Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa
 Wakati Kamati za Kudumu za Bunge zinatarajiwa kuanza kukutana na kutekeleza majukumu ya kibunge jijini Dar es Salaam kuanzia Machi 18, tayari kampeni za chinichini zimeshaanza kwa baadhi ya wabunge ambao wangependa kuwa wenyeviti wa kamati hizo mpya.

Vikao vya kamati hizo vitaanza mara baada ya kukamilika kwa uundwaji wa Kamati Mpya za Bunge pamoja na uchaguzi wa wenyeviti wa kamati hizo utakaofanyika kesho.

Taarifa za ndani zisizo rasmi zinaeleza kuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu wamebaki katika Kamati ya Mambo ya Nje ambayo Lowassa alikuwa Mwenyekiti na Zungu, Makamu wake.

Taarifa hizo zilieleza kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge, Brigedia Mstaafu Hassan Ngwilizi amepangiwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambayo imemegwa kutoka Kamati ya Mambo ya Nje.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali(PAC), John Cheyo, taarifa zinadai watakuwapo katika kamati hiyo moja ya PAC.

Habari zaidi zilizopatikana jana zilieleza kuwa wabunge wa CCM wamepanga kukutana leo saa tisa alasiri ili kupanga mkakati wa uchaguzi wa wenyeviti.

Mwishoni mwa mkutano wa 10 wa Bunge mwezi uliopita, Spika wa Bunge, Anne Makinda alitangaza mabadiliko ya kamati hizo, huku akiifuta Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Zitto.

Kutokana na mabadiliko hayo, shughuli za POAC sasa zitafanywa na PAC .

Taarifa ambazo gazeti hili ilizipata jana zinaeleza kuwa majina ya wajumbe wa kamati hizo mpya yanatarajiwa kubandikwa leo katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam.

Imeelezwa kuwa wabunge wengi wamekuwa na mshawasha wa kutaka kujua wamepangwa katika kamati gani hasa wale waliokuwa katika Kamati ya POAC na ile ya Nishati na Madini iliyovunjwa kutokana na kuhusishwa na masuala ya rushwa.

Kamati nyingine iliyofutwa ni ile ya Sheria Ndogo ambayo imeundwa Kamati ya Bajeti, Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na ile ya Ulinzi na Usalama.

Kwa mujibu wa Spika Makinda, majukumu ya kamati mpya ya bajeti ni kufuatilia utekelezaji wa bajeti ya Serikali na sera za fedha pamoja na kuainisha na kupendekeza vyanzo vya mapato ya Serikali na kufuatilia mwenendo wa uchumi.

Chanzo: Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top