Mh. Waziri Mkuu Mizengo Pinda

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amefanya ziara ya ghafla kwa kukagua mashamba ya viongozi wa mkoa wa Katavi kwa kuanza na shamba la Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Rajab Rutengwe.


Pia alikagua shamba la na Katibu Tawala wa Mkoa, Mhandisi Emmanuel Kalobelo. Mashamba yote mawili yako katika kijiji cha Songambele eneo la tankifupi,  kata ya Nsimbo, wilayani Mlele, mkoani Katavi.



Shamba la Mkuu wa Mkoa lenye ukubwa wa ekari tano lilikuwa limepandwa mahindi na linatumika kama shamba darasa wakati lile la Katibu Tawala wa Mkoa lenye ukubwa wa ekari nne na nusu lilikuwa limepandwa mahindi na miembe ya kisasa. Pia kulikuwa na banda la ng’ombe.



Waziri Mkuu alichukua uamuzi  huo jana jioni (Jumatatu, Desemba 17, 2012) mara baada ya kuzungumza na wakazi wa kijiji cha Songambele kwenye kata ya Nsimbo na kuwatangazia amri 10 za kuendeleza mkoa huo na wilaya yao mpya.



Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya tano ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi alisema amelazimika kuandaa amri hizo 10 kwa sababu anatambua kwamba kila mtu anahitaji kula chakula bila kujali kama mtu huyo ni kiongozi wa ngazi ya juu, mwananchi wa kawaida au ni kiongozi wa dini.



“Tumbo halijali wewe ni Waziri Mkuu, mwalimu, Mkuu wa Mkoa au Askofu, njaa ikiuma linataka kulishwa. Kama kila mtu anahitaji kula, basi ni lazima kila mtu alime. Tutakaowasamehe ni watoto, wazee na wagonjwa,” alisema.



Akifafanua kuhusu wale wenye ulemavu, Waziri Mkuu alisema: “Wako walemavu ambao wanaweza kulima, nao pia walime.”



Alisema yeye ameandaa amri 10 za kuharakisha maendeleo ya mkoa na kuzitaja kuwa ni: Kila mtu lazima ale; kila mtu lazima aondokane na umaskini; kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi ni lazima alime; kila mtu awe na ekari moja ifikapo mwaka 2013 na maandalizi ya shamba yaanze mapema.



“Ekari hizi mojamoja ziwe zinaongezeka kila mwaka ekari moja, yaani mwaka 2014 mtu awe na ekari mbili na mwaka 2015 awe na ekari tatu, mkifanya hivyo mtaona matunda yake,” aliongeza.



Akitaja amri nyingine, Waziri Mkuu alisema kila ekari itakayolimwa ni lazima iwe imepimwa kitaalam kwamba ina ukubwa wa hatua 70 kwa 70; ekari hiyo ilimwe kwa sesa na siyo matuta; ekari hiyo ipandwe kwa kutumia mbegu bora, kwa mistari na kwa nafasi wanazoelekeza wataalamu.



“Ni lazima ekari moja ikupe miche 16,000 ya mahindi. Nalisema hili kwa uchungu kwa sababu nimetembea hapa nchini na nje ya nchi na kuona jinsi wenzetu walivyoendelea kutokana na kilimo,” alisema. “Panda ekari yako kutumia mbole ya minjingu mazao sababu yenyewe haihitaji kuongeza mbolea ya kukuzia na tena panda kwa mstari kwa kutumia kamba,” alisisitiza huku akitumia lugha za Kiswahili, Kifipa na Kipimbwe.



Akitaja amri ya nane, Waziri Mkuu alisema ni lazima palizi ifanyike kwa wakati. Alisema wanapaswa kuvuna kwa wakati na kuhifadhi ghalani mazao yao. “Siku hizi mahindi hayakai ghalani, bali yanaishia kwenye magunia, hii hapana, haifai.”



Akitaja amri ya 10, Waziri Mkuu alizitaka Halmashauri za Mkoa huo, kila kijiji kuhakikisha wanatunga sheria ndogondogo za kuwasaidia wananchi kutekeleza amri hizo.



Aliwataka viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo wawe wakulima kwanza ndipo waisimamie Serikali kuona kama inatekeleza yale iliyoyazimia.



Kesho (Jumatano, Desemba 19, 2012) Waziri Mkuu atakwenda kata ya Majimoto ambako atapokea taarifa ya mnada na kisha atazungumza na wananchi.

           

 
            MAPAMBANO DHIDI YA UHALIFU



RPC KATAVI ATANGAZA NAMBA YAKE YA SIMU KWA WANANCHI

                                                                                    

 



KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Dhamiri Kidavashari ameamua kutangaza namba yake kwa wakazi wa wilaya mpya ya Mlele, mkoani humo.


RPC Kidavashari ambaye anafuatana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwenye ziara yake ya jimbo la Katavi, wilayani Mlele, ametumia fursa ya utambulisho kwa wananchi kwa kutangaza namba yake ambayo ni 0769-168-850 ili wananchi wampatie taarifa kuhusu matukio ya uhalifu.



Aliwaeleza wananchi katika kata na vijiji mbalimbali ambavyo Waziri Mkuu amepitia kwamba ulinzi wa nchi na uwepo wa amani unategemea ushiriki wa wananchi na kwamba suala hilo si la polisi peke yake. Aliwasihi wawe wepesi kutoa taarifa pale wanapohisi kuna jambo ambalo si la kawaida.



Katika mahojiano maalum, jana jioni (Jumatatu, Desemba 17, 2012), Afande Kidavashari alisema uamuzi wake wa kutangaza namba ya simu ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya polisi jamii ambayo inatekelezwa Kitaifa.



“Sasa hivi hata ukiingia kwenye mabasi, utakuta namba za Makamanda wa Polisi wa Mikoa zimebandikwa ndani ya mabasi ikiwa ni njia ya kupunguza ukiritimba wa kupokea taarifa kutoka kwa wananchi... pia ni njia ya kuturahisishia mawasiliano na kutuweka karibu na wananchi,” alisema.



Alipoulizwa kama hatua yake hiyo imeleta manufaa yoyote, Afande Kidavashari alikiri kupokea taarifa zilizosaidia binti mmoja asibakwe na vijana wa bodaboda mwishoni mwa wiki iliyopita. “Kuna raia mwema aliona vijana wakimvamia binti mmoja katika eneo moja hapa Mpanda, akanipigia simu, nikatuma askari ambao waliwahi katika eneo la tukio na kumwokoa yule msichana. Vijana wawili walikamatwa na mmoja alikimbia, bado tunamfuatilia,” alisema.



Akitoa mfano mwingine, afande huyo alisema kuna meseji (sms) aliipokea kutoka Ugalla mara baada ya Waziri Mkuu kufanya mkutano katika kata hiyo ambapo kuna mkazi mmoja alionewa na watu wa Kaliua. “Mimi niliituma ile sms kwa RPC Tabora naye akaituma kwa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kaliua (OCD) na wameniarifu kuwa suala hilo tayari limeanza kushughulikiwa,” aliongeza.



Akizungumzia aina ya matukio ya uhalifu yanayotokea mara kwa mara mkoani humo, Kamanda huyo wa polisi alisema mengi ni ya uhamiaji haramu, uvuvi haramu, wizi wa ng’ombe, wizi wa mbao kwenye misitu ya hifadhi na uingizaji wa silaha haramu.
 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top