Timu ya Chipolopolo
Mabingwa wa Afrika, Zambia (Chipolopolo) wakiwa na msafara wa watu 32 wanatarajia kuwasili nchini kesho (Desemba 19 mwaka huu). Timu hiyo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 11 kamili jioni kwa ndege ya PrecisionAir ikitokea Lusaka.

Mbali ya wachezaji 24, msafara wa Zambia ambayo inakuja nchini kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars utakuwa na maofisa wengine wanane wakiwemo wa benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Herve Renard aliyeipa timu hiyo ubingwa wa Afrika mwaka jana nchini Gabon.

Wachezaji kwenye msafara huo ni Chintu Kampamba, Chisamba Lungu, Christopher Katongo, Danny Munyau, Davy Kaumbwa, Derrick Mwansa, Evans Kangwa, Felix Katongo na Francis Kasonde.

Given Singuluma, Hichani Himonde, Isaac Chansa, James Chamanga, Jimmy Chisenga, Jonas Sakuwaha, Joshua Titima, Kalililo Kakonje, Moses Phiri, Mukuka Mulenga, Rainford Kalaba, Rodrick Kabwe, Salulani Phiri, Shadrack Malambo na Stoppila Sunzu.

Mechi dhidi ya Taifa Stars itafanyika Jumamosi (Desemba 22 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini Dar es Salaam tangu Desemba 12 mwaka huu chini ya Kocha Kim Poulsen kujiandaa kwa mechi hiyo.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 7,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C, sh. 20,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.

Tiketi zinatarajiwa kuanza kuuzwa siku moja kabla ya mechi katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Uwanja wa Uhuru, Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohio na Samora, Sokoni Kariakoo, kituo cha mafuta cha Ubungo OilCom na Dar Live Mbagala.

Pia tiketi zitauzwa Ijumaa (Desemba 21 mwaka huu) kwenye tamasha la Kilimanjaro Premium Lager kuhamasisha washabiki wa Taifa Stars litakalofanyika kwenye viwanja vya Sigara, Chang’ombe.

ROBO FAINALI KOMBE LA UHAI KUPIGWA KESHO
Robo Fainali za michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom zitachezwa kesho (Desemba 19 mwaka huu) kwenye viwanja vya Karume na Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mtibwa Sugar itaumana na African Lyon kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume katika mechi itakayoanza saa 2 kamili asubuhi. Nazo Azam na JKT Ruvu zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Chamazi kuanzia saa 2 kamili asubuhi.

Mechi nyingine ya robo fainali itakuwa kati ya JKT Oljoro na Simba ambayo itachezwa kuanzia saa 9 kamili alasiri kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. Coastal Union na Ruvu Shooting zitacheza kwenye Uwanja wa Chamazi kuanzia saa 10 kamili jioni.

Nusu fainali ya michuano hiyo itachezwa Ijumaa ya Desemba 21 mwaka huu Uwanja wa Chamazi, wakati fainali na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu zitapigwa Jumapili ya Desemba 23 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

TWFA KUCHAGUA VIONGOZI WAPYA MOROGORO
Uchaguzi wa viongozi wapya wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) unafanyika kesho (Desemba 19 mwaka huu) kwenye hoteli ya Midlands mjini Morogoro.

Kamati ya Uchaguzi ya TWFA ikiongozwa na Mama Ombeni Zavala ndiyo itakayoendesha uchaguzi huo chini ya usimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Wagombea katika uchaguzi huo ni Isabela Kapera, Joan Minja na Lina Kessy wanaowania uenyekiti, Rose Kissiwa (mgombea pekee wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti), Amina Karuma na Cecilia Mkafum (wanawania ukatibu mkuu).

Wengine ni Zena Chande (mgombea pekee wa nafasi ya Mjumbe Mkutano Mkuu wa TFF) na Sophia Charles na Triphonia Temba wanaowania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TWFA. TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top