Upo ukweli ambao labda baadhi ya wanasiasa wa Zanzibar na mashabiki wao hawajathubutu kuwaambia maelfu ya vijana na wananchi wa Zanzibar kuhusiana na kile kinachoitwa “Mamlaka Kamili”. Ukweli huu ni mchungu mno na ukiosogelea kwa karibu unatisha kama sumu kali; ni ukweli ambao hautausikia katika mjadala wa “Muungano”; hautausikia katika mjadala wa kama ni “Serikali Mbili au Tatu”; na kwa hakika hautausikia kabisa katika mjadala huko Visiwani wa “Mamlaka Kamili”.
Ni ukweli ambao hata kama hausikiki bado unapiga kelele! Hata kwa wale wenye kuziba masikio ukweli huu bado unapaza sauti na kupasua anga la historia na kufunua yale ambayo yamefichwa mbele ya Wazanzibari. Ni ukweli kuwa Zanzibar iko katika hali ya amani na utulivu na watu wake wakijisikia wako wamoja leo si kwa sababu nyingine yoyote isipokuwa Muungano.
Muungano ulivyo sasa ni ugonjwa na tiba kwa matatizo ya kihistoria ya Zanzibar. Leo hii ukisikia watu wanazungumzia Muungano hasa kundi fulani huko Zanzibar unaweza kabisa kuamini kuwa Muungano ndio tatizo lao kubwa zaidi. Kwamba Wazanzibari wananyonywa na Watanganyika ati wengine wanasema wananyonywa hadi “tongotongo” inavutia masikio ya vijana wasio na muda wa kupeleleza ukweli; unagusa hisia za watu walioumizwa; na labda unaburudisha nyoyo zilizokata tamaa ya maisha. Lakini hili haliondoi ule ukweli kwamba ni Muungano unaowafanya Wazanzibari wakiongozwa na wale waitwao “viongozi wa dini” kudai “Mamlaka Kamili”.
Muungano leo unaangaliwa kama sehemu ya tatizo; na hili laweza kuwa kweli. Lakini historia ni shahidi mzuri tu kuwa ni Muungano ambao kwa miaka hamsini umefanya yale ambayo utawala wa Kisultani na Ukoloni wa Mwingereza haukuweza kufanya kwa karibu miaka mbili na ushee – kuwaunganisha Wazanzibari kuwa kitu kimoja. Lakini hili ni moja tu; kubwa zaidi ni kuwa Muungano umewapa Wazanzibari nafasi ya kukwepa kushughulikia matukio makubwa matatu ya kihistoria ambayo kama yangeachwa yaendelee kwenye Zanzibar iliyo huru; kuna uwezekano mkubwa tu Zanzibar isingekuwa ilipo sasa na labda Muungano ungekuja kwa namna nyingine kabisa.
Uchaguzi Baraza la Kutunga Sheria wa 1963
Kulikuwa na uchaguzi huo ambao ulikuwa unaandaa Zanzibar kuelekea Uhuru; ni uchaguzi ambao mshindi ndiye ataunda Serikali ya Zanzibar huru. Vyama vikubwa vitatu vya Zanzibar vya wakati huo vilisimamisha wagombea sehemu mbalimbali lakini ni Ushirika wa chama cha ZNP (Zanzibar National Party) na kile cha ZPPP (Zanzibar and Pemba People’s Party) vilishinda kwa kupata viti vingi kulinganisha na ASP (Afro-Shirazi Party). Japo ukweli ulikuwa hivyo hata hivyo watu wengi waliipigia kura ASP kuliko muungano ya ZNP na ZPPP (54.21% ASP, 29.85% ZNP na 15.94 ZPPP). Kimsingi na pasi ya shaka ASP ilikubalika zaidi Zanzibar kuliko vyama hivyo vingine lakini kweli hivyo vingine vilikuwa vimeweka ushirika basi vikapewa jukumu la kuunda Serikali.
Zanzibar ilipopata uhuru wake Disemba 10, 1963 ushirika wa ZNP na ZPPP uliunda Serikali ya kwanza chini ya Waziri Mkuu Sheikh Mohammed Shamte Hamad kutoka chama cha ZPPP. Hata hivyo Waingereza walihakikisha kuwa Zanzibar inabakia chini ya utawala wa Kisultani (kama utawala wa Kifalme lakini Waziri Mkuu akiwa ni Mkuu wa Serikali na Mtendaji). Mpango huu haukudumu hata chembe; kwani karibu mwezi mmoja kamili usiku wa kuamkia siku ya Jumapili Januari 12, 1964 Mapinduzi yaliyopindua Serikali ya Shamte na kuukomesha utawala wa kifalme Zanzibar yalitokea.
Tukio hili kubwa na zito mahali popote pale liliacha mshtuko, maumivu, na machungu makubwa sana. Waliokuwa wanacho waliamka na kujikuta hawana, waliodhania kuwa wanacho hata kile kidogo walichofikiria wanacho kikachukuliwa, na wale ambao walikuwa hawana wakaamka na kujikuta kuwa na wao wanacho! Mizani ya mahusiano kati ya watawala na watawaliwa Zanzibar ilibadilika kwa masaa ishirini na nne tu!
Kosa kubwa watu wanapozungumzia Mapinduzi ni kudhania kuwa waliopinduliwa ni Shamte na Jamshid peke yake; kumbe ukweli ni kuwa ulipunduliwa utawala; mfumo wa utawala uliodumu madarakani kwa karibu karne mbili. Kilichopinduliwa ni mfumo kandamizi ambao uliwagawa Wazanzibar na hata kusababisha wengine wavikimbie visiwa hivyo kabla ya matukio ya wakati wa Mkapa kule Pemba. Tukio hili lilisababisha familia kutengana, waliokuwa na kazi kupoteza, watoto kukosa maisha ambayo waliyadhani watakuwa nayo. Kipo kizazi cha watawala Zanzibar ambacho kiliporwa sahani ya dhahabu ya kulia na wale waliokuwa watoto enzi hizo; leo hii ni watu wazima; ukiwasogelea wanasiasa wanaopiga “kelele mamlaka kamili” usije kushangaa wengine ni watoto na wajukuu wa wale waliopoteza mlo! Au wale wanaodhania kuwa sasa ni zamu yao kutawala.
Tukio hili la mapinduzi halikupata muda kushughulikiwa na Wazanzibari; kwa wanaokumbuka historia muda baada ya Mapinduzi ulikuwa ni muda mgumu zaidi labda katika historia ya visiwa hivyo! Muungano uliotokea chini ya miezi mitatu tu baadaye ulihakikisha kuwa mapinduzi yanadumu. Ukisikia watu wanaapa “kudumisha mapinduzi” usidhani ni maneno tu; au ukisikia watu wanaitwa “maadui wa mapinduzi” usije kudhani wameibuka tu kutoka Tanganyika!
Mauaji Baada ya Mapinduzi
Mapinduzi yenyewe kwa kweli kabisa hayakuwa ya umwagikaji damu mkubwa vile; kwani masaa machache tu baada ya uvamizi wa ghala la silaha. Hata hivyo, masaa baada ya mapinduzi yawezekana ndiyo yalikuwa magumu zaidi kwani kuna ushahidi mkubwa wa kihistoria wa kufanyika mauaji holela ya raia (hasa Waarabu) kulikofanywa na makundi ya watu kama sehemu ya kulipiza kisasi. Idadi ya waliouawa kwa kweli haijulikani kwa uhakika – wapo wanaosema ni mamia ya watu huku wengine wakitaja karibu watu elfu ishirini. Vyovyote vile ilivyo kulikuwa na umwagikaji mkubwa wa damu baada ya mapinduzi yenyewe kitu kilicholeta hofu kubwa miongoni mwa wananchi na kusababisha wananchi wengi hasa wenye asili ya Kiarabu kuamua kuondoka Zanzibar na kutafuta hifadhi nje ya visiwa hivyo.
Yale yaliyotokea baada ya mapinduzi, mauaji, watu kukimbia nchi yao n.k ni matukio ambayo hayajawahi kuchunguzwa na kuangaliwa kwa karibu. Je wale waliokimbia visiwa hivyo kufuatia mapinduzi wana haki gani visiwani humo? Je wale waliouawa na kunyang’anywa mali zao wana haki gani humo? Matukio haya kwa watu wa bara kwa kweli ni mageni; japo harakati za uhuru Tanganyika zilikuwa na matukio yake na misisimko yake (Kesi ya Meru, Suala la Ng’ombe Mwanza n.k) hakuna tukio linalokaribiana kwa ukali, na uzito kama la mapinduzi. Muungano haujatoa nafasi kwa Wazanzibar kuzungumzia hili. Wengi wanalizunguka pembeni lakini hili lipo.
Utawala wa Karume
Mojawapo ya matukio ambayo Wazanzibar hawajapata nafasi ya kupitia na kuyaangalia kwa karibu na yamebakia kama kivuli katika historia ni utawala wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar baada ya Mapinduzi – Mzee Abeid Amaan Karume. Kwa wengine yeye ndiye alikuwa shujaa wa mapinduzi na kwa wengine yeye pia alikuwa ni mtu ambaye ukatili wake hauna mfano. Wengine walikuwa wanamuona kama dikteta fulani hivi.
Ukweli kuwa mapinduzi ya Januari 12, 1964 hayakuongozwa na Karume ni ukweli wa historia. Siyo Karume (wa ASP) au Abdulrahman Mohammed Babu wa Umma ambaye alikuwepo Zanzibar wakati mapinduzi yanatokea. Na ukweli wa historia kwamba mtu aliyejipa ushujaa wa kuongoza mapinduzi hayo John Okello alikuwa ni mtu kutoka Bara (Uganda) ni ukweli ambao hausikiki Zanzibar. Sijui hata kama kuna mtaa mmoja unaoitwa kwa jina la John Okello; na sidhani kuna tuzo yoyote au shukrani yoyote ambayo WAzanzibari – wenye kuamini mapinduzi- wamewahi kumpa John Okello. Lakini sifa zote zinawendea Karume.
Maamuzi yake mbalimbali – Karume – ukiyaangalia kwa karibu unaweza kuona jinsi gani nayo yalichangia namna ya uhasama na hisia hasi baina ya makundi visiwani humo. Kwa wanaokumbuka mauaji yake mwaka 1972 yalimfanya Sultani aliyeko uhamisho kuombea kweli kuwa labda yangetokea mapinduzi mengine ili arudi. Hakukutokea mapinduzi mengine Zanzibar kwa sababu ya Muungano. Huu ni ukweli wa historia.
Matukio haya matatu; na mengine yanayotokana na hayo yanaangaza ukweli kuwa Zanzibar inahitaji kutazamana na historia yake na kupatana nayo. Historia ambayo kwa muda imepewa kinga na Muungano (Tanganyika kwa kweli). Kelele tunazozisikia Zanzibar ni kelele zinazotokana na watu kuwa na adui mmoja – Tanganyika. Tukiwasaidia kuwaondolea adui huyu mwenye kuwanyonya hadi tongotongo Wazanzibar hawa watalazimika tu kutazamana na historia yao, kupatana na kwa vile tayari wameonesha uwezo mkubwa wa kufanya mapatano nina uhakika wataweza kupatanisha makundi yao mbalimbali yenye uhasama wa kihistoria.
Ninawasihi wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Zanzibar wasikubali kamwe wazo la Serikali Tatu; kwani wazo hili lengo lake bado ni lile lile – kuilinda Zanzibar. Watanganyika tumefanya hivyo kwa muda wa miaka hamsini na sasa inatosha. Wazanzibar wamekomaa vya kutosha na nina uhakika wana wanasiasa na wanadiplomasia waliobobea ambao wanaweza kabisa kupatanisha pande mbalimbali zenye maslahi yenye kukinzana.
Hoja ya kwamba ati kuna undugu baina yetu si hoja ya msingi; undugu haung’ang’aniwi. Ndugu yako akikuita mwizi, kila siku analalamika unampora hata vya kula vya watoto wake, ndugu yako mwenye kukusimanga kila akipata nafasi tena kwa matusi na kejeli, kuna wakati unafika unapeana naye mkono wa kwaheri! Yeye aende zake na wewe uende zako! Muungano huu wa sasa hivi na mapendekezo ya Serikali Tatu vyote vinajaribu kulazimisha undugu; kulazimisha umoja, kulazimisha nasaba. Hata tukitengana damu hazitengani! Tumeona Korea ya Kaskazini na Kusini, tumeona Crimea na Russia, tumeona nchi nyingi tu ambazo zimegawanyika huku zikigawana ndugu! Hata Marekani na Uingereza zina ndugu wengi waliotenganishwa na historia! Lakini leo hakuna nchi zenye ushirika wa karibu kama hizi.
Kwa upande wangu, mimi ni muumini wa Serikali Moja – moja ya kwao, moja ya kwetu, tukutane Umoja wa Mataifa! Naupenda Muungano lakini Mungu ameupenda zaidi.
Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com
Fb
0 comments:
Post a Comment