Freeman Mbowe
Wilbrod Slaa
VITA ya kisiasa ya kuwania kushika hatamu za uongozi wa dola mwaka 2015, inayopiganwa na vyama vya siasa vyenye nguvu ya ushawishi kwa wananchi hapa nchini, sasa imeanza kuliyumbisha taifa.

Mwenendo wa vita hiyo ambao umekuwa ukishika kasi kadiri uchaguzi mkuu ujao unavyokaribia, umesababisha athari mbaya kwa wananchi na hata kuhatarisha hali ya amani, utulivu na mshikamano ambayo Watanzania wamedumu nayo kwa muda mrefu.
Mwingulu Nchemba
Wafuatiliaji wa masuala ya siasa za hapa nyumbani waliozungumza na Mtanzania Jumapili, wameeleza kuwa chanzo cha kuibuka kwa udini, ukabila na watu kutekwa, msingi wake ni vita vya wanasiasa vya kuwania uongozi wa dola.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ndivyo vinavyotajwa sasa kupalilia udini, ukabila na hata vitendo vya uvunjifu wa amani ili kukidhi matakwa ya kisiasa ya vyama hivyo ambayo ni kushika madaraka.

Kwa mujibu wa tathimini ya wafuatiliaji hao wa mwenendo wa siasa za hapa nyumbani, waliohojiwa na gazeti hili kwa nyakati tofauti, imeonyesha kuwa kusambaa kwa udini na ukabila kumechochewa na matamshi na vitendo vya wanasiasa wanaopambana kupata uungwaji mkono wa wananchi katika sanduku la kura.

CCM ndicho kinachotajwa kuasisi siasa za udini nchini kwa lengo la kuvidhoofisha vyama vya upinzani vinavyoonekana kutishia uwepo wake madarakani.

Mfano unaotolewa na wachambuzi hawa kuhalalisha hoja yao hii ni hatua ya makada ya CCM kumuhusisha aliyekuwa mgombea urais wa Chadema katika uchaguzi mkuu wa 2010, Dk. Willbrod Slaa, na imani yake ya dini ya Kikristu.

Sambamba na hilo, CCM pia kinatajwa kutumia udini kama moja ya silaha zake za kushinda uchaguzi mkuu wa 2010, baada ya ilani yake ya uchaguzi kubeba ahadi zilizokuwa na mwelekeo wa upendeleo wa kidini kwa waumini wa dini ya Kiislamu jambo ambalo sasa linaigharimu Serikali yake, baada ya kushindwa kutekeleza ahadi hizo.

Aidha, mlolongo wa matukio ya kisiasa ambayo yamekuwa yakifanyika katika nyumba za Ibada na katika mikusanyiko ya kidini ambayo wanasiasa wamekuwa wakiitumia kujipigia debe wao binafsi na hata vyama vyao, nayo ni mambo yanayozidi kuchochea mbegu za udini hapa nchini.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kumbukumbu zilizopo, zinaonyesha kuwa CCM kilikuwa cha kwanza kueneza sumu ya udini hapa nchini, baada ya kukituhumu Chama cha Wananchi (CUF) kuendesha siasa za kidini katika maeneo ya Ibada hususan yale yanayotumiwa kuabudu na waumini wa dini ya Kiislamu.

Sumu hii ya CCM dhidi ya upinzani ilipata nguvu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na ule wa 2005, baada ya CUF kuelekeza nguvu kubwa ya kutafuta uungwaji mkono misikitini, jambo ambalo lilipata kuingiliwa kati na vyombo vya dola ambavyo kwa nyakati tofauti viliwahi kuvamia baadhi ya misikiti, kwa madai ya kusaka silaha zilizodaiwa kuwa za wanachama wa CUF wenye msimamo mkali ambao walitaka kuhatarisha amani wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Katika mwenendo huo huo wa kutafuta nguvu za kisiasa kutoka kwa wananchi, hivi sasa CCM na Chadema vimeingia katika vita mpya yenye mwelekeo wa kutisha zaidi inayowahusisha makada wake na vitendo vya kigaidi.

Kuibuka kwa vita hii kumeligawa taifa, ambapo kundi la wafuasi na mashabiki wa Chadema wanaamini kuwa vitendo vya kigaidi vya utekaji na utesaji kinyama raia, vinaratibiwa na kutekelezwa na makachero chini ya usimamizi wa Serikali ya CCM.

Kwa upande wa mashabiki na wanachama wa CCM, sasa wanaamini kuwa kukamatwa kwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, akihusishwa na tuhuma za ugaidi kunadhihirisha madai ya muda mrefu yanayokihusisha chama hicho na vitendo vya uvunjifu wa amani.

Vita ya maneno ya viongozi wa vyama hivi viwili ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikifukuta chini kwa chini katika siasa za majukwaani kabla ya hivi karibuni kuibuka kwa nguvu bungeni, nayo imezidisha hali ya mpasuko na kutokuaminiana kwa wananchi wanaoviunga mkono, kila upande ukiutazama mwingine kwa jicho la mashaka.

Wakati huo huo, ikiwa ni siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kueleza jinsi anavyosononeshwa na mpasuko wa kidini nchini, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, jana ameibuka na kumtuhumu kuwa ndiye muasisi wa tatizo hilo.

Mbowe ametoa tuhuma hizo wakati akihutubia mkutano wa ufunguzi wa Kanda ya Pwani ya Chadema kwa kueleza kuwa vipo vikundi vya kidini vilivyokuwa vikipewa fedha na Ikulu, kwa ajili ya kuendesha migogoro ya kidini hapa nchini.

Alieleza kushangazwa na hatua ya Rais Kikwete kuanza kulalamikia udini sasa, huku akijua kuwa alishiriki kwa karibu kufadhili vikundi hivyo.

“Taarifa tunazo na tunawafahamu watu waliokuwa mstari wa mbele kufadhili vikundi vya kidini, leo hii iweje waanze kujikosha na wakati walikaribisha watu Ikulu, wakawahonga fedha ili waendeshe migogoro ya kidini nchini?

“Nawaambieni huu ni utawala mufilisi, una upungufu mwingi, ni hatari kwa maisha ya Watanzania. Suala la udini leo linawatafuna wanaanza kujikanyaga hovyo, wakati walilifadhili kwa nguvu zao zote,” alisema Mbowe.

Aliwataka wanachama wa Chadema kupuuza Propaganda za ugaidi kinazoelekezewa chama hicho na kuwataka wanachama kuwa makini na uzushi mwingi wenye lengo la kukichafua.

Aliishambulia Idara ya Usalama wa Taifa kwa kuendesha mpango wa kuwanunua maofisa wa chama hicho, ili wakipake matope kwa Watanzania.

“Msiwaogope Usalama wa Taifa, wepesi sana …tena weupe kweli kweli, wala wasiwatishe, hatutatetereka, tunasonga mbele. Nimepata fursa ya kumtembelea Mkurugenzi wa Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, ambaye yupo mahabusu kwa tuhuma za kuandaa mipango ya kufanya matukio ya kigaidi, nilimpongeza kwa jitihada za kuendelea kutoa elimu ya umma huko gerezani,” alisema Mbowe.

Akizungumzia mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya, alisema Chadema kinakusudia kumuondoa muwakilishi wake kwenye Tume ya Katiba kwa sababu ya ukiritimba unaofanywa na viongozi wa tume hiyo.

Alisema iwapo Serikali haitafanya marekebisho ya sheria hadi ifikapo Aprili 30, Chadema kitamuondoa mwakilishi wake aliyemtaja kuwa ni Profesa Mwesiga Baregu kwa kuzuiwa kufanya mawasiliano na chama chake kuhusu muundo wa Katiba mpya.

Naye, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, akizungumza katika mkutano huo, alisema tuhuma za ugaidi kinazoelekezewa chama hicho kinawapa hasira ya kufanya kazi zaidi ili kuchukua dola mwaka 2015.

Kama Mbowe, naye alisema Chadema kinajua mipango inayofanywa na Idara ya Usalama wa Taifa, kuwahonga fedha baadhi ya maofisa wa chama hicho ili wakichafue kwa tuhuma za Ugaidi.

Wakati viongozi wakuu wa Chadema wakieleza hayo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Bara, Mwigulu Nchemba amesisitiza kauli yake ambayo amekuwa akiitoa kila mara kuwa Chadema ndiyo waasisi wa udini nchini na kumtaja Dk. Wilbrod Slaa kuwa kinara wa migogoro ya udini nchini.

Nchemba alisema, wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Dk. Slaa alifanya kampeni za udini kwa kueneza chuki dhidi ya dini nyingine kwa kuwatumia wachungaji.

Akizungumzia tuhuma za ugaidi ambazo amekuwa akitajwa kuziibua, alisema Chadema hakiwezi kukwepa tuhuma hizo kwa sababu taarifa za mipango ya makada wake kuhusika nazo zinatolewa na wanachama wake wanaoitakia mema Tanzania.
Chanzo: Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top