MSEMAJI Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Maliasili
na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa.
MSEMAJI Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Maliasili
na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, amewalipua vigogo wa serikali na
makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akidai kuwa wana maslahi
yanayotilia shaka katika sekta ya uwindaji wa kitalii na kusababisha
kuwapo kwa ujangili.
Kama alivyofanya mwaka jana na hata kwenye mikutano yake mingi ya
hadhara, Msigwa alimtaja tena Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na
mkewe, kwamba anamiliki kampuni ya Sharaf Shipping Co, Ltd ambayo meli
yake inadaiwa kunaswa na kontena la shehena ya meno ya tembo.
Hata hivyo, hotuba ya Msigwa ilikatizwa kwa mwongozo wa mbunge wa Viti
Maalumu, Anna Abdallah (CCM), akihoji kitendo cha mbunge mwenzake kudai
ofisi ya Spika ni kaburi la kuzika haki. Hata hivyo Spika Anna Makinda
aliwataka wawe wavumilivu kwani yako maneno mengine mengi kama hayo.
Hata hivyo Msigwa aliendelea kusoma maoni ya kambi ya upinzani kuhusu
makadirio ya matumizi na mapato ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa
mwaka wa fedha wa 2013/14.
Huku wabunge wa CCM wakimwangalia kwa makini na wengine kutikisa
vichwa kumpinga, Msigwa alimtaja mfanyabiashara na kada wa CCM, Mohsin
Abdallah.
Msigwa ambaye alikuwa akikariri taarifa ya kamati ya waziri wa zamani
wa wizara hiyo, Antony Diallo, aliwataja makada waandamizi wengine wa
CCM wenye maslahi ya aina hii kuwa ni kampuni ya Coastal Wilderness (Tz)
Ltd., ambayo wakurugenzi wake wanatajwa kuwa ni Napono Edward Moringe
Sokoine na Namelok Edward Moringe Sokoine; Enzagi Safaris (Tz) Ltd.,
yenye wakurugenzi Makongoro Nyerere, Muhamed Seif Khatib na Saidi
Kawawa; na Hunting Safaris yenye wakurugenzi, Chande Kawawa na Hassan
Kawawa.
Kampuni zingine ni M.S.K. Tours & Hunting Safari Co. ya Muhamed Seif Khatib.
Msigwa alisema mengi ya makampuni haya yalipewa vitalu vya uwindaji
wakati hayana uzoefu wala mtaji wa kuendesha biashara ya uwindaji wa
kitalii katika vitalu hivyo.
Alisema matokeo yake ni kwamba makampuni hayo yalishindwa kusimamia
uhifadhi wa wanyamapori katika vitalu vyao na kusababisha tatizo la
ujangili kushamiri katika vitalu hivyo.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa kauli mbele
ya Bunge lako tukufu ni kwa nini serikali hii ya CCM imekuwa ikitoa
vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa makada waandamizi wa CCM ambao
wanajulikana kuwa hawana weledi wala uwezo wa kibiashara wa kuendesha
biashara ya uwindaji wa kitalii na hivyo kusababisha tatizo la ujangili
kuwa kubwa zaidi na kuleta hasara kwa taifa letu!” alisema.
Akiwa amerejea bungeni baada ya adhabu ya siku tano, Msingwa alisema
serikali imeanza kufedheheshwa katika mikutano ya kimataifa ya uhifadhi
kwa sababu CCM imeamua kukumbatia makada wake waandamizi aliodai
wanajihusisha na ujangili.
Alitolea mfano Mkutano wa 16 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Biashara
ya Kimataifa ya Wanyama Walio Hatarini Kutoweka (CITES) uliofanyika
Bangkok, nchini Thailand mwezi uliopita.
Msigwa alisema kuwa Mohsin Abdallah alitajwa na Shirika la Upelelezi
wa Masuala ya Mazingira (Environmental Investigations Agency, EIA) kuwa
ni mmoja wa majangili wakubwa wanaojihusisha na biashara haramu ya meno
ya tembo lakini serikali imeshindwa kumchukulia hatua za kisheria kwa
sababu ya ushawishi wake mkubwa katika siasa za ndani ya chama tawala na
serikali.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni fedheha ya aina gani
kimataifa itakayoiamsha serikali hii ya CCM katika usingizi wake wa
pono ili iweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya makada wa CCM wa aina
hii?”alihoji Msigwa.
Kuhusu Kinana, Msigwa alisema kampuni yake ya wakala wa meli ya Sharaf
Shipping Co. Ltd, si tu kwamba imehusishwa na usafirishaji haramu wa
pembe za ndovu kutoka Tanzania bali pia inadaiwa kutoa ajira haramu kwa
wageni.
Alisema wakati shehena ya meno hayo ya tembo inakamatwa nchini
Vietnam, nyaraka zilizoambatana na shehena hiyo zilionyesha kwamba
kibali cha kusafirisha shehena hiyo kilisainiwa na raia wa India
anayeitwa Samir Hemani mnamo Novemba 13, 2008.
Alisema wakati raia huyo wa kigeni anasaini kibali cha kusafirisha
shehena ya meno ya tembo kwa niaba ya wateja wa Kinana na mkewe, kibali
chake cha kuishi Tanzania kilikuwa kimeisha tangu Mei 7, 2008.
Msigwa alimshambulia Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis
Kagasheki, na kumtaka ajiuzulu kwa madai kuwa ameshindwa kulinda
rasilimali za nchi na kusababisha wanyamapori kutoweka kwa kuuawa na
majangili.
Alimshambulia pia Spika Anna Makinda kuwa Bunge lake limekuwa kaburi
la kuzikia utekelezaji wa maazimio mengi kuhusu kashfa mbalimbali
zilizogubika utendaji wa Ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii na
utekelezaji wa majukumu yake kisheria.
Nchimbi ajibu mapigo
Hoja za Msigwa zilimlazimu Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel
Nchimbi, kuomba nafasi ya kwanza kuchangia hotuba ya Waziri Kagaeshiki
na hivyo kutumia muda huo kurusha makombora mazito kwa CHADEMA kwa
kuwaita kuwa ni genge la uongo ndani ya Bunge.
“Kabla sijaendelea, nitumie nafasi hii kuipongeza Wizara ya Maliasili
na Utalii kwa kazi nzuri na katika hotuba hii ya Waziri Kagasheki
imejidhihirisha wazi kwa kipindi hiki kifupi kuwa wamekamata watuhumiwa
wa ujangili 354 na zipo mahakamani kesi 283, bunduki 435 zimekamatwa.
“Ukiona mtu anasimama na kusema serikali haijafanya kazi, basi upeo wake wa kufikiri ni mdogo,” alisema Nchimbi.
Waziri huyo alijielekeza kwenye baadhi ya hoja zilizolengwa dhidi ya
Kinana ambapo alisema Msigwa ameamua kusema uongo ili kulipotosha Bunge
na Watanzania kwa ujumla kwamba katibu huyo alikamatwa na meno ya tembo
nje.
“Nimejaribu kufuatilia kwa umakini kujua kwamba kifungu hicho
alikimaanisha, alikielewa, alikitafakari au aliandikiwa tu kisha akaenda
kukisoma.
“Baada ya kutafakari kwa kina nimegundua kwamba hakuwa na nia mbaya bali alikuwa ameandikiwa tu na kuisoma,” alisema.
Nchimbi alitumia muda huo kufafanua majumu ya kati ya Shipping Agency na Clearing and Fowarding.
“Kampuni ya shipping agency duniani kote ni kumwakilisha mwenye meli,
agenti hawezi kuwa mwenye meli ila anamwakilisha mwenye meli, kuna
shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye meli.
“Kuna mambo ya kuhudumia watumishi kwenye meli, kuwapelekea chakula
watumishi, kufanya usafi, kupelekea mahitaji muhimu lakini wapo watu
wanaofanya ‘clearing and fowarding’ na Kiswahili chake ni kupeleka na
kutoa.
“Hawa ndio wanaopeleka mizigo bandarini na kule ndiko kuna utaratibu
wa upekuzi kwa hiyo huko hahusiki mtu wa shipping agency, sina mashaka
hata kidogo kuwa Mchungaji Msigwa analijua hili ila amelifumbia macho
kwa makusudi na kwa maslahi yasiyokubalika kwa taifa,” alisema.
Wakati akiendelea kuchangia, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
(CHADEMA), aliomba mwongozo wa Spika kutaka kutoa ufafanuzi, lakini
Spika alikataa.
“Mliposema ninyi, wenzenu walinyamaza, mtulie hivyo hivyo, naomba
uendelee hakuna cha taarifa, endelea Mheshimiwa Nchimbi na nyie
mnanyamaza kama walivyonyamaza wenzenu,” alisema Makinda.
Nchimbi aliendelea kusema kumekuwepo uvumi ambao unafanywa kwa Kinana
kwamba anamiliki meli iliyotumika kusafirisha pembe za ndovu.
Alisema baada ya uchunguzi wa kutosha kuhusu kesi hii, ikabainika na
watuhumiwa wakashtakiwa kwa uhujumu uchumi kwa kufunguliwa kesi namba 3
na 4 ya mwaka 2006.
Nchimbi aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Eradius Tesha, Shaban Abura, Eric, Issa Abubakar na Omar Hussein.
“Mh Spika, hawa ndiyo waliopelekwa mahakamani na uchunguzi
ulijidhihirisha kuwa hawa ndiyo watuhumiwa wa kesi hiyo na kambi ya
upinzani inalijua hili,” alisema.
Alisema wakati kesi iko Kisutu, ulihitajika ushahidi kutoka nchi ya
Vietnam na nchi hiyo imesema haina ushirikiano na Tanzania katika mambo
ya jinai.
“Hivi sasa tunazungumza na ubalozi wa China watupe kibali cha kufanya
upelelezi ili kesi hiyo iweze kuendelea na kwa msingi huo Mahakama ya
Kisutu inataka ushahidi huo ili kesi iendelee na hili wapinzani
wanalijua,” alisema.

0 comments:
Post a Comment