Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova .
MAOFISA watano wa polisi wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na
upotevu wa Sh milioni 150 zilizoporwa katika eneo la Kariakoo, jijini
Dar es Salaam, wamepandishwa kizimbani.
Maofisa hao waliopambana na majambazi katika eneo hilo na kutuhumiwa kuiba mamilioni ya hizo fedha jana walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Polisi hao walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauro na kusomewa mashitaka yanayowakabili na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Benard Kongola.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Sajenti Dancan Mwasabila (43) mkazi wa Kiwalani, Koplo Geofrey (39) mkazi wa Mbezi Luis, Koplo Rajabu Juma Nkurukwa (46) mkazi wa Buguruni, Koplo Kawanani Humphrey (34) na Koplo Kelvin Mohamed (44) mkazi wa Gongo la Mboto.
“Mheshimiwa, washitakiwa kama nilivyowataja wanadaiwa kwamba Desemba 18, 2012 maeneo ya Kariakoo Dar es Salaam waliiba Sh milioni 150 mali ya Mire Artan Ismail,” alidai Kongola.
Washitakiwa walikana kuiba fedha hizo na upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kesi.
Kongola alidai hakuwa na kipingamizi kwa washitakiwa kupewa dhamana lakini aliomba mahakama izingatie kifungu cha sheria namba 148 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinachozungumzia masharti ya dhamana.
Hakimu Mchauro alisema sheria kuhusu dhamana inasema kwamba washtakiwa wanaotuhumiwa kwa wizi wa fedha wanatakiwa kuwasilisha mahakamani fedha taslimu ambazo ni nusu ya fedha zilizoibwa.
Washitakiwa katika kesi hiyo wanadaiwa kuiba Sh milioni 150 na nusu ya fedha hizo ni Sh milioni 75 kiasi hicho cha fedha kinagawiwa kwa washitakiwa wote watano.
Kwa maana hiyo kila mshitakiwa anatakiwa kuwasilisha Sh milioni 15 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
“Washitakiwa mtadhaminiwa kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye kuaminika, kila mmoja atasaini dhamana ya Sh milioni tano, kila mshtakiwa atasaini dhamana ya kiasi hicho cha fedha na kila mmoja atawasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni 15,”alisema hakimu.
Washitakiwa wanne waliweza kutimiza masharti ya dhamana isipokuwa mshitakiwa wa tano, Koplo Kelvin Mohammed ambaye alirudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Kesi itatajwa tena Machi 27 mwaka huu.
Hatua ya kupandishwa kizimbani mahakamani hapo imekuja baada ya askari hao watano kufukuzwa kazi kutokana na tukio hilo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Suleiman Kova, askari hao walihusika katika kuwakamata watuhumiwa na vilelezo, baada ya majambazi kupora Sh milioi 150 Desemba 14 katika eneo la Kariakoo.
Majambazi walipora fedha hizo katika duka la kampuni ya Artan Ltd. Kwenye makutano ya barabara za Mahiwa na Livingstone.
Chanzo: Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment