NA RAMADHANI ALI/MAELEZO 19/12/2012
Wizara ya Afya Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Chanjo GAVI, Shirika la kuhudumia watoto UNICEF na WHO itaanzisha chanjo mbili mpya zinazokinga maradhi ya Kuharisha na Nyumonia kuanzia mwezi Februari mwakani
Akitoa taarifa ya kuanzishwa chanjo hizo kwenye Mkutano wa wadau katika Hoteli ya Bwawani, Naibu Waziri wa Afya Dk. Sira Ubwa Mwamboya amesema lengo ni kupunguza idadi kubwa ya vifo vya watoto vinavyosababishwa na maradhi hayo.
Amesema
watoto wenye umri wa miaka miwili wako katika hatari kubwa zaidi ya
kupata maambukizi ya ugonjwa wa nyumonia na kuharisha na hatimae
kufariki na ndio iliyopelekea Mashirika ya Kimataifa kuanzisha chanjo hiyo ili kuwanusuru watoto na maradhi hayo.
Ameongeza
kuwa lengo la Wizara ni kuwachanja watoto kufikia kiwango cha zaidi ya
asilimia 95 katika kila Wilaya, hivyo amewataka wazazi na walezi pamoja
na wananchi wote kuchukua juhudi na kushiriki kikamilifu kuhakikisha watoto wote wanafikiwa na huduma za chanjo.
Dk
Mwamboya amesema chanjo ni haki ya kila mtoto na kwa kutambua hilo
mwaka 19981 Mradi wa chanjo Zanzibar ulianzishwa rasmi na chanjo dhidi
ya Kifua kikuu, Kifaduro, Dondakoo. Polio na surua zilianza kutolewa.
“Chanjo nyengine ya homa ya ini iliongezeka katika miaka 2002 na chango dhidi ya ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo na kichomi zilizinduliwa mwaka 2009”, aliongeza Dk. Mwamboya.
Naibu
Waziri amesema huduma za chanjo zimechangia kwa kiasi kikubwa kufikia
malengo ya Melenia katika kupunguza vifo na magonjwa yanayozuilika kwa
chanjo miongoni mwa watoto chini ya miaka mitano.
Amesema Wizara ya Afya inathamini juhudi zinazochukuliwa na wadau mbali mbali pamoja na viongozi katika kuimarisha
huduma za chanjo Zanzibar hata hivyo amesisitiza juhudi zaidi
zinahitajika ili kuhakikisha watoto wote wanapatiwa huduma hiyo ambayo
itatolewa bila malipo.
Amewahakikishia wananchi kuwa chanjo hizo ni salama na hazina madhara yoyote na baadhi ya nchi duniani zinaendelea kuzitumia na zimepata mafanikio makubwa ya kuwaepusha watoto na maradhi hayo.
Naibu Waziri amewakumbusha washiriki wa mkutano huo kwamba kiwango cha chango zilizopita kitaifa kimeonyesha kuongezeka lakini zipo baadhi ya Wilaya kiwango chake cha uchanjaji kipo chini ya asilimia 80 .
Amezitaja Wilaya zilizofanya vibaya kuwa ni Mkoani na Micheweni kwa miaka miwili mfululizo, Kaskazini A na Kaskazini B pamoja na Wilaya ya Chake Chake.
Mkuu
wa Kitengo cha chango Katika Wizara ya Afya Dk Yussuf Makame amewaeleza
washiriki wa Mkutano huo kwamba magonjwa ya nyumoni yanaathiri mapafu,
uti wa mgongo na ubongo na husababishwa na bacteria aina ya
Streptococcus.
“Magonjwa
ya nyumonia huenezwa kwa njia ya hewa wakati mtu mwenye vimelea vya
ugonjwa huo anapopiga chafya au kukohoa”, amesema Dk. Yussuf Makame.
Ameeleza chanjo hiyo itatolewa kwa watoto ambao hawajapatiwa chanjo ya aina yoyote na watoto wachanga watakaozaliwa .
Akizungumzia
ugonjwa wa kuharisha , Msaidizi Mkuu wa Kitengo cha chanjo Dk.
Abdulhamid Ameir Saleh amesema maradhi hayo yanasababishwa na virusi vya
Rota na huenezwa kwa njia ya kula ama kunywa maji yaliyochafuliwa na
kinyesi chenye virusi hivyo.
Katika michango yao washiriki wa mkutano huo wamesema takwimu zisizo sahihi zinazofuatwa na mafiasa wa Wizara ya afya zimepelekea kuonekana baadhi ya Wilaya kutofikia viwango vya chanjo zilizowahi kutolewa miaka iliyopita.
Wameshauri kutumika takwimu walizonazo masheha katika chanjo za nyumonia na kuharisha kwani ziko sahihi na zinakwenda na wakati.
Mwisho
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment