SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete imetajwa kufanya vibaya katika
kuwaondolea umaskini wananchi kutokana na kuendekeza tabia ya
kuwakumbatia viongozi walioshindwa kiutendaji.
Hali hiyo inadaiwa kuwa inatokana na uteuzi wa wasaidizi wa rais
kufanyika kwa kuzingatia misingi ya urafiki na hivyo pale wanaposhindwa
kufanya kazi anapata wakati mgumu kuwawajibisha.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Waitara Mwikwabe wakati akihutubia
mikutano ya hadhara katika maeneo tofauti ya Mugumu mjini, Natta na
Misenyi wilayani Serengeti mkoani Mara.
Mwikwabe alisema kushamiri kwa umaskini miongoni mwa Watanzania
kunasababishwa na uongozi mbovu wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), ambao wameteuliwa kirafiki na kindugu badala ya kujali utendaji
wao.
Mwanasiasa huyo aliwataja baadhi ya viongozi aliodai wameteuliwa kwa
kufuata undugu na urafiki kuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia na Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
Kwa mujibu wa Mwikwabe, viongozi wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi
(IGP), Said Mwema na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Seleman Kova aliyedai ni rafiki mkubwa wa IGP Mwema.
“Watanzania mnapolia na umaskini, CHADEMA tunawashangaa sana. Tatizo la umaskini chanzo chake ni Rais Kikwete na CCM yake.
“Huyu mtu anafanya uteuzi wake kwa kuangalia undugu na urafiki badala
ya uwezo wa mtu kiutendaji. Sasa CHADEMA tumejiandaa vizuri sana
kuchukua nchi 2015,” alisema.
Aliwaomba wananchi kubadilika kifikra ikiwa ni pamoja na kuchukizwa na
uongozi mbovu wa Serikali ya CCM, kwani tangu nchi ipate uhuru miaka 51
iliyopita umaskini unazidi kuongezeka.
0 comments:
Post a Comment