MAOFISA WA FIFA WATUA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO
OFISA Maendeleo wa Kusini mwa Afrika wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ashford Mamelodi amesema FIFA haina mpango wa kufanya mbinu za kijanja ili kupanga safu ya uongozi wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania bali wapiga kura ndiyo wataamua.
Ashford amesema kuwa wanachohitajika wao wakiombwa ushauri au mwongozo na watafanya kwa sababu ni kazi ya ushirikiano na anaamini wajumbe watakaotumwa hivi karibuni kuchunguza suala la uchaguzi kutoka FIFA watatoa mapendekezo mazuri ya kuhakikisha uongozi uimara unawekwa kuchukua nafasi ya uongozi unaoongozwa na Rais wa TFF Leodgar Tenga.
Ofisa huyo wa FIFA amempongeza Rais huyo wa TFF kwa kuwa na maadili ya uongozi kwa kuamini katika kile anachokisema na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano wake na kuacha tabia ya kung’ang’ania madarakani  kwa vipindi vingi zaidi.
 
Katika hatua nyingine Bwana Mamelodi amewataka wadau kuwekeza katika soka hususani kwa vijana wadogo huku akishangaa Waafrika wengi kutaka mafanikio kwa njia za mkato bila kujikita katika uwekezaji.
Ashford Mamelodi amewasili nchini kwa ajili ya kufuatilia shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu nchini huku akimtambulisha pia Msaidizi wake katika ukanda wa CECAFA Patrick Onyango ambaye ni raia wa KENYA.
Kwa upande wa mwenyeji Leodgar Chilla Tenga amesema anashukuru kwa ushirikiano wanaopata kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo ya Mpira wa miguu hapa nchini.
Mamelodi, ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa shughuli za maendeleo nchini Tanzania tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo, pia amekuja kumtambulisha msaidizi wake, Patrick Onyango aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo hivi karibuni.
Wakiwa nchini, wawili hao wanatarajiwa kupata taarifa ya maendeleo ya mradi wa kuweka nyasi bandia kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, baada ya FIFA kuipa Tanzania mradi wa nne (GOAL Project 4) wa kuweka miundombinu kusaidia maendeleo ya mpira wa miguu.
Mwanza ilipata mradi huo baada ya Halmashauri ya Jiji hilo kukubali masharti ya mradi huo ya kulipia nakisi ya fedha zinazolipwa na FIFA, ambazo ni sh. milioni 700. Mradi huo wa kuweka nyasi bandia Nyamagana utagharimu sh. milioni 900, hivyo nakisi y ash. milioni 200 italipiwa na Jiji la Mwanza.
Pia Mamelodi na Onyango watapata taarifa ya maendeleo ya Uwanja wa Gombani uliowekwa nyasi za bandia kwa msaada wa FIFA katika mradi wa GOAL Project 3; na pia kupata mikakati ya maendeleo ya TFF kwa mwaka 2013, ikiwa ni pamoja na kozi na semina mbalimbali zitakazofanyika nchini mwaka huu.
Mamelodi na Onyango pia watapata taarifa ya maendeleo ya uboreshaji wa mashindano ya Copa Coca-Cola baada ya FIFA kuingia rasmi kwenye mashindano hayo mwaka jana kwa kuendesha kozi kwa walimu wa timu za kombaini ya mikoa na waamuzi.
Kwa sasa mashindano hayo yanashirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 17, lakini FIFA inataka yahusishe umri mdogo zaidi ili kuendeleza soka ya vijana na kushirikisha kikamilifu shule. Maofisa hao wataondoka nchini Jumatatu asubuhi.


 SIMBA YAJIGAMBA KUZIKATA NGEBE ZA MTIBWA SUGAR
Kikosi cha Simba
 Uongozi wa Simba umesema kuwa unauchukulia kwa umakini mkubwa mchezo wa ligi kuu tanzania bara  dhidi ya Mtibwa hapo kesho Jumapili.
Afisa habari wa Simba Ezekiel Kamwaga amesema kocha wake amesema ushindi waliopata dhidi ya Prisons umewarudisha kwenye kinyang’anyiro cha kutetea ubingwa wao.
Afisa habari huyo amesema kocha mkuu wa Simba Patrick Liewig hataweza kuwatumia baadhi ya wachezaji kutokana na sababu mbalimbali mathalani Mussa Mudde ambaye amerejea lakini hatakuwemo kikosini kutokana kuwa katika mapumziko kutokana  na kufiwa pia Shomari Kapombe ambaye ametoka kuwa majeruhi na ameanza mazoezi mepesi.
Hata hivyo kwa upande mwingine Kamwaga amesema matokeo ya leo baina ya Yanga na Azam yana umuhimu mkubwa kwao kuliko wakati wowote kwani yatawapa wao nafasi ya namna ya kujipanga kuchukua nafasi za juu za ligi hiyo.
KUOGELEA
 Zaidi ya watoto na vijana 200 wameshiriki katika mashindano ya kuogelea ambayo yamefanyika katika bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika IST iliyoko upanga jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa  Mashindano hayo Najet Ahmed amesema lengo mashindano hayo ni kuibua vipaji vya watoto pia kuwafanya vijana kujishughulisha na michezo kama ajira na sehemu ya mazoezi kwa ajili ya Afya zao.
Mratibu huyo amesema moja ya changamoto kubwa ya mchezo huo ni kukosekana kwa miundo mbinu yenye hadhi ya kimataifa hivyo kuwafanya wachezaji wa tanzania kushindwa kufurukuta katika medani ya kimataifa.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top