Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Said Mwambungu akielekezwa jambo na ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Norbert Mtega. |
Jengo la utawala ambalo bado halijaanza kutumika |
Jengo la hosteli ya wanafunzi ambalo bado halijaanza kutumika
|
Serikali imepongeza uamuzi wa Chuo
Kikuu cha Mt Augostino Tanzania kuanzisha kitivo cha udaktari katika kituo chake cha Songea. Hayo
yalisemwa jana tarehe 15.12.2012 na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma ndugu Said Thabit Mwambungu alipofanya
ziara ya kukagua maendeleo ya chuo hicho kilicho katika eneo la Peramiho. Amesema kuanzishwa chuo hicho ni ukombozi kwa
Mkoa wa Ruvuma ambao awali haukuwa na vyuo vya elimu ya juu.
“Kuanzishwa kwa chuo cha Tiba ni
lulu kwa mkoa wa Ruvuma kwa vile kitapunguza usumbufu kwa wananchi wa ukanda
huu ”alisema Mwambungu.
Aidha, akijibu risala ya chuo
kuhusu tatizo la ardhi kwa ajili ya upanuzi wa eneo la chuo, Mwambungu amewataka
watendaji walio chini yake wakae na uongozi wa chuo kwa ufumbuzi.
Alisisitiza kuwa anaamini liko ndani ya uwezo wao.
“Watendaji kuanzia kijiji kaeni
na viongozi wa chuo kupata ufumbuzi wa tatizo hili nanaamini
hata likiwashinda, ofisi ya Mkuu wa Wilaya itawasaidia” alisema ndugu
Mwambungu.
Akizungumzia tatizo la maji,
amekemea tabia ya wananchi kuharibu mazingira na vyanzo vya maji na kusababisha tatizo la
maji. Amewataka wananchi waache tabia hii mara moja. Akifafanua zaidi amewataka
viongozi wa dini waisaidie serikali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tatizo la
uharibifu wa mazingira na athari zake.
“Nawaomba viongozi wa dini mzungumze
na waumini wenu kuhusu tatizo hili wakati serikali inasimamia sheria kuhusu
waharibifu na uharibifu mazingira” Alisema Mwambungu.
Kwa upande wa umeme alisema
watakaa na pande zote zinazohusika ili kupata ufumbuzi kwa
vile linaigusa serikali pia.
Awali mratibu wa Kitivo cha Udaktari
Peramiho Chuo cha Mtakatifu Agustino Tawi la Songea Padre Dunstan M. Mbano
alisema Padre Mbano alisema chuo kina wanafunzi 39 wa mwaka wa kwanza wanaosoma
masomo ya udaktari ambao wamelazimika kupelekwa kwa muda katika Chuo cha
Ifakara-Morogoro kilicho chini ya Chuo Mama cha Mtakatifu Augustino wakisubiri
kukamilika kwa miundo mbinu. Alisema, hata hivyo, wanafunzi hawa kiutawala bado
wako chini ya Chuo Kikuu cha Mt Augustino Kituo cha Songea. Alisema Kituo cha Songea
kilizinduliwa Novemba mwaka 2011 na kina jumla ya wanafunzi 631. Wanafunzi wa
shahada ya kwanza ualimu kwa mwaka wa kwanza na wa pili ni 592 na wanaosoma
udaktari ni 39.
Padre Mbano alisema ujenzi wa
chuo umegawanyika katika awamu tatu. Awamu ya kwanza ilihusu ukarabati wa
majengo ya iliyokuwa hospitali ya wakoma, nyumba ya Mkuu wa Chuo, jengo la
utawala na hostel kwa ajili ya wanafunzi. Awamu ya pili na tatu zitahusisha
ujenzi wa hostel mbili, ukumbi, maktaba, ,adarasa na nyumba za walimu.
Padre Mbano alisema chuo
kinakabiliwa na changamoto za ukosefu wa umeme, maji na samani na vifaa vya
kufundishia. Kuhusu umeme, alisema zinahitajika shilingi za Kitanzania milioni
178.3 kuufikisha umeme katika eneo hilo na kwa upande wa samani na vifaa vya
kufundishia zinahitajika shilingi za Kitanzania milioni 57.3.
Habari na mwanablog
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment