Mwanablog amefika msibani kwa ajili ya kushiriki mazishi ya ndugu yake (Mbwiga Yabhamba) kijijini Jojo kata ya Santilya Mbeya Vijijini. Hata hivyo, kuna jambo linamvutia kiasi cha kumfanya aanze kuliangalia kwa jicho la pekee. Si jingine zaidi ya utekelezaji wa wosia ulioachwa na marehemu kwa watoto wake. Alisema mambo mawili: kwanza, nataka mnizike jirani na nyumba yangu na mwanandani (ngwenya) uwe katika nyumba yangu. Pili, msinizike katikati kama mnavyozika siku hizi badala yake mnizike kama zamani; mtanichimbia mwanandani na huko kunikalisha katika kiti changu. Hivyo, Kabla ya kufariki, marehemu alinunuliwa kiti chake na kukikagua.
Zifuatazo ni picha na maelezo ya maziko ya marehemu yaliyofanyika siku ya Jumatatu ya tarehe 10.12.2012 na kushuhudiwa na mwanablog. Nakusihi ufuatilie kisha uone falsafa iliyokuwa katika mazishi ya kabila hili na hata Waafrika kwa ujumla hasa kabla ya ujio wa wageni. Kumbuka kuwa mazishi ya aina hii hupatikana mara chache siku hizi katika kabila hili.
Marehemu enzi za uhai wake aliagiza pia kuwa awekewe mwanandani na mwili wake kuwekwa huko. Vijana wanachimba mwanandani kama walivyoelekezwa. |
Mwili wa marehemu unashushwa kaburini tayari kwa mazishi. Wametanguliza miguu. |
Ni mwiko katika kabila hili kumtaguliza miguu marehemu wakati wa kumwingiza eneo la mwanandani. Hivyo, wamelazimika kumgeuza ili atangulie kichwa kama inavyotakiwa, zoezi limefanikiwa, wanamwingiza. |
Mwili wa marehemu umewekwa sehemu ya mwanandani kama yeye (marehemu) mwenyewe alivyoagiza. Vijana wanamuweka vizuri. |
Zoezi la kuuweka vyema mwili wa marehemu ikiwa ni pamoja na kumkalisha kwenye kiti chake kama ilivyoagizwa na yeye mwenyewe (Marehemu)linaendelea. |
Waombolezaji kwa majonzi makubwa wakifuatilia tukio la mazishi ya ndugu yao kwa vile hawatakuwa naye tena. |
Vijana wanaendelea na zoezi la kufukia ingawa baridi ni kali pia. |
Kwa heri ya kuonana Hii ni nyumba ya milele. Kushoto ni nyumba ya marehemu ambako kuna mwanandani. Apumnzike kwa amani. |
Unaweza kuona kufanana au kutofanana kwa namna ya maziko ya kabila hili na maziko asilia ya kabila lako. Kama hujui, mlizikaje, kaulize wazee wachache waliobaki kule mlikotoka. Unaweza kusema pia ni yapi mazuri, yanayofaa kuendelezwa, na yepi yamepitwa na wakati yanayopaswa kuachwa na utakuwa na sababu za uamuzi wako. Lengo la habari hii ni kutaka kukuonesha kuwa Waafrika na Uafrika wetu tumetoka wapi, tuko wapi na pengine tunakwenda wapi.
Kuna mambo mengi yanayotuunganisha na kututambulisha kwa Uafrika wetu.Tatizo letu ni kuona kila kinachofanywa na Mwafrika kimepitwa na wakati hivyo ni kikwazo cha maendeleo ya sayansi na teknolojia hata kama ni mtaji mkubwa kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia hiyo. Tunapenda vya Magharibi zaidi hata kama ni mwiba kuliko vya kwetu. Sasa vinakuja vya Mashariki, naongelea China kwa mfano. Tutavutwa kushoto kulia mpaka lini?
Ifike wakati, kwa dhati kabisa, tuwe jamii huru kifikra inayoweza kuamua na kuyasimamia maamuzi yake. Tusiwe sehemu ya kujaribia mawazo ya watu ambayo yamepitwa na wakati au hayawezi kuishi kwao. Vilevile tusiwe sehemu ya kutupia visivyohitajika kwao nasi kuona ni lulu wakati tukiwaachia vyetu wakijitwalia watakavyo. Wanachota utamaduni wetu wanatuuzia matokeo yake, nasi tunabaki kugombania vivuli vya utajiri wetu. Wao wanabaki kuwa matajiri sisi maskini na umaskini wetu katika nchi zinazonuka utajiri wa kila aina.
Haya yote ni matokeo ya matatizo ya kifkra. Wananchi tubadilike viongozi wabadilike. Kila mtu abadilike. Kama upande mmoja utabadilika basi wananchi wawe wa kwanza. Maana kiongozi ni mwananchi hivyo ni lazima watabadilika. Wewe unasemaje?
Picha na Mwanablog TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment