Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni na
Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kufuatia taarifa za kifo cha
Msanii Mkongwe hapa nchini, Marehemu Fatma Binti Baraka Hamisi ambaye
alijulikana sana kwa jina la kisanii la Bi. Kidude aliyefariki dunia
tarehe 17 Aprili, 2013 akiwa nyumbani kwake katika eneo la Bububu,
Zanzibar kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya Kisukari kwa muda mrefu.
“Nimepokea
kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Msanii Mkongwe na Mwimbaji
Mashuhuri wa Nyimbo za Mwambao hapa nchini, Marehemu Fatma Binti Baraka
Hamisi maarufu kwa jina la Bi Kidude aliyefariki tarehe 17 Aprili, 2013
akiwa nyumbani kwake eneo la Bububu, Zanzibar kutokana na ugonjwa wa
Kisukari”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
Katika salamu hizo, Rais Kikwete amesema alimfahamu Bibi Fatma Binti
Baraka enzi za uhai wake kutokana na mchango wake mkubwa ndani na nje ya
nchi yetu katika nyanja za Sanaa na Utamaduni ambapo alimudu kuitangaza
vyema nchi yetu kupitia kipaji chake cha uimbaji kwenye matamasha
mbalimbali aliyowahi kuhudhuria na uimbaji wake kuwa kivutio kikubwa kwa
watu wengi waliowahi kuhudhuria matamasha hayo, kuyasikiliza kwenye
Radio na kuyatazama kupitia matangazo ya Televisheni.
“Kwa
hakika Fani ya Sanaa na Utamaduni imempoteza mtu muhimu ambaye mchango
wake ulikuwa bado unahitajika sana katika kuinua zaidi kiwango cha
uimbaji wa Muziki wa Mwambao ambao umejizolea sifa nyingi”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake na kuongeza,
“Kufuatia
taarifa hizo za kusikitisha, ninakutumia wewe Waziri wa Habari,
Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara Salamu zangu za
Rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa Wasanii nguli wa Muziki wa Mwambao
hapa nchini”.
“Vilevile
naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa
Wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu Bibi Fatma Baraka Hamisi kwa
kupotelewa na mhimili madhubuti wa familia. Namuomba Mwenyezi Mungu,
Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu.
Amina”, amesema Rais Kikwete.
Aidha Rais Kikwete
amewapa pole Wasanii wote hapa nchini ambao kwa hakika watakuwa
wameguswa sana na kifo cha Bibi Fatma Baraka ambaye alichangia vilivyo
katika kuitangaza sanaa kupitia uimbaji wa Muziki wa Mwambao. Amesema “kwa
wao, njia bora ya kumuenzi Bi. Kidude ni kuendeleza zaidi sanaa ya
uimbaji wa Muziki wa Mwambao na kuyaenzi yote mema na mazuri
aliyolifanyia Taifa letu.”
Rais Kikwete
amewahakikishia wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu Fatma Baraka
kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa.
Imetolewa na: Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu. Dar es Salaam. 17 Aprili, 2013
0 comments:
Post a Comment