Makamu  Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar na Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein

Makamu  Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar na Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezindua sherehe za miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM  na kueleza kuwa chama hicho kitaendelea kuwa imara huku akiwashangaa wanaoubeza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. 
Uzinduzi huo ulifanyika leo huko katika viwanja vya Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui ambapo pana historia kubwa ya ASP ambayo iliungana kuzaliwa kwa CCM, uzinduzi ambao ulienda sambamba na ukabidhishaji wa vifaa vya michezo kwa ajili ya mashindano ya mpira wa miguu katika kusherehekea kuzaliwa kwa chama hicho.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa ipo haja kwa wanaCCM kujipanga zaidi ndani ya miaka 36 kwa lengo la kukivusha chama hicho ili kiendeleze wimbi la ushindi katika uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015. 
Dk. Shein alisema kuwa kuna ulazima wa kudumisha Muungano uliopo na kusema kuwa anawashangaa wanaotoa visingizio vya kudai hati za Muungano wakati kitendo cha kuziunganisha Zanzibar na Tanganyika hakikuwa siri.
Alieleza kuwa kwa wale wanaohoji masuala hayo majibu yake yapo na ushahidi upo hadi chumba kilichosainiwa hati hiyo kipo huko katika jengo la Ikulu mjini Zanzibar na kueleza kua kama wanataka uthibitisho zaidi waende UN, huku akieleza haja ya kuulinda na kuuenzi Muungano huo pamoja na viongozi wake waasisi hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati mzee Abeid Amani Karume..
 Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka Wazanzibar watambue kuwa umoja na mshikamano walionao ndio ngao yao huku akisisitiza amani na utulivu nchini na kuwataka wale wote wanaokusudia kuvunja amani na utulivu uliopo sheria zitachukua mkondo wake. ‘Zanzibar si sehemu ya kuonesha misuli”,alisisitiza Dk. Shein. 
Dk. Shein aliahidi kupita katika Matawi yote ya CCM pamoja na Maskani zake kwa lengo la kukiimarisha chama hicho na kuendelea kupata ushindi kwani chama hicho pamoja na viongozi wao wako imara na wako makini. 
Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein aliwahakikishia wanaCCM kuwa CCM itashinda katika uchaguzi ujao wa mwaka 2015 kwani ndani ya chama hicho ushindi ni lazima
Alisema kuwandani ya chama hicho kuna timu nzuri ya uongozi katika kuhakikisha inapata ushindi katika uchaguzo huo huku akieleza kuwa chama hicho kimejipanga kuanzia Mashina hadi Taifa lakini la msingi ni kuimarisha amani na utulivu. 
Dk. Shein alieleza maendeleo yaliopatikana ndani ya Serikali za CCM, kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara katika sekta zote huku akieleza kuwa chama hicho hakina ubaguzi wa rangi, dini, ukabila wala jinsia na kuwataka wanaCCM wasikubali kugawanywa.
Akieleza juu ya mashindano hayo ya mpira wa miguu ambayo yanadhaminiwa na familia ya  Mhe. Mohammed Raza pamoja na  familia ya Ibrahim Makungu, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Wanafamilia hao kwa mchango wao huo mkubwa na kusisitiza kuwa michezo ina historia kubwa katika uanzishwaji wa chama cha ASP na TANU. 
Alitoa nasaha zake kwa washiriki wote wa mashindano hayo kutambua kuwa azma ya mashindano hayo ni kushindana ili kupata ushindi katika mpira huo wa miguu ambao utazishirikisha timu sita kutoka katika mikoa sita Unguja mine na Pemba miwili.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai nae alisisitiza hja ya muuenzi na kuutunza Muungano uliopo  na kueleza kuwa Muungano wa Unguja na Pemba nao umetokana na Muungano uliopo na iwapo ukisambaratika Zanzibar itakuwa mashakani na ndio maana CCM iko imara katika kuhakikisha Muungano unadumishwa.
Alisema kuwa Wazanzibari wamekuwa wakihushishwa katika harakati kadhaa za Muungano ikiwa ni pamoja na kushiriki katika vita vya Kagera kwa kuikomboa nchi yao.
 
Nae,Mohammed Raza ambaye pia, ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, liliopo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja alisema kuwa vifaa hivyo ilivyotoa familia yake pamoja na familia ya marehemu Ibrahim Makungu ni miongoni mwa ufadhili wa mashindano hayo makubwa ya kusherehekea miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM  yatakayoaanza kesho.
Alisema kuwa timu zote za Unguja na Pemba zitapatiwa usafiri pamoja na malazi na vyakula hadi kumalizika kwa mashindano hayo ambayo kiingilio kitakuwa bure na mgeni rasmi katika fainali zake atakuwa Dk. Shein.
Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na viongozi wengine wa CCM. Ambapo pia sherehe hizo zilipambwa na taarabu, nyimbo maalum ya CCM, pamoja na vijana wa Kimasai nao walionesha umahiri wao wa kucheza katika nyimbo zao za asili. Kilele cha Sherehe hizo zitafanyika Mkoani Kigoma Febuari 5 mwaka huu.  


TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top