TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
RAIS KIKWETE
AHUDHURIA MAZISHI YA BABA
YAKE RAIS
MUSEVENI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete jana februari 24, 2013 aliungana na
mamia ya wananchi wa Uganda katika mazishi ya Mzee Amos Kaguta (97), Baba
wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda, yaliyofanyika katika kijiji cha Rwakitura, Magharibi
ya Uganda.
Rais Kikwete
aliwasili katika mazishi hayo akitokea Addis Ababa, mji Mkuu wa Ethiopia alipohudhuria
Mkutano wa viongozi wa kutafuta amani ya kudumu katika Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo.
Akitoa salamu
zake za rambirambi katika msiba huo, Rais Kikwete alisema kuwa Watanzania wapo
pamoja na ndugu zao wa Uganda wakati huu wa majonzi na kusema kuwa yeye binafsi
anampa pole Rais Museveni na familia yake na kumtaka awe na moyo wa subira
katika kipindi hiki na kumuombea marehemu.
Rais Museveni
alimshukuru Rais Kikwete kwa kufika katika msiba huo ambapo alisema kuwa
Marehemu Mzee Amos atakumbukwa kwa kuithamini elimu ambapo aliwapeleka watoto
wake shule na kwa kufanya mabadiliko ambapo alikubali kufuata njia bora za
ufugaji wenye tija jambo ambalo ni gumu kwa wazee wengi wenye umri wake (97).
Rais Museveni
alitumia fursa hiyo kuwaasa vijana kuwatunza vyema wazazi wao ili waishi muda
mrefu na kulaani tabia ya baadhi ya vijana kuishi kwa kutegemea mali za wazazi
wao badala ya kuzalisha mali yao wenyewe akiongeza kuwa wazee wana hazina kubwa
ya maarifa kutokana na kukumbana na changamoto nyingi katika maisha yao.
Marehemu Mzee
Amos Kaguta alizaliwa mwaka 1916 katika kijiji cha Kabahambi, Kikoni Ntungamo
nchini Uganda.
Rais Kikwete
na ujumbe wake akiwemo Waziri wa Ulinzi Mh. Shamsi Vuai Nahodha waliondoka
kurejea jijini Dar es Salaam baada ya mazishi hayo.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
25
Februari, 2013
0 comments:
Post a Comment