ya kichwa. Aling’olewa meno mawili na kucha mbili, tena bila gazi. Watekaji
hawa, katika unyama wa ajabu kabisa, walimkata pingiri ya kidole cha pete chini
ya kucha na kuondokana nayo.
Hali hiyo iliibua
maswali mengi, watu wengi wakajiuliza na kutafuta sababu za kutekwa na kuumizwa
kwa Kibanda kiasi hiki. Kutokana na kuwapo kwa maelezo mengi yanayotofautiana
kuhusu tukio hilo, ikabidi Jukwaa la Wahariri Tanzania lifanye uamuzi.
Katika kikao cha Machi
8, 2013 Jukwaa la Wahariri Tanzania liliunda TIMU ya watu watano na kuipa
hadidu rejea za kufanya uchunguzi wa kihabari juu ya shambulio hilo kubaini limetokana
na nini.
Timu hiyo iliundwa
kufuatia uamuzi wa Jukwaa la Wahariri kufanya uchunguzi huo na baada ya kukubalika
kwa ombi la ruzuku ya kufanya uchunguzi huo wa kihabari kutoka Mfuko wa Vyombo
Vya Habari Tanzania (TMF).
Ruzuku ya TMF ililenga
kiujumla kutumia tukio la Kibanda kuwa chanzo cha kutengeneza mazingira salama
zaidi kwa waandishi na wahariri na kwamba kiwango cha matukio ya kuteswa,
kupigwa na kuuawa kwa waandishi yanapungua kila mwaka.
Timu hii imefanya kazi usiku
na mchana kwa kwa zaidi ya mwezi. Timu imezungumza na wadau 26. Kati ya hawa
yumo Kibanda mwenyewe, mke wake, ndugu zake, wasaidizi wake, waajiri wake wa
zamani na wa sasa, viongozi wa kisiasa na vyombo vya dola kutafuta ukweli wa
jambo hili. Pia tumesoma matamko na habari zilizochapishwa kwenye mitandao ya
kijamii na magazeti ya kati ya Machi 5, 2012 na Aprili 5, 2012 kwa nia ya
kufanya ulinganishi wa taarifa tulizozipata kutokana na uchunguzi na habari
zilizochapishwa baada ya kutekwa kwake.
Vyombo vya dola akiwamo
Waziri mwenye dhamana walikataa kuhojiwa wakisema kuna tume ya serikali
inayofanya kazi hiyo na kwamba kuhojiwa kungeonyesha kutokuwa na imani na tume
hiyo.
Leo tunawasilisha
muhtasari wa ripoti hii. Ripoti kubwa pamoja na viambatanisho vyake,
itachapishwa na kuwekwa katika kitabu kimoja. Utaratibu mwingine wa kuchapisha
habari ambazo hazijachapishwa kuhusiana na tukio hili (untold stories) pia
utaandaliwa kwa ushirikiano na Jukwaa la Wahariri kwa nia ya kuieleza jamii
maajabu juu ya kadhia hii.
Tulipewa Hadidu Rejea
ziafuatazo:-
HADIDU REJEA:
1. Kuchunguza
mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya
kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote
vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake.
2. Kuchunguza
mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima
ya Jumanne Machi 5, 2013.
3. Kuangalia
mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006), Ltd na nje ya kampuni
hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka
jana na kuhamia New Habari.
4. Kuchunguza
jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa
kwa Kibanda.
5. Kuchunguza
mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua
kutokana na kile kitakachobainika.
YALIYOJIRI KATIKA UCHUNGUZI:
1.0.
Kuchunguza
mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya
kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote
vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake.
Timu ya uchunguzi
ilitumia muda mwingi katika eneo hili, kubaini iwapo kulikuwapo viashiria,
sababu au matukio ya wazi yenye mwelekeo wa kujitokeza kwa shambulio hili.
Tuliangalia pia iwapo wapo watu au makundi yaliyokwishapata kuonyesha ishara
kwa matendo au kwa kauli juu ya uwapo wa nia hii. Uchunguzi umebaini kuwa kuliwapo
viashiria vingi, isipokuwa Kibanda au watu wake wa karibu hawakupata kufikiri
kuwa huenda vingeweza kuleta madhara makubwa kiasi hiki kama ifuatayo:-
1.1. Wiki tatu kabla ya Kibanda kuvamiwa,
kutekwa na kuumizwa, gari la polisi aina ya gofu Na PT 180 liliwafuatilia kwa
muda mrefu Absalom Kibanda na Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd,
Hussein Bashe likiwa limeegeshwa nje ya ofisi zao Sinza Kijiweni na baadaye likawafuatilia
hadi Sinza Makaburini, ambapo walisimamisha magari yao na kuzungumza na polisi
hao waliosema walikuwa wanatilia shaka magari yao. Baada ya kuzungumza kwa muda
polisi waliondoka.
1.2. Usiku wa Februari 25, mwaka huu majira
ya saa 09:00 usiku, Kibanda walivamiwa na watu walioingia kwenye uzio wa nyumba
yao wakavunja kioo cha gari analotumia, lakini kioo kilipovunjwa ‘alarm’
ilipiga kelele, Kibanda akatoka nje na watu hao wakakimbia.
1.3. Kutokana na uvamizi huo, Kibanda na
wapangaji wengine katika nyumba zilizopo kwenye uzio mmoja, waliona hatari ya
kuvamiwa hivyo wakaanza mazungumzo na kampuni ya Ulinzi ya Kiwango, iliyowataka
kufunga kamera za usalama na kuweka walinzi watano. Hadi Kibanda anatekwa, walikuwa
hawajahitimisha mazungumzo na kampuni hii ya Kiwango.
1.4. Kuna askari anayefanya kazi Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ) miezi minane kabla alipata kumpa Kibanda taarifa za
kinteligensia, kuwa kulikuwapo mpango wa kumteka na kumuumiza. Taarifa kama
hizo pia alipewa na wasamaria wanaofanya kazi katika Jeshi la Polisi. Kwa
maneno yake Kibanda alisema:
“Kuna rafiki yangu askari wa
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kama miezi minane au tisa hivi aliwahi
kuniambia ‘unaandika sana usidhani kama watu wanakupenda. Chukua tahadhari hasa
unapofika getini nyumbani kwako’. Tangu wakati huo nimekuwa nikichukua
tahadhari sana.
“Wiki mbili kabla ya tukio,
niliwahi kuhisi kitu kama hicho [cha kuvamiwa] nikiwa getini. Nilipiga honi
wakachelewa kuja kunifungulia, niliogopa sana. Hata nilipoingia ndani nilikuwa
nimekosa raha kabisa.
“Pia kuna rafiki zangu polisi
waliwahi kuniambia kwamba ninatafutwa na kwamba watu wananifuatilia na ikibidi
wanitengenezee ajali au kunifanyia kama Ulimboka au Kubenea.”
1.5. Ndani ya miezi mitatu mbele ya
mlango wa ofisi yake Kibanda (Free Media Limited) ilikuwa mara kwa mara muda wa
asubuhi anapofika ofisini anakuta damu. Haikufahamika kama damu hiyo ilikuwa ni
ya binadamu, kuku, ng’ombe, kunguru au mbuzi, bali waliipuuza wakidhani ni
masuala ya ushirikina. Mhariri Mtendaji wa sasa, Ansbert Ngurumo, amethibitisha
kuwapo kwa tukio hilo.
1.6. Mfanyakazi mwandamizi wa
Kampuni ya New Habari anakofanya kazi sasa Kibanda ndani ya wiki mbili kabla ya
kutekwa na kuumizwa kwake alipata kumwabia Kibanda maneno mazito mara tatu, na
hapa tunamnukuhu Kibanda:
“Aliniambia Danny Mwakiteleko
[aliyekuwa Naibu Mhariri Mtendaji wa New Habari] hakufa kwa ajali, bali alikufa
kutokana na blood clotting (kuganda kwa damu). Hivyo ikitokea mtu ukapata ajali
au ukapigwa na kuumizwa sana sehemu za kichwa hivi au tumbo, ni lazima
madaktari wadhibiti sana blood clotting.
“Na kweli, nilivyoletwa hapa
Milpark hospitalini, madaktari walikuwa
wananidunga sindano sita kila siku kwenye kitovu kuzuia blood clotting. ....
(jina linahifadhiwa) aliniambia maneno haya mara tatu, katika mazingira
yasiliyotarajiwa na kwa msisitizo ambao sikujua maana yake. Nasema .... (jina
linahifadhiwa) naye achunguzwe kwa kina. Inawezekana kuna jambo analijua.”
Ofisa huyu, alipishana dakika
chache na Kibanda muda wa kutoka ofisini baada ya kipindi cha kwanza cha mechi
kati ya Real Madrid na Manchester united kumaliza nusu ya kwanza (half time).
Dakika ishirini baadaye Kibanda alishambuliwa.
2.0.
Kuchunguza
mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima
ya Jumanne Machi 5, 2013.
2.1. Familia ya Kibanda na Kibanda
Mwenyewe hawakuwa na wasiwasi wowote siku hiyo kwani hawakuwa na hisia wala
wazo kuwa ungetokea uvamizi huo.
2.2. Kibanda alipopiga honi, mlinzi
alisogea langoni kumfungulia. Ghafla akasikia kishindo kikubwa. Akasikia kelele
za Kibanda akiomba msaada. Kijana huyu Baraka Ibrahim mwenye umri wa miaka 27,
aliogopa. Aliogopa kwa mana hakuwa na silaha yoyote mkononi. Hakuwa na panga,
kisu, rungu, wala filimbi. Kwa maneno yake anasema:
“Nilivyoona ningefungua geti
hata mimi ningekufa, nilikimbia kuwaamsha majirani. Sikuwa hata na namba ya
simu ya mtu yeyote kati ya mabosi wangu ninaowalinda. Nilikuwa mimi tu, imani
yangu na Mungu wangu.... kutokana na maisha naifanya hivyo hivyo tu. Vinginevyo
milele nisingefanya kazi hii ya ulinzi.”
Mlinzi huyo alikimbilia kwa
majirani katika nyumba aliyoamini yumo mwanaume, lakini akaanza kumwamsha House
Girl, ili house girl amwamshe baba mwenyenyumba. Kitendo cha kuamshana na
kuwapa taarifa kilichukua dakika tano hadi saba, na ndani ya muda huo, Mlinzi
anasema watekaji wa Kibanda walifanyafanya unyama na uasi huo na kuondoka ndani
ya muda mfupi kiasi hicho. “Watu hawa wana mafunzo maalumu,” anahitimisha.
2.3. Mke wake alikwenda kazini
asubuhi na kurejea nyumbani jioni, lakini tofauti na utaratibu wake wa kawaida
ambapo huwa anaangalia televisheni sebuleni hadi Kibanda anaporejea nyumbani,
siku hiyo alikwenda kuangalia televisheni akiwa chumbani na usingizi ukampitia.
Anasema hakusikia honi wala tukio la Kibanda kutekwa. “Hii inanitesa sana
moyoni. Najiuliza kwa nini siku hiyo tu sikukaa sebuleni? Kwa nini siku hiyo tu
nimelala mapema kabla Baba Joshua hajarudi (machozi yanamlengalenga). Najiuliza
sipati jibu.”
2.4. Mmoja kati ya wasaidizi wawili wa nyumbani kwa
Kibanda, alisikia kelele za Kibanda akiomba msaada. Alimwamsha mwenzake na
kumwambia. “Nasikia Baba Joshua anapiga kelele kama amevamiwa hivi.” Mwenzake
alimwambia “Unaota maana kuna kelele za mpira.” Siku hiyo kulikuwa na mechi
kati ya Real Madrid na Manchester United.
Ni kweli zilikuwapo pia kelele
za wanaoshangilia mpira siku hiyo, hivyo Kibanda alipoomba msaada, hata
waliosikia walidhani watu wanashangilia mpira. Binti aliwaamsha Angela na
mwenzake, wakaenda sebuleni, wakakaa na kuchungulia dirishani, wakaona mwanga
wa gari getini, lakini baada ya kutosikia kelele yoyote wakarejea kulala
wakidhani siye. Lakini binti mmoja alibaki sebuleni. Baada ya muda jirani mmoja
akampigia simu Angela kumweleza kuwa mumewe ameshambuliwa.
2.5. Kibanda kwa upande wake, anasema alipofika
getini, alipiga honi, ghafla akaona watu wawili wamesimama pembeni mwa gari
lake na mtu wa tatu akiwa kwa mbali. Kisha akasikia kishindo kikubwa, akidhani
wanataka kuiba gari, aliatokea mlango wa abiria na kuanza kukimbia huku akiita.
“Mama Joshua nisaidieeeeee.”
Katika kukimbia, aliteleza
akaanguka. Huku watesaji wake wakisema mara tatu “Afande piga risasi.” Kibanda
alijaribu kupambana, akashika rungu, akawahoji amewakosea nini hadi wampige
kiasi hicho, lakini hawakumjibu lolote. Waliendelea kumpiga, hadi akapoteza
fahamu. Hakujua jicho limetobolewa saa ngapi, meno yameng’olewaje na wala pingiri
ya kidole chake imekatawaje. Ifuatayo ni
sauti ya Kibanda mwenyewe. Inasikitisha ila tuwe wavumilivu na tuisikilize.
3.0.
Kuangalia
mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na nje ya kampuni
hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka
jana na kuhamia New Habari.
3.1. Mazingira ya kazi ndani ya New Habari (2006)
Limited na Freemedia Limited, yanaacha maswali kadhaa yenye kustahili majibu. Kama
ilivyoelezwa kwenye Hadidu Rejea Na: 1, ndani ya kampuni ya New Habari imekuwapo
misuguano isiyo na afya kwa kazi ya Kibanda kama mwandishi na tasnia ya habari
kwa ujumla.
3.2. Mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New
Habari (2006) Ltd ni utata. Uhusiano katika chumba cha habari si mzuri. Ndani
ya kampuni hawaaminiani na imefikia hatua wanatuhumiana kuwa huenda baadhi ya
viongozi ndani ya New Habari wamehusika kumteka na kumuumiza Kibanda. Haya
yameandikwa ndani ya mitandao ya kijamii, ikidai kwamba kiongozi mmoja ndani ya
kampuni hiyo alihusika na utekaji wa Kibanda.
Mkurugenzi wa Uhariri,
Prince Bagenda anasema waliohusika kusambaza taarifa chafu dhidi ya kiongozi huyo
wa New Habari wanatoka ndani ya kampuni hiyo.
3.3. Timu ya uchunguzi ilibaini kuwapo
mgawanyiko mkubwa ndani ya New Habari (2006) Ltd kwa kuwapo kundi la ‘Habari
Wazawa’ na ‘Habari wa Kuja’. Malalamiko mengi yanajikita katika msingi kuwa ajira
hazitangazwi na watu wanaajiriwa bila kuzingatia sifa za kitaaluma.
3.4. Kibanda hakuhama Free Media kwa amani. Uchunguzi
unaonyesha kuwa miezi kadhaa kabla ya kuondoka kwake alianza kupoteza mamlaka. Mwenyekiti
wa Kampuni ya Free Media Ltd, Freeman Mbowe alianza kumsikiliza zaidi msaidizi
wake ambaye alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji, Ansbert Ngurumo kuliko yeye Kibanda.
Kwa maneno yake, anasema:
“Nilihofu kuwa Mbowe anaweza kutugombanisha. Nikaona ni bora niondoke
nisije nikagombana na Mbowe au Ngurumo.”
Anasema alianza kupoteza
mamlaka yake na kutoaminika kwa mwajiri wake baada ya kuandika makala kuhusu Abdulrahman
Kinana ambayo kabla ya kuiandika hakuwa na wazo la kuondoka. Yaliyofuata baada
ya makala hiyo, yalimsukuma aondoke.
4.0.
Kuchunguza
jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa
kwa Kibanda.
4.1. Uchunguzi ulifuatilia masuala mbalimbali ikiwamo
mienendo ya watu waliotajwa kwa njia moja au nyingine kuhusinaa na tukio hili.
Hata hivyo, karibu watu wote waliohojiwa, akiwamo Kibanda mwenyewe aliyeumizwa
walimtaja kwa kutilia shaka mwenendo wa kijana Joseph Ludovick. Hofu yao,
iliongezwa nguvu na maandishi aliyoyachapisha Ludovick kwenye mitandano ya
kijamii siku ya Machi 6, 2013.
4.2. Usiku aliotekwa na kuumizwa Kibanda, Ludovick
naye alidai kuwa ametekwa katika eneo la Shekilango na kupelekwa hadi Kigogo.
Baada ya kutekwa aliibiwa kila kitu, ikiwamo begi, laptop, simu mbili, fedha taslimu
Sh 35,000, akavuliwa nguo na kubaki na chupi tu. Pia alieleza kuwa alitoa
taarifa hizo kituo cha polisi Mabibo.
4.3. Maelezo ya Ludovick
yalitiliwa shaka na watu wengi hasa baada ya kueleza kuwa watekaji walitumia
muda wa saa mbili kumtoa Shekilango hadi Mabibo, umbali ambao kwa kiwaida mwendo
wake hauwezi kuzidi dakika 10.
4.4. Daniel Chongolo aliiambia
timu kuwa alfajiri ya Machi 6, siku anayodai kutekwa Ludovick yeye alimuona eneo
la Mabibo wakati anatoka Muhimbili. Taarifa za polisi Mabibo zinaonyesha kuwa Ludovick alitoa taarifa polisi kuwa alikuwa
ametekwa ila akarudishiwa mali zake zote.
“Alipouliza
amefuata nini polisi, akawambia kama raia mwema amefika kuandikisha kumbukumbu
kwa nia ya kuonyesha kiwango cha uhalifu kinavyoongezeka nchini,” kilisema
chanzo chetu kituoni hapo. Timu ya uchunguzi iliamua kutafuta taarifa hizo
baada ya uongozi wa kituo hicho kukataa kupitia leja ya ripoti ya Ludovick.
4.5. Pia taarifa za
uchunguzi wa timu hii zinathibitisha kuwapo kwa utata juu ya madai ya kuibwa
kwa simu za Joseph Ludovick, kwani simu yake ya tigo (inayodaiwa kuibwa)
ilitumika saa 01:21 asubuhi siku ya Machi 6, 2013. Muda huu ofisi za Serikali
na Kampuni ya Tigo zilikuwa hazijafunguliwa
5.0.
Kuchunguza
mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua
kutokana na kile kitakachobainika.
5.1. Uchunguzi umebaini
kuwa maisha ya wanahabari yapo hatarini. Hatari hii inatokana na makundi mengi
yenye masilahi kuwaona wanahabari wanaosimamia ukweli kuwa maadui wa masilahi yao
haramu. Kuna hatari kubwa inayowakabili waandishi wakati nchi inapoelekea
kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.
5.2. Uchunguzi umebaini
kuwa usiri umepungua katika vyombo vya habari. Tofauti na zamani ambapo habari
nyeti ziliandikwa kwa kuhifadhi majina ya waandishi wakitumia jina la MWANDISHI
WETU. Simu hizi hata habari za kutisha waandishi wanaweka majina yao na hata
wasipoweka, ndani ya vyumba vya habari vingi waandishi wapo tayari kutaja nani
ameandika habari fulani.
5.3. Usaliti miongoni mwa
waandishi wenyewe ndani ya vyumba vya habari unazidi kuongezeka na
usipodhibitiwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi. Mwenyekiti wa MOAT, Dk. Reginald
Mengi anasema: “Hili ni jambo muhimu sana. Tuache usaliti vinginevyo wengi
wataumia.”
5.4. Pia alishauri waandishi
wa habari kurejea katika msingi wa taaluma, ambayo inawataka wao kuwa ndio
wenye kuendesha vyombo vya habari badala ya kutegemea matakwa ya wamiliki au
makundi yenye masilahi binafsi.
6.0.
KILICHOBAINIKA:
6.1. Uchambuzi uliofanywa
ni timu hii umebaini kuwa hoja nne zinazungumzwa kuhusiana na kutekwa na
kuumizwa kwa Kibanda. Hoja hizi ni:-
(i)
Kazi yake ya uandishi wa habari
(ii)
Uhusiano wa kisiasa na vyama au wanasiasa mbalimbali
(iii)Uhusiano
wa kijamii ikiwamo mapenzi
(iv)
Vitendo vya rushwa.
6.2. Timu imejiridhisha
kutokana na majibu ya wengi kuwa dhana ya mapenzi na rushwa, havina nafasi
yoyote katika tukio hili. Wote waliohojiwa walieleza pasi na shaka kwamba suala
hili la kushambuliwa na kuumizwa kwa kiwango kikubwa kwa Kibanda, halina
uhusiano wowote na rushwa au mapenzi.
6.3. Kutokana na yaliyotajwa
hapo juu kazi yake na siasa vikiunganishwa vimechangia kwa kiasi kikubwa
kuvamiwa kwa Kibanda. Timu imebaini kuwa
kuna kutupiana mpira kati ya vyombo vya dola na vyama vya siasa. Mchezo huu
mchafu unaweza ukawa mwanzo wa kuumizwa kwa Kibanda na waandishin wengine.
6.4. Baadhi ya waliohojiwa walidai
kuwa utekaji huu umefanywa na vyombo vya dola ukiwa sehemu ya mpango mkakati wa
vyombo hivi kukihusisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na vitendo
vya ugaidi.
6.5. Wanayataja matukio ya
Uchaguzi Mdogo wa Igunga, maandamano ya Morogoro na Mkanda anaodaiwa kurekodiwa
Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare kuwa vililenga kukifanya
CHADEMA kichukiwe na Watanzania kwa kukitaja kama chama cha kigaidi ambacho kinateka
watu na kinawaumiza.
6.6. Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe anadai kwamba mpango kama huo vyombo vya dola viliutumia kwa NCCR
Mageuzi vikakisambaratisha, Chama cha Wananchi (CUF) kilisingiziwa udini
kikapoteza mwelekeo na sasa vyombo hivyo vililenga kukifanya CHADEMA kionekane cha
kigaidi mbele ya macho ya jamii ndiyo maana imerekodiwa mikanda kwa nia ya
kuitumia kujenga hoja hiyo.
6.7. Wakati Mbowe akisema hayo,
baadhi ya watu waliohojiwa wanadai kuwa CHADEMA kimepewa mafunzo na ushauri
kutoka nje ya nchi kuwa kikitumia baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wasiokuwa
waaminifu kuteka, kuumiza na hata kuua baadhi ya watu maarufu nchini wakiwamo
waandishi na wanasiasa, basi wananchi wataamini kuwa Chama Cha Mapinduzi na
Serikali yake kimeshindwa uongozi na sasa kimeanza kazi ya kuua wanaowapinga.
6.8. Kwa njia hiyo,
inaelezwa kuwa hesabu za Chadema ni kuwa wananchi wataichukia CCM na Serikali
yake na kukipa nafasi ya kuingia madarakani. Hapa kauli ya Chadema kuwa NCHI
HAITATAWALIKA itakuwa imetimia.
6.9. Dhana nyingine
iliyojitokeza ni kuwa wapo wafanyabiashara ambao wana vita binafsi, hivyo
wanaamua kuumiza watu wasiowaunga mkono katika mipango yao na hilo ndilo
limemkumba Kibanda, baada ya kuwa ameepusha mauaji ya mwandishi mmoja na aliyekuwa
ameandaa mpango wa kuua mwandishi huyo hakuridhika hivyo akaamua amshughulikie
Kibanda.
7.0.
MAPENDEKEZO:
Baada ya Timu kupata
taarifa hizi na nyingine nyingi, inapendekeza yafuatayo:-
7.1. Taarifa hii ichukuliwe kama
chanzo cha uchunguzi zaidi wa vyombo husika.
7.2. Yanahitajika marekebisho
makubwa na ya haraka katika mifumo ya uendeshaji wa vyumba vya habari kwa nia
ya kurejesha misingi ya uandishi wa habari inayokubalika.
7.3. Usalama wa wanahabari
unapaswa kupewa kipaumbele na wamiliki, wanahabari wenyewe na jamii kwa ujumla.
Hapa Timu inapendekeza yawepo mafunzo ya kuwawezesha wanahabari kutambua
viashiria vya hatari na kuchukua hatua mara moja.
7.4. Kwa kiwango alichoumizwa
Kibanda iwapo mwajiri wake asingejitolea kugharamia matibabu, hatujui hatima
yake ingekuwaje leo hii. Tunapendekeza taasisi na mifuko mbalimbali
inayojihusisha na masuala ya wanahabari kama Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ,
Baraza la Habari Tanzania (MCT), Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) na
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kuanzisha mfuko wa pamoja
utakaotumika kugharamia matibabu ya waandishi watakaoumia wakiwa kazini.
7.5. Tukio la kutekwa kwa Kibanda
limeonyesha mwanga kuwa wahariri tumegawanyika mno. Habari zilizochapishwa
katika magazeti mbalimbali na mitandao ya kijamii zimeonyesha haja ya kuwafanya
wahariri kuwa kitu kimoja kwa kuondoa tofauti zao zisizo na masilahi kwa tasnia
ya habari.
7.6. Kuna viashiria vingi kuwa
kuelekea mwaka 2015 matukio ya waandishi kuumizwa au kutekwa yanaweza kuongezeka
kutokana na wanasiasa na vyama kuwania madaraka huku wakitumia baadhi ya
watumishi katika vyombo vya dola. Kwa mantiki hiyo, vyombo vya habari na
waandishi wa habari wachukue tahadhari kuanzia sasa.
7.7. Taasisi za habari zifanye
juhudi za makusudi kukutana na vyama viwili vya siasa vya CCM na CHADEMA haraka
iwezekanavyo, kuzungumzia viashiria hivi vya hatari vinavyoelekea kuvuruga
amani ya Tanzania.
8.0.
HITIMISHO:
Ni dhahiri kuwa kupigwa
na kuteswa kwa Kibanda kumejiegemeza katika siasa na kazi yake, hali inayofanya
makundi muhimu kuchukua wajibu wa msingi. Kwa upande wa Serikali ni muhimu
kufuatilia viashiria katika taarifa hii kwa nia ya kupata ukweli zaidi na
kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya wahusika.
Na kwa upande wa vyombo vya habari na taasisi za kihabari zinapaswa
kutambua viashiria vinavyohatarisha usalama wa waandishi wa habari na wahariri
na kutengeneza mazingira yatayokuwa salama zaidi kwa waandishi kufanya kazi zao.
9.0.
SHUKRANI:
9.1. Tunapenda kulishukuru Jukwaa
la Wahariri Tanzania, kwa kufanya uamuzi sahihi wa kuwezesha kufanyika kwa
uchunguzi huu ulioanza kuonyesha mwanga wa nini kilitokea.
9.2. Tunapenda kulishukuru Baraza
la Habari Tanzania (MCT) kwa kushiriki kikamilifu na kuiwezesha timu hii kwa
Rasilimali Watu na Mali kufanikisha kazi hii.
9.3. Tunapenda kuwashukuru Mfuko
wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa uwezeshaji wa ruzuku, uliofanikisha kufanya
uchunguzi wa kihabari uliohusisha kwenda nchini Afrika Kusini kufanya mahojiano
na Kibanda. Uwezeshaji huo pia unahusisha kutengeneza mwongozo kwa waandishi
wenye lengo la kuwaepusha na hatari za kiusalama.
9.4. Tunawashukuru Kibanda, mkewe
Angela, wanafamilia, ndugu na jamaa wa Kibanda na wanahabari wote waliohojiwa kwa
ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Timu hii.
9.5. Tunawashukuru wahariri wote
kila mtu kwa nafasi yake, kutokana na ushauri wa mara kwa mara mliotupatia
katika kufanikisha uchunguzi huu.
10.
WAJUMBE
WA TIMU:
Timu hii iliundwa na wajumbe
watano ambalo ni:
1. Deodatus
Balile – Mwenyekiti
2. Pili
Mtambalike – Mjumbe
3. Jane
Mihanji – Mjumbe
4. Tumaini
Mwailenge – Mjumbe
5. Rashid
Kejo – Katibu
Mwisho.....
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment