Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano , Mh. Anne Makinda

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mh. Anne Makinda ameliambia bunge leo asubuhi kuwa adhabu iliyotolewa kwa wabunge sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni sahihi hivyo wahusika wataendela kuitumikia.


Mheshimiwa Spika amesema  kuwa kwa sasa hakuna kanuni kuhusu jambo hilo, hivyo uamuzi wa Naibu Spika utabaki halali na utaingizwa kwenye kumbukumbu za bunge kwa ajili ya kutumika huko mbele kwa ajili ya maamuzi pale itakapotokea tukio kama hilo. 
Kwa uamuzi huo Wabunge hao watakosa vikao vya Bunge kwa siku tano kuanzia Alhamisi (jana), Ijumaa (leo) pamoja na siku tatu za juma lijalo za Jumatatu, Jumanne na Jumatano.

Mhemiwa Spika alilazimika kutoa ufafanuzi huo kufuatia ombi lililotolewa na Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni la kutaka kupata mwongozo juu ya uhalali wa kutolewa nje na kisha kufungiwa vikao vitano kwa wabunge sita (6) wa Chadema uliotolewa juzi na Naibu Spika.
Juzi, Ndugai aliwasimamisha wabunge Tundu Lissu (Singida Mashariki), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Ezekiah Wenje (Nyamagana) na Godbless Lema wa Arusha Mjini kwa siku tano.
Uamuzi wa Naibu Spika, Mheshimiwa Ndugai ulitolewa baada ya Mnadhimu wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Tundu Lissu kuendelea kudai mwongozo wakati mbunge mwingine akizungumza hatua iliyomfanya Lissu, kwa mujibu wa Ndugai, aonekane kuwa ameomba mwongozo mara nyingi hivyo kuwapotezea muda wabunge wengine.

Baada ya Tundu Lissu kuzidi kuomba mwongozo, Naibu Spika aliamuru askari wa bunge kumtoa nje jambo lililozua tafrani na kufanya wabunge wengine wa CHADEMA kuingilia kati na kupelekea adhabu kutolewa kwa wabunge walioshiriki katika mvutano huo.




TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top