Balozi wa Marekani nchini Tanzania Alfonso Lenhardt.
 
MAREKANI imeeleza kuvutiwa kwake na mafanikio yaliopatikana katika miradi inayoiendesha visiwani  Zanzibar na kuahidi kuunga mkono miradi mengine ikiwemo miradi mipya ya Changamoto ya Milenia (MCC)

Hayo yamesemwa  na Balozi wa Marekani nchini Alfonso Lenhardt wakati walipokuwa na mazungumzo na Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
 
Balozi huyo alieleza kuwa Marekani inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar na kusisitiza kuwa itaendelea kuiunga mkono katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inayoisimamia ukiwemo mradi mkubwa wa umeme inafanikiwa.
 
Katika maelezo yake, Balozi huyo alisifu juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kupambana na Malaria pamoja na kuimarisha sekta zake za maendeleo huku akieleza jinsi hatua zinazochukuliwa na Ubalozi wake katika kuitangaza Zanzibar nchini mwake kutokana na amani na utulivu uliopo ikiwa ni miongoni mwa hatua za kuutangaza utalii wa Zanzibar.
 
 
Kwa upande wa mradi wa MCC, Mkurugenzi Mkaazi wa Mradi huo nchini Tanzania Bwana Karl Fickenscher, alieleza  maendeleo yaliofikiwa katika  mradi mpya wa umeme kutoka Ras Kiromoni hadi Fumba ambapo tayari ulazaji waya umeshakamilika na uwekaji nguzo pamoja na uwekaji waya kutoka Fumba hadi mtoni umefikia hatua nzuri na kueleza mategemeo ya kazi za mradi huo kumalizika mwishoni mwa mwezi ujao.
 
 
Naye Rais  Shein  kwa upande wake alimueleza Balozi huyo pamoja na ujumbe aliofuatana nao kuwa Zanzibar inathamini sana ushirikiano kati yake na Marekani pamoja na juhudi zake za kuunga mkono miradi ya Zanzibar.
 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top