TAIFA STARS YAINGIA KAMBINI KUIWINDA MOROCCO
Timu ya taifa ya mpira wa miguu Tanzania,Taifa Stars imeanza kambi wikiendi iliyopita ambapo wachezaji 14 kati ya 23 walioitwa wameripoti na kufanya mazoezi leo asubuhi chini ya Kocha Kim Poulsen.



Wachezaji walioripoti ni nahodha Juma Kaseja kutoka Simba na msaidizi wake Aggrey Morris wa Azam, Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Nassoro Masoud Cholo (Simba), Shomari Kapombe (Simba) na Salum Abubakar (Azam).



Wengine ni Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Mrisho Ngasa (Simba) na Simon Msuva (Yanga).



Wachezaji Hussein Shariff, Issa Rashid na Shabani Nditi ambao timu yao ya Mtibwa Sugar jana ilicheza mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) mjini Turiani wataripoti kambini leo jioni.



Kikosi hicho kitakamilika Jumanne asubuhi baada ya wachezaji walio katika kikosi cha Azam nchini Liberia kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho kurejea nchini. Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemorasi ya Congo (DRC) wanatarajiwa kutua nchini kesho usiku.

WAANGOLA KUCHEZESHA MECHI YA STARS

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeteua waamuzi kutoka Angola kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas).



Mechi hiyo ya kundi C itachezwa Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ivory Coast ndiyo inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne na kufuatiwa na Taifa Stars yenye pointi tatu.



Mwamuzi wa mechi hiyo ni Helder Martins de Carvalho wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Inacio Manuel Candido huku Ricardo Daniel Cachicumi akiwa mwamuzi msaidizi namba mbili. Mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Antonio Muachihuissa Caxala.



Waamuzi hao watawasili nchini saa 1.20 usiku Machi 22 mwaka huu kwa ndege ya Kenya Airways wakitokea Luanda, Angola kupitia Nairobi, Kenya.



Kamishna wa mechi hiyo atakuwa David Fani kutoka Botswana anatarajiwa kuwasili Machi 22 mwaka huu saa 1.45 usiku kwa ndege ya South African Airways.



Naye mtathmini wa waamuzi (referee assessor) Neermal Boodhoo kutoka Afrika Kusini atawasili nchini Machi 22 mwaka huu 1.45 usiku kwa ndege ya South African Airways.

MECHI YA RUVU SHOOTING, YANGA YAINGIZA MIL 62/-

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Ruvu Shooting na Yanga iliyochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 62,228,000 kutokana na watazamaji 10,929.

Viingilio katika mechi hiyo namba 146 iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 14,336,764.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 9,492,406.78.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,289,880.48, tiketi sh. 4,136,390, gharama za mechi sh. 4,373,928.29, Kamati ya Ligi sh. 4,373,928.29, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,186,964.14, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 850,486.06 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 850,486.06.

MABADILIKO SEMINA ELEKEZI COPA COCA-COLA
Semina elekezi kwa ajili ya michuano ya Copa Coca-Cola 2013 iliyokuwa ifanyike Jumanne (Machi 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam sasa imesogezwa mbele hadi Machi 26 mwaka huu.

Uamuzi wa kusogeza mbele semina hiyo umetokana na maombi ya wadhamini, Coca-Cola ambao katika tarehe ya awali watakuwa na shughuli nyingine za kampuni hiyo.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawaomba radhi wajumbe kwa usumbufu wowote utakaokuwa umejitokeza kutokana na semina hiyo kusogezwa mbele.

Hivyo, washiriki wa semina hiyo wanatakiwa kuripoti Dar es Salaam (TFF) siku moja kabla (Machi 25 mwaka huu).

Washiriki hao ni makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar. Pia waratibu wa mikoa wa mashindano ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).

Barua za mwaliko kwa ajili ya semina hiyo tayari zimetumwa kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa.



 CHASAMATA KUFUATILIA MATUMIZI YA FEDHA

CHAMA Cha sanaa za maonyesho Tanzania(CHASAMATA) kimeunda kamati ya  wajumbe sita watakao husika na ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za serikali(PETS) katika wilaya ya ilala hili kubaini mapungufu ya utendaji katika sekta ya Sanaa.

 katibu wa CHASAMATA Dennisi Mango alisema kuwa uteuzi huo ambao umefanywa na wasanii wenyewe mara baada ya kupata mafunzo ya Pets na kuona nani anaweza kufanya kazi hiyo. 
Mango alisema wajumbe hao waliochaguliwa ni Raisi wa shirikisho la sanaa za maonyesho Agnes Lukanga, Mwandishi wa habari kutoka New Habari (2006) ltd Humphrey Shao, Asha Salvado kutoka Sayari Sanaa Group , Irene  lembarati kutoka Jivunie Sanaa Group, Hassan kutema na Hamadi Julius kutoka Ilala.

“kamati hii itakuwa muongozo kwetu kwa kuwa ya kwanza kufanya kazi ya ufuatiliaji wa bejeti katika idara ya utamaduni na matumizi ya fedha za bajeti zilizo tengwa mwaka jana kwa ajili ya shughuli za maonesho ya sanaa kama yalivyo ainishwa katika makablasha ya manispaa” alisema Mango

Kwa upande wake mkufunzio wa mafunzo ya Pets Bakari Mbelemba(Mzee Jangala) aliwataka vijana hao kuwa na moyo wa kazi na kutoogopa vitisho kwani kazi hiyo ni ngumu na inachangamoto kubwa kwa nchi kama hii iliyojaa mafisadi wadogowadogo wengi.

“sitegemei kuona mkirubuniwa vijana wangu na vipesa vidogo vya wanasiasa naomba mkajitume kwa moyo mmoja kwani roho zote za wasanii zipo mikononi mwenu kujua ni jinsi gani fedha za sanaa zinaibiwa na watendaji wa manispaa” alisema Jangala

Aliongeza kuwa mbali na kamati hiyo kila msanii anajukumu la kufuatilia tatizo hili kwani sasa ni wakati wa weredi na sio uzalendo kwenye sanaa kama ilivyokuwa enzi za mwalimu hivyo sanaa itatumika kuwafunda na kuwaelimisha watu waliokaa maofisni wakila fedha za wanyonge.

Mango alisema kuwa mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo wasanii na wadau wa sanaa  yamefadhiliwa na shirikika lisilo la kiserikali la Foundation for Civil society na kushirikina na CHASAMATA.



TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top