Kamati ya ulinzi na usalama ya  bunge imewasilisha   azimio la kuitaka serikali kuimarisha  masuala ya ulinzi na usalama ikiwa ni siku chache tu tangu kutokea kwa tukio la shambulio la bomu lilitokea katika kanisa la Mtakatifu Joseph jimbo la Arusha.

Akiwasilisha azimio hilo bungeni mjini Dodoma,mwenyekiti wa kamati hiyo Mheshimiwa Anna Abdallah ameitaka serikali kuhakikisha inachukua hatua stahiki ili vitendo kama hivyo visijitokeze katika siku za usoni.

Aidha amesema serikali inapaswa kuchukua hatua kali za kisheria kwa viashiria vyotevyote vyenye kuchochea chuki na kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu uliokuwepo kwa muda  mrefu nchini.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa tukio hilo limewasababishia hofu wananchi katika shughuli zao mbalimbali hivyo kupitishwa kwa azimio na utekelezaji wake utachangia kurejesha amani na utulivu kwa wananchi.

Nao wabunge mbalimbali waliochangia katika azimio hilo wamesema sheria zitungwe ili kuwabana hata viongozi wenye kinga ya kutoshitakiwa wakiwemo wabunge kutosema kauli zenye mwelekeo wa kuvunja amani ya nchi.

Awali kabla ya azimio hilo Spika wa bunge Anne Makinda  amesema azimio la kamati hiyo lilipendekeza wabunge kutembelea kanisa la Mtakatifu Joseph na kwamba  posho ya  wabunge  ya siku moja itatumika kuwafariji waathirika wa tukio hilo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top