Wachezaji wa Timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars)
Mbwana Samata (Mwenye jezi ya bluu) akiwa kazini
Tomath Ulimwengu
Henry Joseph
Na Azimio Sote
Bila kina Samata na Ulimwengu inawezekana. Huu ni ujumbe ambao bila shaka uligonga vichwa vya Watanzania wengi jana wakati Timu ya Taifa Tanzania  ilipocheza na jirani zake Timu ya Taifa ya Zambia (Chipolopolo) na kushinda. 

Hii inatokana na sababu kubwa mbili. kwanza, ni jitihada za kila aina zilizofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na hata wadau wengine za kuhakikisha kuwa wachezaji hawa wanajiunga na Timu ya Taifa (Taifa Stars), jitihada ambazo hazikuzaa matunda. Pili, Chipolopolo wakaja, vijana wakacheza, tena wakashinda bila ya akina Mbwana Samata na Tomath Ulimwengu.

Si lengo langu kusema kwamba akina Samata na Ulimwengu waliigomea TFF wala sikusudii kusema kuwa wachezaji hawa hawana mchango wowote na  hawahitajiki katika Timu ya Taifa.

Ninachokiona, na huu ndio mtazamo wangu, ni kuwa tunawahitaji mno na hata kupoteza muda kwa ajili yao kuwafuatilia lakini tunaishia kuwakosa kwa vile tu mwajiri wao hayupo tayari kuwaruhusu. 

Athari ya kuendelea kuwahusudu inaweza kujitokeza kwa wachezaji kwa kujenga imani kuwa wao hawawezi kufanya vizuri bila ya akina Samata. Vilevile wanaweza kuamini kuwa Watanzania hawana imani nao kama ilivyo kwa akina Samata. Kibaya zaidi wachezaji chipukizi wanaweza kukosa nafasi wanapoona wachezaji wanaowategemea nje ya akina Samata hawapewi nafasi kwa vile akina Samata wamejengewa imani zaidi.

Lakini kibaya zaidi ni kuwa kuna michezo walikuwepo na Taifa Stars haikushinda. Tusipokuwa makini tunaweza kuwaona kuwa ni wasaliti kwa vile hawaiwezeshi timu kushinda

Watanzania tujenge imani na wachezaji tulio nao uwanjani. Tijitahidi kuwajengea uwezo  ili waweze kufanya vizuri wawapo uwanjani. Kila mtu awaunge mkono wanapofanya vizuri na kuwapa moyo wanapoteleza maana kuna matokeo ya aina tatu kushinda, kutoka sare na kushindwa. 
Haiwezekani kwa taifa lenye watu zaidi ya milioni arobaini kukosa akina Samata wengine na tena wazuri zaidi. Ni jukumu la wachezaji kujitambua kuwa wanaweza, wakipata nafasi, wahakikishe kuwa wanafanya vizuri zaidi ili pengo la akina Ulimwengu na wenzake lisionekane. 

Watanzania tuwaone akina Samata kama vijana wetu. Tuwatunze. Wakifanya vizuri tuwapongeze wakikosea tuwape moyo. Wakikosa nafasi ya kujiunga na Timu ya Taifa tuone kuwa bila wao inawezekana. 

Picha kwa msaada wa mtandao
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top