Mbunge wa kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
  •  Asema deni linalodaiwa serikalini limepanda kutoka Tsh. 3.4 trilioni hadi 6 trilioni.
  •   Serikali yalipa deni la Tsh. 30 bilioni tu.
  •   Akiri PSPF ilifilisika tangu Juni, 2011.
Yafuatayo ni maelezo ya Zitto kuhusu PSPF yaliyopatikana katika ukurasa wake wa facebook.
Mwaka 2011 Mwezi Aprili iliyokuwa Kamati ya POAC ilitoa taarifa yake Bungeni kuhusu suala la madeni inayodaiwa serikali na Mfuko wa PSPF. Wakati huo deni lilikuwa ni Tshs 3.4 trilioni. CAG katoa taarifa yake kwa Umma jana na kusema kuwa hivi sasa deni limefikia zaidi ya tshs 6 trilioni.

Katika taarifa ya Kamati tulionyesha kuwa Serikali ilikiri kudaiwa na kuahidi kuanza kulipa. Kisha wakalipa tshs 30bilioni. Kumbe baadaye hawakulipa tena na uchambuzi wa "acturials" umeonyesha ukubwa wa deni karibu mara mbili ya ilivyokuwa mwaka 2010.

Kwenye nchi za wenzetu Pensheni ni siasa kubwa sana. Nashukuru leo magazeti mengi yametoa kipaumbele kuhusu suala hili. Naomba pia group letu hili tujadili kwa kina tatizo hili.

Ilikuwaje?

Mwaka 1999 Serikali iliamua kuunda PSPF na kuachana na mtindo wa Serikali kulipa pensheni kutoka kwenye bajeti na badala yake watumishi wachangie pensheni zao. 
Hata hivyo kulikuwa na madeni ya pensheni ya miaka ya nyuma ya zaidi ya Tshs. 600 bilioni ambazo serikali iliahidi kulipa. Mfuko ukaanza kwa kulipa pensheni kutokana na michango ya wanachama. 
Serikali haikulipa licha ya kukiri 'liability' hiyo. Mwaka 2011 POAC ikaibana serikali kulipa na ikalipa kiduchu. Haikulipa tena.
 Hivi sasa deni ndio hilo Tshs 6 trilion. Kimsingi mfuko huu ulifilisika mwezi Juni mwaka 2011. Huu ndio mfuko wenye wastaafu wengi zaidi nchini kuliko mifuko yote na ndio mfuko unalipa wastaafu kiwango kidogo sana (ilikuwa 20,000 Tshs na sasa ni 50,000 sawa na PPF na chini kidogo ya NSSF ambayo inalipa 80,000).

Extract ya Taarifa ya POAC, Aprili 2011

2.4.5 Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa umma (PSPF)

Mheshimiwa Spika, Tathimini iliyofanyika katika mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya umma (PSPF) ulibaini tatizo kubwa la madeni ambayo Mfuko unaidai , Serikali mengi yakiwa ni ya siku za nyuma kabla ya mwaka 1999 ambapo baadhi ya watumishi wa umma walitakiwa kulipwa pensheni lakini hawakuwa wakichangia kwenye mifuko ya Hifadhi za jamii hivyo Serikali ikachukua deni hilo la shilingi trilioni 2.6 na shilingi bilioni 719 ambazo PSPF imekwisha lipa wastaafu baada ya kuanzishwa kwake.

Baada ya kupokea hoja za ukaguzi za taarifa ya hesabu ya PSPF, Kamati ilipata wasi wasi juu ya ukubwa wa deni hilo na hivyo kuamua kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na uchumi ili kulijadili deni hilo kwa kina.

Mheshimiwa Spika, Kikao hicho muhimu kilifanyika tarehe 25/03/2011 ambapo majadiliano hayo yalizaa matunda, Kamati inapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali ilianza mara moja kulipa deni hilo na kwa mwezi Machi 2011 Serikali imeilipa PSPF shilingi bilioni 30 kwa bajeti ya mwaka 2009/2010 na imetoa uthibitisho wa kuendelea kulipa deni hilo kwa kutenga kipaumbele katika bajeti ya mwaka husika.
Zitto  
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top