SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis kumvua ujumbe wa Baraza Kuu la umoja huo, aliyekuwa mgombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa, Paul Makonda, utata mkubwa umetanda kuhusu uamuzi huo.

Makonda alivuliwa wadhifa huo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu, muda mfupi tangu ateuliwe na Sadifa Oktoba mwaka jana, baada ya kushindwa na Mboni Mhita katika uchaguzi wa UVCCM.

Hata hivyo, wadadisi wa masuala ya kisiasa wanalitafsiri suala hilo kama msuguano wa makundi yanayotajwa kusaka urais wa 2015 kupitia CCM, kwani Makonda anatajwa kuwa mfuasi wa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta wakati Sadifa anadaiwa kumuunga mkono Edward Lowassa.

Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu kuenguliwa kwake, Makonda alidai ni mapema sana kulizungumzia, kwani bado anajipanga ili kutoa taarifa kamili, lakini akamshtumu mwenyekiti wake Sadifa kuwa ana uelewa mdogo, wala si suala la makundi.

“Mimi nilipoteuliwa sikutaka kukubali uteuzi huo haraka, bali nilijipa muda kwanza nitafakari na kupooza hasira za makundi yaliyokuwa yakituunga mkono. Leo kama naondolewa kwa sababu hiyo nikiitwa mtovu wa nidhamu itakuwa ni ajabu,” alisema.

Makonda ambaye alizungumza kwa tahadhari ya kutotaka kujiingiza kwenye malumbano kwa sasa, aliongeza kuwa aliteuliwa kupitia mkutano mkuu, na hivyo mwenye mamlaka ya kumwengua ni mkutano huo.

“Huyu kaniita mwenyewe Dodoma, nikalipwa posho halafu naingia kwenye kikao naambiwa nimevuliwa wadhifa wangu. Nimeamua kuondoka zangu kabisa Dodoma ili nisije kuonekana nina mkono katika mivutano inayoendelea ndani ya UVCCM,” alisema.

Alifafanua kuwa hadi jana mchana wajumbe wa Baraza la UVCCM walikuwa wakivutana na mwenyekiti wao tangu asubuhi, lakini akasisitiza kuwa msimamo wake ni kwamba “mwenye haki akifedheheshwa, mbingu husimama nyuma yake”.

Makonda aliongeza kuwa, CCM haina makundi bali kuna magenge yanayotumia nafasi ya mbio za urais kujionesha kuwa kuna makundi yenye malengo fulani kumbe ni ajenda zao binafsi.
Kuhusu kuhusishwa kwake na kundi la Sitta katika kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015, Makonda alitumia mifano zaidi kumsifu mwanasiasa huyo, na kuhoji ni nani asiyetambua umahiri na uwezo wake katika uongozi.

Alisema kuwa Sitta aliliongoza Bunge la Tanzania na kulipatia sifa kubwa iliyotukuka katika mabunge ya Jumuiya ya Madola, huku akihoji kuna ubaya gani kwake kujivunia mtu kama huyo?
“Hivi hao wanaosema kuna makundi, na kudai mimi namuunga mkono Sitta, ni kwanini wasitambue kuwa anabebwa na sifa na utendaji wake uliotukuka katika kuliongoza Bunge la Tisa? Mimi kujivunia mtu kama huyo kuna tatizo gani?” alihoji.

Makonda alikwenda mbele zaidi na kuwataja Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na yule wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kuwa uchapakazi na uadilifu wao hakuna asiyefurahishwa nao, huku akihoji kuwa, watu wanataka waendelee kujivunia nini katika ufisadi wa Richmond?
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top