Shughuli ya kupiga kura kumchagua mchezaji bora wa mwaka 2012 wa BBC imekamilika.
Mshindi wa tuzo hio ambayo hutolewa kila mwaka na shirika la habari la BBC atatangazwa rasmi tarehe 17 mwezi huu.Wachezaji watano wanawania tuzo hilo na ni pamoja na Yaya Toure na Didier Drogba kutoka Ivory Coast, Demba Ba kutoka Senegal, Younes Belhanda wa Morocco na Naodha wa Zambia Christopher Katongo.Wachezaji hao watano wameonyesha mchezo mzuri mwaka huu na wanne kati yao waliongoza vilabu vyao kushinda mataji mbali mbali.
Drogba alitimisha kandarasi yake na klabu ya Chelsea kwa kufunga bao la ushindi lililoipa Chelsea ushindi katika fainali ya kuwania kombe la klabu bingwa barani Ulaya, kwa mara ya kwanza na pia kufunga bao ambalo liliisaidia Chelsea kushinda kombe la FA.
Nani atakuwa mshindi?
Yaya Toure, amekuwa nyota wa Klabu ya Manchester City ambayo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 44, ilinyakuwa kombe la ligi kuu ya Premier ya England.Barani Afrika, Chris Katongo aliongoza timu ya taifa ya soka ya Zambia kushinda kombe la mataifa bingwa barani Afrika. Vijana hao wa Chipolopo waliishinda timu ya taifa ya Ivory Coast kwenye fainali hizo.
Kinyume na, Katongo, Demba Ba, hakuwa na la kujivunia, katika fainali hizo za Afrika, baada ya Senegal kuondolewa kwenye raundi ya makundi, lakini akiwa na klabu yake ya Newcastle, Ba, alimaliza ligi akiwa mfungaji bora katika klabu hiyo iliyomaliza katika nafasi ya tano kwa kufunga magoli 17
Kwa Ujumla wachezaji kumi na mmoja wamewahi kushinda tuzo hili la mchezaji bora wa soka wa BBC.
Jay Jay Okocha kutoka Nigeria ndiye mchezaji wa pekee ambaye amewahi kushinda kombe hili kwa miaka miwili mfululizo mwaka wa 2003 na 2004.
Miongoni wa walioteuliwa mwaka huu, Drogba amewahi kushinda mara moja naye Yahya Toure hakuwa hata miongoni mwa wachezaji bora watano mwaka uliopita.
Christopher Katongo kwa upande wake atakuwa akiwania kuwa mchezaji wa kwanza kutoka kanda ya Afrika Kusini kuwahi kushinda tuzo hili.
Via www.bbc.co.uk
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment