TANZANIA VETERANS WAZIDI KUIKOMALIA TFF
KUHUSU KUENGULIWA KWA JAMAL MALINZI
Mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars Bakari Malima Jembe Ulaya na
Madaraka Suleimani mzee wa kiminyio wakiongea na waandishi wa habari
kuhusiana na hali ya sekeseke la uchaguzi linalozidi kufukuta na
kutishia soka la Tanzania kwenda halijojo.
Baadhi ya wadau wa michezo wamesema
kitendo kumuengua JAMAL MALINZI aliyekuwa mgombea URAIS wa TFF kilichofanywa na
kamati ya Rufaa ya shirikisho la kandanda Tanzania TFF ni kukandamiza na
kurudisha nyuma maendeleo ya mchezo wa soka hapa nchini.
Wadau hao kwa kauli moja wamesema wako
tayari kulipeleka suala hilo kwa mahakamani ili kuhakikisha haki inatendeka.
Beki mahiri wa klabu ya Yanga na timu
ya Taifa Stars Bakari Malima ni miongoni mwa wadau waliopendekeza kuwa jina la
Jamal Malinzi linarejeshwa katika orodha ya wagombea ili kupambana na Athumani
Nyamlani ambaye amebaki kama mgombea pekee.
Wadau wengine walioongea na vyombo vya
habari walikuwa Mchezaji wa Zamani Simba
na Taifa Stars Madaraka Suleimani maarufu Mzee wa Kiminyio wamedai maendeleo ya soka hayawezi kufikiwa
kama mizengwe itaendelea katika mchezo huo.
Hassan Mbashiri ambaye ni miongoni
wajumbe wa wanakamati wa kuhakikisha uchaguzi wa TFF unafanyika kwa mujibu wa
sheria na si kuona mpira unaburuzwa huku wadau wakibaki watazamaji tuu.
Hata hivyo katibu mkuu wa Shirikisho
Angetile Osiah amesema hawezi kuyatolea ufafanuzi malalamiko ya wadau kuwa
baadhi ya majina yameondolewa kimizengwe wakati kuna sheria,kanuni na taratibu
zilizotumika kuwaengua wagombea husika.
Baadhi ya wagombea ambao rufaa zao
zimedunda ni Michael Richard Wambura aliyekuwa anawania nafasi ya makamu rais
wa TFF Omari Nkurulo aliyekuwa akigombea nafasi ya Urais TFF.
AZAM TAYARI KUKIPIGA
NA AL NASRI JUBA
Kikosi cha Timu ya Azam
Uongozi wa klabu ya Azam umesema
umejipanga kuhakikksha inaibuka na ushindi katika mechi ya kombe la Shirikisho
la kandanda barani Afrika dhidi ya Al Nasri Juba ya Sudan Kusini ikiwa ni mara
ya kwanza kushiriki katika michuano hiyo mikubwa.
Afisa habari wa klabu ya Azam Jaffar
Idd amesema licha ya kwamba wapinzani wao hawakutoa taarifa mapema ya Ujio wao
lakini wanaisubiri kwa hamu,hapo Jumamosi Februari 16 katika uwanja wa Taifa.
SIMBA KUIVAA RECREATIVO LIBOLO JUMAPILI
Mabingwa wa ligi kuu ya kandanda
Tanzania, Simba ya Dar es Salaam wanataraji kushuka dimbani Jumapili wiki hii
dhidi ya Recreative de Libolo ya Angola katika ligi ya mabingwa barani Afrika.
Mechi hiyo itapigwa katika dimba la
Taifa inataraji kuwa vuta nikuvute kutokana na uimara wa timu zote mbili.
Mwenyekiti wa klabu ya Simba Ismail
Aden Rage amesema wamefanya maandalizi ya kutosha kutoka kwa kocha Patrick
Liewig ambaye anaongoza jopo la ufundi la Wekundu wa Msimbazi.
Klabu ya Simba ilifanya vizuri kwa mara
ya mwisho mwaka 2003 ambapo ilitinga hatua robo fainali.
Simba imewahi kutinga hatua nusu
fainali ya michuano hiyo mwaka 1974 na kutolewa na Mehalla el Kubra ya Misri hata hivyo mwaka 1993 imewahi
kutinga hatua ya fainali ya michuano ya kombe la shirikisho maarufu kama michuano ya CAF dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast.
wakati huo huo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linazitakia kila la kheri timu za Azam, Jamhuri na Simba ambazo
zinaiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la
Shirikisho.
Azam inacheza na Al Nasir Juba ya Sudan
Kusini katika mchezo wa Kombe la Shirikisho utakaofanyika Jumamosi (Februari 16
mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Nayo Jamhuri ya Zanzibar kesho itacheza
na St. Georges ya Ethiopia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika
utakaofanyika Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba. Simba itacheza na Recreativo do
Libolo ya Angola keshokutwa (Februari 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
CAF YASITISHA UKAMISHNA WA HAFIDH ALI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) limesitisha ukamishna wa Hafidh Ali. Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya
Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyokutana Januari 17 mwaka huu
jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa
CAF, Hicham El Amrani kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
ukamishna huo umesitishwa kwa vile hadi sasa Shirikisho hilo halijapata ripoti
ya mechi namba 78 kati ya Comoro na Libya ambayo Ali aliteuliwa kuisimamia.
YANGA, AFRICAN LYON ZAINGIZA MIL 68/-
Mechi namba 119 ya Ligi Kuu ya Vodacom
iliyochezwa juzi (Februari 13 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na
kumalizika kwa Yanga kuibuka ushindi wa mabao 4-0 imeingiza sh. 68,438,000.
Watazamaji 12,147 walikata tiketi
kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh.
15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 16,170,252.45 wakati
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 10,439,694.92.
Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho
kilichovutia watazamaji wengi ambapo 10,982 walikata tiketi hizo na kuingiza
sh. 54,910,000.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni
asilimia 15 ya uwanja sh. 8,222,162.26, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi
sh. 4,933,297.36, Kamati ya Ligi sh. 4,933,297.36, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira
wa Miguu (FDF) sh. 2,466,648.68 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es
Salaam (DRFA) sh. 1,918,504.53.
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA TASMA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya
Michezo Tanzania (TASMA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Februari 10
mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Ushindi waliopata viongozi
waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa
TASMA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia tiba ya wanasoka nchini.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano
wake kwa Kamati ya Utendaji ya TASMA chini ya uenyekiti wa Dk. Mwanandi
Mwankemwa aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo kwa kura 18 dhidi ya 7 za
aliyekuwa Mwenyekiti Biyondho Ngome
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi,
kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia
katiba ya TASMA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya
Uchaguzi ya TASMA chini ya Dk. Paul Marealle na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa
kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF.
Safu nzima ya uongozi wa TASMA
iliyochaguliwa inaundwa na Dk. Mwanandi Mwankemwa (Mwenyekiti), Dk. Nassoro
Matuzya (Katibu Mkuu), Sheky Mngazija (Katibu Msaidizi), Dk. Juma Mzimbiri (Mhazini),
Joakim Mshanga (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF) na Dk. Hemed Mziray (mjumbe wa
Kamati ya Utendaji).
0 comments:
Post a Comment