Kikosi cha Taifa Stars.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen
leo (Mei 16 mwaka huu) ametaja kikosi cha wachezaji 26 watakaoingia kambini
kujiwinda kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayochezwa
Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech, Morocco.
Katika kikosi hicho, Kim ameita
wachezaji wapya sita ingawa baadhi yao wamewahi kuchezea timu hiyo, huku
akiacha wengine watatu aliokuwa nao kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Morocco
ambapo Taifa Stars ilishinda mabao 3-1.
Wapya aliowaita katika kikosi hicho
kitakachoingia kambini Mei 20 mwaka huu, saa 1 jioni kwenye hoteli ya Tansoma
jijini Dar es Salaam ni Ally Mustafa, Vicent Barnabas, Juma Luzio, Haruna
Chanongo, Mudhathiri Yahya na Zahoro Pazi. Wachezaji aliowaacha ni Shabani
Nditi, Nassoro Masoud Cholo na Issa Rashid.
Kikosi kamili cha Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ambacho kabla ya kwenda Morocco
kitapita jijini Addis Ababa, Ethiopia kucheza mechi ya kirafiki Juni 2 mwaka
huu dhidi ya Sudan ni kama ifuatavyo;
Makipa ni nahodha Juma Kaseja (Simba),
Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni
Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub
(Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Vicent Barnabas (Mtibwa Sugar) na Waziri
Salum (Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman
Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam),
Mwinyi Kazimoto (Simba), Mudathiri Yahya (Azam) na Salum Abubakar (Azam).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam),
Juma Luzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP
Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na Zahoro Pazi (JKT Ruvu).
Kocha Kim amesema kikosi kitakachoingia
kambini kitakuwa na wachezaji 24 ambapo Samata na Ulimwengu watajiunga na timu
jijini Marrakech, lakini wachezaji atakaondoka nao Dar es Salaam kwenda Addis
Ababa ni 22 ambapo ataacha kipa mmoja na mchezaji mmoja wa ndani.
Awali TFF ilikuwa imeitafutia Taifa
Stars mechi ya kirafiki Juni 1 mwaka huu dhidi ya Algeria, Libya au Misri.
Lakini baadaye Algeria ikasema itacheza na Togo, wakati Misri ilitaka mechi
hiyo ichezwe Juni 4 jijini Cairo, jambo ambalo lisingewezekana kwa Stars kwani
ina mechi ya mashindano Juni 8 mwaka huu.
Kwa upande wa Libya mechi hiyo
ilikubaliwa ichezwe Tunis, Tunisia, Juni 2 mwaka huu. Lakini baadaye Libya
ikataka mechi hiyo ichezewe jijini Tripoli ambapo TFF ilikataa kutokana na
sababu za kiusalama.
TIKETI SIMBA, YANGA KUANZA KUUZWA KESHO
Kikosi Cha Simba
Kikosi cha Yanga
Tiketi kwa ajili ya pambano la Ligi Kuu
ya Vodacom kati ya Simba na Yanga litakalochezwa keshokutwa (Jumamosi) kwenye
Uwanja wa Taifa zitaanza kuuzwa kesho (Ijumaa) kwenye vituo mbalimbali jijini
Dar es Salaam.
Vituo vitakavyouza tiketi hizo kuanzia
saa 3 asubuhi hadi saa 10 jioni ni Uwanja wa Taifa, mgahawa wa Steers ulioko
Mtaa wa Ohio na Samora, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, OilCom Ubungo, kituo
cha mafuta Buguruni, BMM Barbershop Sinza Madukani, Dar Live Mbagala na Sokoni
Kariakoo.
Tiketi hizo zitakuwa zikiuzwa katika
magari maalumu yaliyoegeshwa katika vituo hivyo. Viingilio katika mechi hiyo ya
kufunga msimu ni sh. 5,000 kwa viti vya kijani, sh. 7,000 viti vya bluu, sh.
10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B n ash.
30,000 kwa VIP A.
TANZANIA YAJIONDOA MICHUANO YA COSAFA
Tanzania (Taifa Stars) imejitoa kwenye
michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA)
itakayofanyika nchini Zambia kuanzia Julai 2-26 mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah amesema Stars ambayo iliingizwa katika
michuano hiyo kama timu mwalikwa imejitoa kutokana na mwingiliano wa ratiba
kati ya michuano hiyo na mechi za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani
(CHAN).
Amesema awali Tanzania ilithibitisha
kushiriki michuano kwa matarajio kwamba Uganda ingekubali ombi la TFF la
kubadilisha ratiba ya mechi za CHAN, lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda
(FUFA) likagoma kwa vile kipindi ambacho kilipendekezwa lenyewe litakuwa na
uchaguzi wa viongozi wao.
Taifa Stars itacheza na Uganda (The
Cranes) katika mechi za CHAN ambapo mechi ya kwanza itachezwa jijini Dar es
Salaam kati ya Julai 12-14 mwaka huu wakati ya marudiano itafanyika jijini
Kampala kati ya Julai 26-28 mwaka huu.
Akizungumzia michuano ya COSAFA, Kocha
Kim amesema angependa kushiriki michuano hiyo kwani ingekuwa kipimo kizuri kwa
kikosi chake, lakini kwa sasa malengo makubwa ya Stars kwenye mechi za mchujo
za Kombe la Dunia na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambayo
fainali zake zitafanyika mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment