Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Mwigulu Nchemba
SIKU moja baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Mwigulu Nchemba, kukiri kuhusika na video inayomuonesha
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, maswali
mengi yameibuka juu ya kada huo.
Baadhi ya wananchi wamelidokeza Tanzania Daima Jumatano kuwa kwa
kukiri huko, Mwigulu alitakiwa kukamatwa na Jeshi la Polisi na
kufunguliwa mashtaka kutokana na nyendo zake kuonesha kwamba anahusika
na mchezo huo.
Mwigulu alikiri kuwa ndiye aliyeipeleka video ya Lwakatare polisi na
kwamba alifanya hivyo baada ya kuripoti kuandikiwa ujumbe wa simu wa
kutishiwa maisha na baadhi ya viongozi wa CHADEMA.
Hata hivyo wananchi hao wameibua maswali magumu wakihoji alikoipata
video hiyo inayoashiria vitendo vya uchochezi na kwamba iweje msamaria
mwema aipeleke kwake badala ya vyombo vya dola.
“Kwanza, Mwigulu ametusaidia kutambua mchezo mzima, kwani tutapaswa
kuelezwa yeye ni nani hadi msamaria mwema atoke CHADEMA, ampelekee
video inayopanga mauaji badala ya kuipeleka polisi?” alihoji
mwanasheria mmoja aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.
Mkanganyiko zaidi ulizidi kutawala baada ya Mwigulu kuandika ujumbe
kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forum jana, akidai hausiki kurekodi
mkanda wa video ya Lwakatare.
Katika ujumbe wake huo, Mwigulu aliandika: “Ndg wana JF sijashiriki
kurekodi mkanda wa video unaomwonesha kiongozi mwandamizi wa CHADEMA
akipanga mauaji ya mhariri wa gazeti.
“Mambo yako dhahiri, kwani video inaonesha pale ni nyumbani kwake.
Pili, sikumtuma mtu akarekodi mkanda huo. Niliwahi kusema nina mkanda,
haina maana kuwa nilituma mtu,” alisema.
Mwigulu aliongeza kuwa: “Mikanda niliyokuwa nayo nilipewa na kiongozi wa CHADEMA anayechukizwa na vitendo hivyo vya kinyama.
“Ndugu zangu wa CHADEMA, najua nawakera na hampendi kusikia haya,
nawashauri msihangaikie habari ya Mwigulu ameshiriki, bali hangaikieni
kwanini kiongozi mwandamizi anafanya hayo, pia kwanini anafanya kizembe
mpaka mkanda unanaswa na tatu mjiulize,” alindika.
Ujumbe huo ulizidi kusomeka kuwa: “Kwangu mimi sioni kama kupata
mkanda huo kwa kupewa au kwa hela ni dhambi kubwa kuliko ya kupanga
mauaji. Niwambie tu mkanda niliopewa sikuweka hata nukta na nilikabidhi
vyombo vya usalama,” alihitimisha.
Kufuatia ujumbe huo, wachangiaji mbalimbali waliujadili kwa njia ya
mtandao huku wengine wakipiga simu katika chumba cha habari cha gazeti
hili wakitaka Jeshi la Polisi litoe ufafanuzi ni kwanini limekaa kimya
bila kumkamata na kumshtaki Mwigulu.
Mchangiaji mmoja katika mtandao huo, alisema: “Huo mkanda uliukabidhi
lini kwa polisi? Mbona wao polisi wamefanyia kazi ule uliorushwa Jamii
forums?
“Na je, kwanini utoke kipindi ambacho amefanyiwa ukatiri Mwenyekiti
wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda miezi kadhaa mbele? Waweza
kuni-convince (shawishi) kwamba si watu wa usalama wamefanya kitendo
kile ili iendane vizuri na suala la Lwakatare?” alihoji.
Aliongeza kuwa: “Mwigulu kumbukeni huwezi ukafanya uchawi gizani
miaka yote usigundulike, ipo siku Watanzania wataelewa ni fitna gani
CCM mnazifanya.
“Suala la wauaji wa Kolimba (Horace) kuua, kwenda jela na baadaye
kutolewa kinyemela lilitufunua fikra kidogo kuhusu Usalama wa Taifa na
CCM, hili suala lilipita na likavumiliwa na Watanzania,” alisema
mchangiaji huyo kwenye mtandao.
Kwamba hata suala la Dk. Stephen Ulimboka kupigiwa simu na mtu
anayemfahamu, kuhojiwa na mtu huyo huyo baadaye kutekwa na kufanyiwa
ukatili akiwa katika mazungumzo na mtu yule yule anayedaiwa kuwa
alitumwa kutoka Ikulu bila kumkamata linatia shaka.
“Mtu aliyekuwa naye dakika za mwisho kwa maongezi alipaswa kukamatwa
ili aisaidie polisi hata baada ya kutolewa mtiririko wa mawasiliano ya
hawa watu wawili na gazeti la MwanaHalisi, hili suala pia lilitufunua
mtazamo na fikra kuhusu CCM na Usalama wa Taifa.
“Na sasa hili suala la Lwakatare pia linatupa picha halisi ya CCM na
Usalama wa Taifa, ila siwezi kubashiri kama litavumiliwa na kusahauliwa
pia. Sifa ya kwamba Tanzania ni nchi ya amani inatolewa na watu
wasiojua tafsiri halisi ya amani,” alisema.
Mchnagiaji mwingine katika mtandao huo alijadili utetezi wa Mwigulu
akisema: “Huoni unajichanganya…imekuwaje unakuwa na mawasiliano na
Ludovick (Joseph) na wakati huo huo unamtumia hela kwa M-pesa?
“Hii inaonyesha kuna kitu kimejificha, vyombo vya dola vimekaa na
hiyo video miezi mitatu…ndipo mtuhumiwa akamatwe, huoni kuna walakini?
“Najua vyombo vya dola vilitaka kumteka Mhariri wa Mwananchi ila
bahati mbaya watekaji wakaenda kwa Kibanda na video ikatolewa muda huo
huo...huoni kwamba polisi inatakiwa kuhojiwa kwa kukaa na video miezi
mitatu?” alihoji.
Mwingine aliandika akisema: “Unaweweseka we...wewe ni shahidi katika
kesi hii...na ni engineer number moja wa mpango mzima...utaenda kujibu
mahakamani.
“Kuja humu JF kujitetea ni kutafuta sympathy (huruma) toka kwa
wafuasi wako....You have a big case to answer in the court of
law.....get prepared...we mbunge gani unafanya ujasusi?” alihoji.
Aliongeza kuwa: “Unaacha kuwatumikia watu wako wanaokula majani
jimboni mwako...unashiriki jinai. We kiongozi gani...maneno na matendo
yako yanaonekana kwa Watanzania,” alisisitiza mchangiaji huyo.
Hata wachangiaji waliopiga simu walijikita kuhoji sababu za video
kupelekwa kwa Mwigulu na kiongozi wa CHADEMA badala ya vyombo husika
ili vichukue hatua.
Wapo waliohoji ni kwanini Mwigulu alitangaza kuwa na video ya mauaji
kwenye vyombo vya habari wakati alikwisha wakabidhi polisi na
wanaendelea na uchunguzi.
“Hapa kuna maswali mengi yanahitaji majibu na kama Jeshi la Polisi
litafumba macho kuruhusu upuuzi huu wa siasa za kijinga kama hizi
tutalipeleka taifa pabaya kwa michezo hii ya kina Mwigulu.
“Kitendo cha kutangaza kwenye vyombo vya habari wakati akijua polisi
inaendelea na uchunguzi, kwanza angeweza kupoteza ushahidi, angeweza
kudhuriwa lakini kwa muda wote zaidi ya miezi mitatu tangu akabidhi
video hiyo mbona hakuna mauji yaliyotokea,” alisema Bakari Athuman
mkazi wa Iringa.
Naye mwanaharakati aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, alishangaa kuona
polisi waliibuka kuifanyia kazi video hiyo baada ya Kibanda kuteswa,
akihoji walikuwa wakingoja nini.
“Nadhani ukweli umeanza kujionesha kuwa huu ni mkakati wa kuichafua
CHADEMA, maana Mwigulu anasema aliwapa video polisi, baada ya miezi
mitatu wakawa kimya, kisha ikawekwa kwenye mtandaoo wa kijamii ndipo
Lwakatare akakamatwa na kushtakiwa.
“Sasa tunajiuliza, ni nani aliweka video hiyo You tube kati ya
Mwigulu na Jeshi la polisi? Je, kwani Mwigulu afahamu hata mahojiano
baina ya polisi na Lwakatare? Kuna jambo limejificha, aibu yao
inakuja,” alisema.
Katika mohojiano na gazeti hili kwa simu juzi, Mwigulu alikiri kuwa
ndiye aliyeipeleka video ya Lwakatare polisi na kwamba alifanya hivyo
baada ya kuripoti kuandikiwa ujumbe wa simu wa kutishiwa maisha na
baadhi ya viongozi wa CHADEMA.
“Niliwapelekea mimi hiyo video polisi na wakati nasema kwenye
televisheni nilikuwa tayari nimewapa. Na pale nilisema makusudi baada
ya Zitto Kabwe kudai kuwa mwaka jana kulitokea mauaji mengi, ndipo
nikataka kumuonesha kuwa chama chake kinahusika na mikakati hiyo,”
alisema.
Alipoulizwa aliipataje video hiyo na kwanini hajahojiwa polisi ili
kutoa uthibitisho wa uhalali wake, Mwigulu alisema: “Kuna msamaria
mwema aliniletea.”
Mwigulu alipobanwa ana uhakika gani kama video hiyo ina ukweli,
alijibu kuwa: “Ile huhitaji akili kubwa kutambua uhalisia wake. Suala
la Lwakatare CHADEMA wakubali tu na wajitokeze hadharani kwenye
makanisa na misikiti, watubu na kuomba radhi kwa umma.”
Hata hivyo katika kile kinachoweza kuongeza mashaka ya Mwigulu
kuhusishwa kutengeneza video hiyo, alikwenda mbali zaidi akitoa hata
siri za polisi, akisimulia maelezo aliyodai kuwa ndiyo yalitolewa na
Lwakatare wakati akihojiwa na polisi.
“Pale video inaonesha ni nyumbani kwake, tena jikoni na hilo amekiri
katika maelezo yake polisi. Pia amekubali kuwa siku hiyo alipiga chafya
kama inavyoonekana. Sasa wewe mwandishi unatetea nini wakati yeye
amekiri polisi kila kitu kilichomo mle,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment