Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani, Freeman Mbowe
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeibana serikali
kikitaka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walionaswa wakifanya
mawasiliano na watuhumiwa wa ugaidi wa kubambikizwa waunganishwe kwenye
kesi hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani, Freeman Mbowe, wakati akiwasilisha hotuba mbadala ya makadirio
ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2013/2014 katika Ofisi ya
Waziri Mkuu.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA taifa na Mbunge wa Hai,
alisema vitendo vya viongozi wa dini kujeruhiwa na kuuawa kwa kupigwa
risasi, kuchoma moto nyumba za ibada huko Zanzibar na Dar es Salaam ni
ugaidi kwa mujibu wa tafsiri ya Sheria ya Ugaidi ya Tanzania.
“Kambi Rasmi ya Upinzani inashangazwa sana kuona kwamba serikali
haikuyachukulia matukio haya ya wazi ya kigaidi kama ni ugaidi ila
imekuwa hodari sana kuchukua suala la mtu aliyebambikiwa kesi ya ugaidi
kwa ushahidi wa kughushi kuwa yeye ndiye gaidi.
“Pili, kwa mujibu wa Sheria ya Ugaidi, mtu yeyote anayefanya
mawasiliano na gaidi au magaidi, yeye pia anahamasisha ugaidi, hivyo
naye anastahili kuunganishwa katika tuhuma hizo za mashtaka ya ugaidi,”
alisema Mbowe.
Ingawa Mbowe hakutaja jina la mtu, lakini ni dhahiri alikuwa
akimzungumzia Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Willfred
Lwakatare na kijana Ludovick Joseph, ambao wamefunguliwa mashtaka ya
ugaidi kwa madai ya kupanga njama za kutaka kumdhuru Mhariri wa gazeti
la Mwananchi, Dennis Msacky.
Kufunguliwa kwa kesi hiyo kumeibua mjadala mkali miongoni mwa wananchi
wakihoji ni kwanini Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, ambaye
amekiri kuwa na video hiyo inayoonesha mipango ya kigaidi hakushtakiwa.
Mwigulu pia amedaiwa kuwa na mawasiliano ya karibu na Ludovick kabla
na baada ya video hiyo kurekodiwa ikiwa ni pamoja na kumtumia fedha kwa
njia ya M-pesa kupitia namba yake ya simu.
Hivyo kauli ya Mbowe ni kama alimlenga Nchemba ambaye anadaiwa kufanya
mawasiliano na watuhumiwa hao wa ugaidi na bado yupo nje wala
hajahojiwa na polisi.
Alisema kuwa hivi sasa taifa linashuhudia kuibuka kwa uchochezi mpya
wa kisiasa tena wenye ubia kati ya CCM na vyombo vya dola na kinachoitwa
‘ugaidi’.
“Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitika sana
kuona wale wote waliokuwa wakiwasiliana na hao wanaoitwa magaidi, ambao
pia ni viongozi wa CCM na washirika wao hawajachukuliwa hatua yoyote,”
alisema.
Aliongeza kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaulaani mkakati huu wenye nia ovu ya kufifisha demokrasia hapa nchini.
Mbowe alifafanua kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kwamba, kamwe
mpango huu haramu hautafanikiwa na alitumia nafasi hiyo kuonya kuwa
vyama vya siasa vifanye siasa zake kwa ushindani wa sera na isiwe kwa
mikakati ya kiharamia ya kudhuru, kubambikiza na kisha kutengeneza
ushahidi kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama.
“Hili nalo likiachiwa likakomaa litaliingiza taifa letu katika hatari nyingine ya machafuko,” alisisitiza.
Akieleza chanzo cha chuki hiyo, Mbowe alisema ilipaliliwa kisiasa na
sasa ndiyo inayoitesa nchi na kwamba linastahili kuwa somo kwa
wanasiasa wote walioasisi uhalifu huu dhidi ya mustakabali mwema wa
taifa.
“Mheshimiwa Spika, uchochezi na propaganda za kidini na kikabila
vilichagizwa kasi na CCM mara baada ya kuanza mfumo wa vyama vingi vya
siasa kama mojawapo ya turufu yake ya kukabiliana na vyama vya upinzani.
“Uchochezi huu ulishika kasi katika uchaguzi wa mwaka 2005 na mwaka
2010. Vikundi kadhaa vya kidini vilifadhiliwa kuhubiri chuki dhidi ya
dini nyingine waziwazi na kwa muda mrefu katika maeneo kadhaa ya nchi,”
alisema.
Mbowe alifafanua kuwa mihadhara, mahubiri na hata matamko ya hatari na
uchochezi yalitolewa waziwazi hata kupitia vyombo kadhaa vya habari vya
kidini na mitandao ya kijamii.
“Malalamiko mengi yalitolewa lakini serikali ilifumbia macho tatizo
hili, kwani ilionekana kuwa mpasuko na hofu iliyo matokeo ya propaganda
hizo ulikinufaisha zaidi chama tawala na baadhi ya viongozi wake,”
alisema.
Mabadiliko ya Katiba
Kuhusu mabadiliko ya Katiba, Mbowe aliweka msimamo wa chama chake
kuwa kitajitoa kushiriki katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo
yafuatayo hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia mwisho wa mwezi huu.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kufutwa kwa uteuzi/ uchaguzi wa
wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za
Maendeleo za Kata, na badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba ya
wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa kata husika bila
kuchujwa na WDC.
Kwa mujibu wa Mbowe, aliitaka serikali ilete mbele ya Bunge Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yatakayofanyika
maeneo yafuatayo.
Moja, ni vifungu vyote vinavyohusu uwakilishi katika Bunge Maalumu la
Katiba na taasisi zilizoainishwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Pili, alisema ni vifungu vyote vinavyohusu ushirikishi wa wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba kutoka Zanzibar katika mijadala inayohusu mambo
yasiyokuwa ya muungano ya Tanzania Bara.
Tatu, pia alitaja vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya rais kuitisha
tena Bunge Maalumu la Katiba baada ya Bunge hilo kuwa limeshapitisha
Rasimu ya Katiba Mpya kwa lengo la kufanya marekebisho katika rasimu
kabla haijapelekwa kwenye kura ya maoni.
Nnne, ni vifungu vyote vinavyohusu mamlaka ya kikatiba na ya kisheria
yatakayoiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendesha na kusimamia kura
ya maoni.
Mbowe alisema kuwa kwa mujibu wa Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji
Joseph Warioba, hadi awamu nne za kukusanya maoni ya wananchi
zinakamilika Desemba 19 mwaka jana, tume ilikwisha kufanya mikutano
1,776 nchi nzima.
Kwamba kufikia kipindi hicho wananchi wapatao 64,737 walikwishatoa
maoni yao kwa kuzungumza wakati 253,486 walitoa maoni kwa njia ya
maandishi, na wengine 16,261 walitumia njia ya posta, tovuti ya tume,
mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu za mkononi.
“Kwa hiyo, kwa mujibu wa taarifa hizi za tume, kati ya Watanzania
takriban milioni 45, ni Watanzania 334,484 ndio waliotoa maoni juu ya
Katiba Mpya hadi kufikia Januari 4, mwaka huu. Idadi hii ni sawa
na asilimia 0.7 ya Watanzania wote.
“Na hao ndio waliotoa maoni yao kwa muda wa dakika tano kila mmoja,
wakiwamo waheshimiwa wabunge wa Bunge hili tukufu. Mheshimiwa Spika, ni
wazi kwa takwimu hizi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa vyovyote
vile, Katiba Mpya itakayotokana na maoni haya haiwezi kuwa Katiba Mpya
ya Watanzania wote,” alisema.
Mbowe alisema kuwa utaratibu wa hovyo namna hiyo utazaa Katiba Mpya ya
hovyo, kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini utaratibu huu wa
hovyo hauwezi kutupatia Katiba Mpya yenye maridhiano ya kitaifa kwa
ajili ya kutatua migogoro mingi ya kisiasa, kijamii na kidini ambayo
inaikabili nchi yetu kwa sasa.
Alisema CHADEMA haiwezi kuendelea kushiriki na kubariki mchakato huu
kama ulivyo sasa kwani ishara zote ziko wazi kuwa Katiba inayokusudiwa
ni ile tu itakayokidhi matakwa ya Wana CCM na washirika wake, hivyo
kutokutimiza azima ya kuwa na Katiba itakayoponya majeraha mbalimbali na
kurejesha uzalendo, mshikamano na upendo wa dhati miongoni mwa
Watanzania.
Hatima ya waliofeli
Kuhusu waliofeli elimu ya msingi na sekondari, Mbowe alisema vijana hao kwa sasa ni wastani wa watoto 800,000.
Alisema wengi wao wanatoka familia maskini, hawana uwezo wa
kujiendeleza na hawana sifa za kuajiriwa ikiwa ni pamoja na umri mdogo.
Mbowe aliongeza kuwa kwa kipindi cha miaka 51 ya Uhuru, serikali
haijatengeneza sera yoyote au sheria ya kusaidia kundi hili kubwa ili
liweze kushiriki katika shughuli za kiuchumi ili liweze kujikimu na
kuchangia katika pato la taifa.
“Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kueleza
mbele ya Bunge hili kwamba ina mpango gani wa kupunguza idadi hii ya
watoto wanaobaki mitaani bila shughuli rasmi ya kufanya,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment