Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
WAZIRI
MKUU, Mizengo Pinda amewaonya baadhi ya watu wanaofanya ushabiki wa kisiasa kwenye
tukio la mlipuko wa Arusha na kuwataka wasitumie tukio hilo kujipatia umaarufu
na badala yake watumie fursa hiyo kuwafariji walioathirika na kuwa watulivu
hadi suala hilo lifikie hatma yake.
Waziri Mkuu amesema tukio hilo ni
kubwa, na kitendo hicho ni kibaya kinachostahili kulaaniwa vikali kwa hiyo
haifai watu wachahe kujipatia umaarufu kupitia tukio hilo.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Jumanne,
Mei 7, 2013) wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwatembelea
ili kuwajulia hali majeruhi waliolazwa kwenye Hospitali ya Mount
Meru, jijini Arusha.
Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na
hali ya utulivu wa wananchi wa Arusha na hasa waliokaribu na Kanisa la Mt. Joseph
Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, kufuatia mlipuko wa mabomu uliotokea Jumapili
iliyopita, Mei 5, mwaka huu.
Alisema ameguswa pia na hali ya
matibabu inayotolewa kwa majeruhi katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount
Meru, jijini Arusha.
Waziri Mkuu alikatisha shughuli za
Bunge jana mchana na kuelekea Arusha. Mara baada ya kuwasili KIA jana jioni,
Waziri Mkuu alikwenda moja kwa moja Parokia ya Olasiti ili kujionea hali halisi
na kuwapa pole wamunini wa Kanisa hilo.
Baadaye alikwenda kumjulia hali
Askofu wa Jimbo Kuu la Arusha, Mhashamu Josephat Lebulu pamoja na Balozi wa
Vatican, Mhashamu Askofu Fransisko Padilla ambako alifanya nao mazungumzo na
kuwahakikishia viongozi hao kwamba Serikali itafanya kila iwezalo hadi iwabane
wahusika.
Akiwa hospitali ya Mount Meru leo
asubuhi, Waziri Mkuu alimweleza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Frida Mokiti
kuwa asisite kuwasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Magesa Mulongo endapo
hali ya majeruhi itabadilika na watahitaji matibabu zaidi.
Katika ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu
alikabidhi vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 23.3 ambavyo ni dawa na vifaa
tiba kwa uongozi wa hospitali hiyo ambavyo vilitolewa na Shirika la Hifadhi za
Taifa (TANAPA) chini ya uhamasishaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kukabidhi misaada hiyo, Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu alisema jana (Jumatatu, Mei
6, 2013), TANAPA ilitoa mablanketi 50 hospitali hiyo na kwamba wafanyabiashara
wa sekta ya utalii wa mjini Arusha wamejipanga kutoa msaada zaidi ili kuisaidia
hospitali hiyo kumudu kuwahudumia majeruhi wa mlipuko huo.
Hadi sasa, watu watatu wamepoteza
maisha kutokana na mlipuko huo ambapo watu wanane wamekamatwa na kuhojiwa na
polisi. Kati yao, wanne ni raia wa Saudi Arabia na waliobakia ni wakazi wa
Arusha. Polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tulio hilo.
Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu,
Mkuu wa Mkoa wa Arusha alisema wagonjwa watatu wana hali mbaya ambapo mgonjwa
mmoja yuko Muhimbili na wawili wako hapo hapo Mount Meru.
“Watu 66 waliathirika na mlipuko
huo, watatu wamefariki na kati ya wagonjwa 63 waliobakia, wagonjwa 24 wamesharuhusiwa
kurudi nyumbani, waliobakia wanaendelea kupatiwa matibabu,” alisema.
Waziri Mkuu amerejea Dodoma mchana
huu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment