Rais wa Madagascar, Mheshimiwa Andry Rajoelina amewasili mjini Dar Es Salaam mchana wa leo, Ijumaa, Desemba 14 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere mjini Dar Es Salaam ambako ndege iliyomleta Rais Rajoelina ilitua saa sita na dakika 45 mchana, amelakiwa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Rais Kikwete na Rais Rajoelina wamekula chakula cha mchana na wanatarajiwa kuanza mazungumzo rasmi baadaye leo.

Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) amepewa jukumu na viongozi wenzake ndani ya Jumuiya hiyo kukutana na viongozi wa Madagascar kuwaelezea maamuzi ya mkutano wa viongozi hao wa SADC uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Dar Es Salaam.

Rais Kikwete tayari amekutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Marc Ravalomanana, kiongozi wa zamani wa Madagascar aliyeondolewa madarakani na Rajoelina.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, mwanzoni mwa wiki hii, Mheshimiwa Ravalomanana alithibitisha kuwa amekubaliana na maamuzi ya viongozi wa SADC.

Miongoni mwa mambo mengine, viongozi hao wa SADC wanataka viongozi hao wawili wa Madagascar washawishiwe na wakubali kutogombea katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika nchini humo mwakani.
 14 Desemba, 2012.

PICHA NA IKULU TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top