SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Nchini (TANESCO) limekana kuwepo mgawo
wa umeme kwa sasa huku likikiri kuwa hali ya upatikanaji wa nishati
hiyo iko katika dharura na haijarejea katika hali ya kawaida kama
inavyotakiwa.
Ufafanuzi huu unakuja baada ya gazeti hili kuripoti hali tete ya
kifedha inayolikabili shirika hili na hivyo kutishia taifa kuingia
gizani wakati wowote.
Hata hivyo TANESCO na serikali kupitia kwa Wizara ya Nishati na Madini
wamekuwa kimya kwa muda pasipo kuzungumzia mgawo wa umeme ambao
umekuwepo kwa wiki takriban mbili katika maeneo mengi nchini.
Akizungumza jana makao makuu ya shirika hilo Ubungo, jijini Dar es
Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Felchesmi Mramba, alisema kuwa hakuna
mgawo wa umeme kwa sasa na kwamba ikitokea serikali ingetangaza.
Pamoja na kukanusha kuwepo kwa mgawo, Mramba alisema ukweli ni kwamba
bado nchi iko katika hali ya dharura na hali ya umeme haijarejea katika
hali yake ya kawaida kiasi cha kuondoka katika hali ya dharura.
“Ushahidi wa kwamba bado tuko katika hali ya dharura ni kwamba bado
mitambo ya dharura tuliyokodi kupambana na hali ya umeme inaendelea
kuhitajika lakini pia mabwawa hayana maji ya kutosha kukidhi mahitaji ya
umeme bila kuhitaji mitambo ya matufa,” alisema.
Aliongeza kuwa vilevile miundombinu ya gesi haiwapi gesi ya kutosha kuwasha mitambo yote ya gesi ya megawati 501.
Mramba alibainisha kuwa tangu Julai mwaka 2012 hadi Februari 2013,
serikali imetumia jumla ya sh bilioni 231.2 kama ruzuku kwa TANESCO kwa
ajili ya kununua mafuta ya mitambo.
“TANESCO kutoka kwenye mapato yake imetumia jumla ya sh bilioni 423.3
katika kipindi hicho kununulia mafuta, hivyo fedha yote iliyotumika
kununulia mafuta ndani ya kipindi hicho ni sh bilioni 654.5,” alisema.
Mramba aliongeza kuwa mitambo ya dharura inahitaji fedha nyingi
kuiendesha kulinganisha na bei halisi ya kuuza umeme huo. Akitolea mfano
alisema kuwa ili kuzalisha zinahitajika megawati 365 kwa mafuta
(Dizeli-lita 1,368,00, HFO-LITA 500,000 na Jet A1-Lita 518,000 kwa siku.
Alisema kuwa jumla ya sh bilioni 5.4 zinahitajika kila siku au sawa na
sh bilioni 162 kwa mwezi na kwamba mapato yanayotokana na kuuza
asilimia 100 ya umeme wote unaozalishwa ni sh bilioni kwa siku sawa na
takriban sh bilioni 70.2 kwa mwezi baada ya kuondoa kodi na tozo
mbalimbali.
“Hata kama TANESCO ingeamua isilipe mishahara wala isifanye
matengenezo ya mitambo, isinunue vifaa vya kuunganishia wateja, au
isiingie gharama nyingine zozote, bado ingepata hasara ya karibu sh
bilioni 90 kila mwezi,” alisema.
Mramba aliongeza kuwa kwa sababu kuna matumizi mengine muhimu ya
kiuendeshaji, TANESCO inajikuta ikipata hasara kubwa zaidi kwa mwezi.
Kuhusu deni la Songas, mkurugenzi huyo alikiri kuwa ni kweli kampuni
hiyo inaidai TANESCO na akasisitiza kuwa mkataba kati ya Songas na
TANESCO unaruhusu hali hiyo.
Hata hivyo, kauli hiyo inatofautiana na kauli ya Naibu Waziri wa
Nishari na Madini, George Simbachawene, aliyesema jana asubuhi kuwa
wanaoshinikiza kuwa kuna deni kati ya Songas na TANESCO ni madalali tu.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment