Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetaka Jeshi la Polisi
nchini livunjwe na ligeuzwe kitengo ndani ya Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ).
Msimamo huo umetolewa jana bungeni na baadhi ya wabunge wa chama hicho
walipokuwa wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi iliyowasilishwa na Waziri Emmanuel Nchimbi.
Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde, alisema Jeshi la Polisi
limeoza, kwa sababu limeshindwa kutekeleza wajibu wake kikamilifu,
ikiwamo kuwakamata wahalifu mbalimbali wanaoshiriki kwenye matukio ya
kihalifu.
“Napendekeza Jeshi la Polisi livunjwe na liingizwe ndani ya Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liwe sehemu ya kitengo katika jeshi hilo.
“Naamini kwa kufanya hivyo tutaboresha utendaji wake, silaha kubwa
iliyobaki kulinusuru taifa hili kwa sasa ni kusema ukweli, kwani bila
kufanya hivyo miaka sita ijayo hali itakuwa mbaya,” alisema.
Aliongeza kuwa lazima Watanzania wakubali kuwa nchi imegubikwa na
matukio ya udini na ukabila, ingawa serikali ama kwa kufanya makusudi au
rais na Waziri Nchimbi kudanganywa wamekuwa wakishindwa kuchukua hatua.
Silinde alisema kuwa kama ilivyoandikwa kwenye maandiko matakatifu
kuwa itafika wakati wenye macho hawataona na wenye masikio kutosikia, na
kuifananisha hali hiyo na CCM ya sasa.
Mbunge huyo aligusia tukio la Arusha akisema huo ni mwendelezo wa kile
walichokipanda CCM kwa kutochukua hatua kwa watu wanaochochea vurugu
hizo za udini.
“Serikali ya CCM haioni tena, haisikii wala haiwezi kunusa tena, hili ndilo anguko la serikali hii,” alisema.
Hata hivyo alimshangaa Waziri Nchimbi kwa kumtaja mtuhumiwa mmoja kwa
jina na kuwaacha wengine watano aliodai ni raia wa kigeni, akisema huo
ni mwendelezo wa kuficha maovu.
“Kama huyu mmoja katajwa, kwanini hao wengine wasitajwe? Tunaficha
nini? Ama ndio mwendelezo huo huo wa kutaka kupindisha ukweli wa tatizo
na kuibua mambo mengine?
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu ‘Sugu’ alisema
serikali imekosa mikakati ya kutuliza vurugu hizo na badala yake inakuja
na maneno ya kisiasa yasiyo na ufumbuzi wa tatizo.
Sugu alishauri Jeshi la Polisi livunjwe kwa kushindwa kazi na kisha
liundwe upya kwa kuwapa kazi vijana wasomi ambao wana uwezo mkubwa
badala ya kung’ang’ania kuwaongeza wastaafu mikataba.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), alisema vitendo
vya vurugu za kidini vinavyoendelea nchini ni matunda ya serikali ya
CCM.
Lissu alianza kujenga hoja yake akitumia usemi wa mwanafalsafa mmoja kuwa hakuna uchochezi mkubwa kama kukaa kimya.
Alisema kile kilichotokea Arusha juzi pamoja na matukio ya kuvamiwa
kwa viongozi wa kidini visiwani Zanzibar ni ukimya wa serikali ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ikiwa ni pamoja na kuchochea matendo hayo.
“Nchi hii imeshuhudia baadhi ya watu wakifanya mihadhara ya kidini na
kuhamasisha uchochezi, magazeti yanaandika kuchochea udini, zipo radio
zinatangaza kashfa mbalimbali dhidi ya dini nyingine, lakini serikali
hii iko kimya.
“IGP Omar Mahita, alitangaza mchana kweupe kuwa Chama cha Wananchi
(CUF) ni cha kigaidi, akaonesha na visu kwenye vyombo vya habari, lakini
serikali hadi leo haijasema kitu juu ya hilo,” alisema.
Lissu aliongeza kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, CCM iliweka
kwenye ilani yake kuwa itawapatia Waislamu Mahakama ya Kadhi na ilipoona
haiwezi kufanya hivyo ikawasingizia maaskofu kuwa ndio hawataki
mahakama hiyo iwepo.
Lissu alifafanua kuwa hali imekuwa mbaya kutokana na uchochezi huo
ulioasisiwa na serikali ya CCM halafu sasa inageuka na kuanza kutaka
kujinasua.
“Tumeambiwa tusimlaumu mtu katika tukio hili la Arusha, nami nakubali
ila ninachosema ni kwamba huu ni wakati wa Waziri Nchimbi kuachia ngazi
mwenywewe kutokana na kushindwa kazi ama awajibishwe.
“Huu ni wakati wa IGP Said Mwema kujiuzulu na akishindwa awajibishwe kwa kushindwa kazi,” alisema.
Lissu alisema kuwa serikali ya CCM ndiyo imepalilia uchochezi wa udini
na ukabila nchini kama kinga ya kujilinda na kasi ya vyama vya
upinzani.
“Serikali hii ndiyo ilisema CHADEMA ni chama cha Wachaga, serikali hii
ndiyo ilisema CHADEMA ni chama cha Wakristo, ni chama cha Wakatoliki.
Leo wanajigeuza na kuanza kujifanya wanachukia vitendo hivi.
“Mheshimiwa Spika lazima tuambiwe kwanza CUF imeacha lini kuwa chama
cha kigaidi na Uislamu wenye itikadi kali, CHADEMA kimeacha lini kuwa
chama cha Wachaga, Wakristo na Wakatoliki?” alihoji Lissu.
Nchimbi atoa kauli
Mapema akisoma kauli ya serikali bungeni kueleza mlipuko huo wa
Arusha, Waziri Nchimbi alisema idadi ya watu waliokufa ni wawili baada
ya mmoja kuongezeka usiku wa kuamkia jana.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Regina Kurusei (45) aliyefariki juzi
akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount Meru na James Gabriel (16)
aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana huku watu wengine 59 wakiachwa
majeruhi, ambapo miongoni mwao watatu ni mahututi.
Dk. Nchimbi alisema kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mlipuko huo
ni bomu na kwamba uchunguzi wa kubaini aina ya bomu lililotumika
unaendelea kufanywa na Jeshi la Polisi na wataalamu wa JWTZ.
“Hadi sasa watuhumiwa sita wanashikiliwa na polisi. Miongoni mwao ni
Victor Ambrose (20) dereva wa bodaboda, mkazi wa Kwa Mrombo, Arusha
ambaye anatuhumiwa kurusha bomu hilo. Watuhumiwa wengine watano
waliokamatwa ni raia wanne wa kigeni na Mtanzania mmoja, ambao
wanashikiliwa kwa mahojiano,” alisema.
CCM yanena
Nacho Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu Mkuu wake,
Abdulrahman Kinana, kimeeleza kusikitishwa na kitendo hicho cha
kulipuliwa kwa kanisa mjini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Kinana alisema
kuwa CCM imeguswa na tukio hilo na kwamba wanalilaani kwa nguvu zote
pamoja na kuitaka serikali kufanya kila mbinu kuwakamata wahusika na
kuwachukulia hatua.
Kinana alitoa pole kwa waathirika wa tukio hilo wakiwamo wafiwa,
majeruhi pamoja na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, akisema kuwa
wanaamini kuwa serikali itachukua kwa karibu kila taarifa kuhusiana na tukio hilo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment