MVUTANO mkali umeibuka bungeni baada ya serikali na baadhi ya
wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutaka hotuba ya Msemaji wa
Kambi ya Upinzani isisomwe.
Mawaziri na baadhi ya wabunge wa CCM walipinga hotuba hiyo isisomwe
kwa madai kuwa inagusa kesi ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa
CHADEMA, Wilfred Lwakatare, Dk. Steven Ulimboka na Absalom Kibanda
ambao walidai masuala yao yako mahakamani na masuala ya Usalama wa
Taifa.
Hali hiyo iliibua malumbano mazito ya kisheria na kusababisha Naibu
Spika, Job Ndugai, kuahirisha mjadala huo na kuagiza Kamati ya Kanuni
kukutana kwa dharura kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Katika mjadala huo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM)
alijikuta akipandwa jaziba na kutoa tusi ambalo gazeti hili haliwezi
kulichapisha.
Mbunge wa kwanza kuwasha moto huo alikuwa Serukamba ambaye aliomba
mwongozo wa spika kutaka kiti cha spika kizuie kujadili hotuba hiyo.
Serukamba alitoa mwongozo huo takriban dakika mbili kupita tangu
Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Profesa Kolikoyela Kahigi, kuanza kusoma
hotuba mbadala ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa
Umma kwa mwaka wa fedha 2013/ 2014.
“Mheshimiwa Spika, ukisoma taarifa ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani,
ukurasa wa pili hadi wa nne, kwanza tunaingilia uhuru wa mahakama. Ni
juzi tu Mheshimiwa Mustafa Akonay (CHADEMA), alitukumbusha juu ya jambo
hili.
Pili, tunataka kuleta jambo la mahakamani kulifanyia siasa ndani ya
Bunge, na tatu tutakuwa taifa na Bunge la ajabu sana duniani, tunataka
kujadili jambo ambalo liko mahakamani,” alisema Serukamba.
Kauli ya Serukamba ilimnyanyua Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
(CHADEMA) na kutoa taarifa bungeni kupinga mwongozo wa mbunge
aliyetangulia.
“Mheshimiwa Spika, msemaji aliyetangulia (Serukamba), amefanya rejea ya hotuba ya kambi ya upinzani hata kabla haijasomwa.
Taarifa ni kwamba katika kurasa alizozitaja hakuna jambo la
mahakamani. Kurasa hizo zinazungumzia kuhusu utekaji nyara wa Dk.
Uimboka, Kibanda, gazeti la MwanaHalisi kufungiwa na kazi za Usalama wa
Taifa. Hakuna jambo lililoko mahakamani hapo,” alisema Mnyika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge,
William Lukuvi, naye alisimama na kuomba mwongozo wa spika akitaka
hotuba ya kambi ya upinzani isisomwe.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunaweza kufanya sarakasi nyingi bila sababu
za msingi. Ukurasa wa tatu umetaja jina la Lwakatare. Alichosema
Serukamba ni utangulizi tu. Hii kesi ipo mahakamani na ni kuingilia
uhuru wa mahakama.
“Na hii ni kinyume cha sheria ya Usalama wa Taifa. Ni marufuku kutaja
hata majina ya watumishi wa Usalama wa Taifa, lakini hotuba ya wenzetu
inataja mambo ya Usalama wa Taifa.
“Mimi nashangaa mambo hayo hayo yanarudi tena bungeni kwa mlango wa
nyuma. Lengo langu ni kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa nne yanayohusu
masuala ya Usalama wa Taifa, Ulimboka na Lwakatare, tuyaache,” alisema
Lukuvi.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, naye alipata nafasi na kutoa ufafanuzi
kwamba kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa tatu hakuna mahala jina la
Lwakatare limetajwa, lakini katika ukurasa wa nne jina lake limetajwa
bila kuingilia mwenendo wa kesi.
Alisema ukurasa wa nne unaeleza jinsi alivyokamatwa, jambo ambalo haliingilii uhuru wa mahakama.
Mbunge huyo ambaye ni mwanasheria, kuhusu sheria ya Usalama wa Taifa,
alimtaka Waziri Lukuvi alete sheria ya Usalama wa Taifa ili
ilinganishwe na hiyo inayotajwa bungeni.
Naye Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alipingana na maelezo
ya Waziri Lukuvi na wabunge waliotaka hotuba hiyo izuiliwe.
“Mheshimiwa Spika, kabla sijasema, niseme ninayo sheria hapa ya Idara
ya Usalama ya mwaka 1996. Maneno kwamba masuala ya Usalama wa Taifa
hayazungumziki bungeni ni maneno ya mitaani.
Kinachokatazwa kwenye magazeti, mikutano na mahala pengine ni kutaja majina ya watumishi wa Usalama wa Taifa.
“Idara ya Usalama wa Taifa inaongozwa na mkurugenzi ambaye anapewa
maelekezo na waziri. Kama wanafanya vibaya huko nje, anayewajibishwa ni
waziri na namna ya kumwajibisha ni kuruhusu msemaji wa upinzani
aendelee,” alisema.
Alisema ni jambo la hatari kumzuia msemaji kuzungunzia idara ya serikali inayotumia fedha za serikali.
”Hakuna mahala popote kesi ya Lwakatare, Idara ya Usalama wa Taifa
imetajwa kwa namna ambayo ina influence uamuzi wa mahakama,” alisema
Lissu.
Alisema kama hakuna mahala popote hotuba ya upinzani imetaja kesi ya
mahakamani, litakuwa jambo baya sana kuiziba mdomo kambi ya upinzani.
Naibu Spika alimpa nafasi tena Serukamba ili kujibu hoja za wabunge
waliopinga ambapo badala ya kuzungumza alijikuta akitoa tusi ambalo
haliwezi kuandikika.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), naye alisema
hotuba hiyo izuiliwe kwa madai kuwa inaingilia uhuru wa mahakama.
Akitoa mwongozo wake, Naibu Spika aliiagiza Kamati ya Kanuni kukutana
mara moja na kuja na majibu ambayo yatasaidia mjadala huo kuendelea
jioni.
Baadaye jioni hotuba hiyo ilisomwa baada ya pande hizo kukubaliana kuwa kurasa zilizokuwa na matatizo ziondolewe.
Hata hivyo, mjadala wa jumla ulipoanza kwa wabunge wote, Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema, aliibua mtafaruku mkubwa pale alipodai
kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye kinara wa mgogoro wa udini nchini.
Kauli ya Lema iliwafanya baadhi ya wabunge wa CCM na mawaziri William
Lukuvi, Stephen Wassira na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick
Werema, kuinuka na kuomba mwongozo wa spika wakimtaka mbunge huyo afute
kauli yake.
Lukuvi alijenga hoja akisema kwa mujibu wa kanuni ni marufuku jina la
rais kutajwa kwa msamaha, hoja ambayo hata hivyo Lissu aliipinga
akidai kanuni inatumika kimakosa kwani haikatai kiongozi huyo
kukosolewa.
Hata hivyo Lema alipopewa nafasi ya kufuta kauli yake ama
kuithibitisha, alirejea maneno yake kuwa Rais Kikwete ndiye kinara wa
udini nchini akishirikiana na mawaziri kama Wassira na Lukuvi.
Kabla ya kubanwa, Lema alitumia muda wake kuwashambulia Usalama wa
Taifa kwa kutajwa kuhusika katika matukio kadhaa ya kuteka na kutesa
raia.
Alisema yuko tayari kung’olewa kucha au meno, lakini hataogopa kusema ukweli.
Akizungumzia zaidi suala la dini, Lema alisema taifa limefika mahala
pabaya na kama hali itaachiwa, kuna hatari ya kutokea vurugu za kidini.
Aliilaumu tena serikali kwa kuachia hali hiyo kwani imeshindwa
kuchukua maamuzi magumu kwa wakati kutokana na hofu na woga usio na
sababu.
”Sasa hivi rais akifanya uteuzi, baada ya nusu saa watu wanaanza
kujadili nani Mkristo, nani Mwislamu. Hii ni hatari,” alisema Lema.
0 comments:
Post a Comment